26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

UMASIKINI WAWATESA WASTAAFU UJERUMANI

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA

TATIZO la wastaafu na watu walio na umri mkubwa katika nchi zinazoendelea kuishi maisha magumu ni jambo la kawaida mno.

Hali hiyo inachangiwa na sababu nyingi ikiwamo kutowekeza vya kutosha wakati walipokuwa na nguvu za kufanya kazi, kipato kidogo walichokuwa nacho au kukosa ajira pamoja na umasikini uliopo katika familia zao, ambazo zinashindwa kuwasaidia ipasavyo.

Kundi hili ni kubwa mno katika nchi nyingi zinazoendelea, ambako ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana pamoja na kipato duni ni jambo la kawaida.

Vijana hawa wanapoingia katika maisha ya uzeeni au kustaafu hali inakuwa mbaya zaidi hivyo kusababisha wengi wao, wastani wa maisha yao wanayoishi kufupishwa.

Lakini kama utadhani tatizo hilo haliko katika mataifa tajiri utakuwa unajidanganya, ingawa si la ukubwa ule unaozikabili nchi za Afrika.

Mfano mzuri wa mataifa tajiri, ambako wastaafu wanaonja adha ya taabu na umasikini ni Ujerumani.

Kundi hilo ni lile la wanawake wanaowalea watoto wao peke yao, watu wanaojituma na ambao mara nyingi hufanya kazi kwa mikataba mifupi kutoka mradi mmoja hadi mwingine.

Wengine ni wafanyakazi wa muda mfupi, vibarua na watu ambao pato lao halizidi Euro 400 sawa na Sh milioni moja, wasomi ambao kwa miaka kadhaa walikuwa wakifanya mafunzo kwa mishahara duni.

Hiyo ni sehemu ya orodha ndefu ya watu wanaokabiliwa na hatari ya kuangukia katika hali ya umaskini nchini humo na kwingineko Ulaya na Marekani.

Kwa mfano, ripoti ya hivi karibuni ilionesha kuwa asilimia 1.3 ya wastaafu nchini Ujerumani wamekuwa wakiishi kutegemea ruzuku ya serikali, idadi ambayo inazidi kuongezeka.

Serikali kuu ya Ujerumani imekuwa ikijadili mara kwa mara kuhusu ruzuku maalum kuwasaidia watu waliostaafu ambao licha ya kufanya kazi kwa muda wa miaka 40, malipo yao ya uzeeni hayatoshi kuwawezesha kuishi ipasavyo.

Yeyote yule anayeishi kwa Euro takriban 700 anaangaliwa kuwa ni mtu anayekabiliwa na hatari ya kukumbwa na umaskini.

Wastaafu wanaoishi kwa ruzuku ya serikali wanakuwa na Euro 100 tu kama fedha taslimu mfukoni mwao.

Hali inakuwa mbaya zaidi nyakati za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya, ambapo wakuu wa vituo vya kuwahudumia wazee waliostaafu hujishughulisha kuvipamba kwa taa za rangi rangi na mapambo ya X-Mas na harufu za vitamtam maalum vya sikukuu hiyo.

Lakini pia kuna baadhi ya wazee katika vituo hivyo ambao hawamudu kununua zawadi za X- Mas kwa ajili ya wajukuu wao watakaojitokeza kuwatembelea.

“Tatizo linakuwapo kama kuna watoto, wajukuu na wengineo ambapo tunalazimika kusema kuwa haiwezekani kununua hivi sasa kwa sababu hakuna kitu,” anasema Irina Suchan.

Suchan anaongoza huduma za jamii katika moja ya vituo hivyo vya kuwahudumia wazee kilichoko nje kidogo ya mji wa Bonn.

Karibu thuluthi moja ya wazee 80 wanaoishi katika kituo hicho wanategemea ruzuku, kuanzia fedha wanazopatiwa walemavu wasioona hadi kufikia msaada wa jamii.

Msaada wa jamii ni Euro 100, ambazo mzee hulipwa na ambazo mara nyingi huishia katika ununuzi wa vidonge vya kupunguza maumivu kama vile Aspirin na kuzungumza kwa njia ya simu na mjukuu.

Mbali ya vituo vya kuhudumia wazee, kuna vile vya huduma za jamii, ambako ni mahala ambapo wazee wanakwenda kuchukua fomu kwa ajili ya kutuma maombi yao wanapohitaji hiki au kile mfano shumizi au koti la baridi.

Suchan mara nyingi anawasaidia wazee hawa wakati wanapotaka kujaza fomu hizo.

“Katika hili mara nyingi kunakuwa na mabishano, kuna wanaohoji kuwa nimefanya kazi muda wote, kwanini hivi sasa niambiwe badala ya kuandika nijuacho?

“Mfano mzuri ni pale maombi hayo yanapohusisha fedha za kulipia makazi na kuwatunza wazee. Kwa sababu maombi kama hayo husikika vingine kuliko ningesema kwa mfano tunabidi sasa tujaze fomu ya kuomba msaada wa jamii,” anasema na kuongeza:

“Kwa sababu fomu kama hiyo ni ya aina yake hasa kwa wale ambao hupandisha mori haraka.”

Viongozi wa kituo hicho tu ndio wanaojua nani kati ya wazee anapokea msaada wa jamii.

Kuna mfuko mmoja wa hisani unaojitolea kuwalipia gharama za simu pamoja na zile zinazotokana na mipango ya kuwatembeza wazee.

Suchan aliwauliza kisiri siri watatu kati ya wazee wanaoishi katika kituo hicho kama watakubali kuhojiwa na wanahabari lakini wote watatu walikataa.

“Wanaona haya na wana wasi wasi pia wengine wasije wakajua kwamba wao ni maskini.

“Ndani ya vyumba vyao kuna kitanda na shuka za rangi ya urujuani, viti viwili na mito yenye rangi za kupendeza zinazooana na shuka na ukutani zimetundikwa picha ya watu wanaotabasamu,” anasema mtaalam huyo wa masuala ya jamii.

Mmoja wa wazee ambaye hakuwa tayari kutajwa anaeleza kuwa alikuwa akifanyakazi katika hospitali ya mumewe.

Anasema: “Waliishi muda mrefu mjini Damascus, Syria kabla ya kurejea nyumbani katika miaka ya 70 na wote wawili si mume wala si mke mwenye bima ya maisha ya uzeeni.”

Wanawake ndio wanaoathirika zaidi na hali ya umaskini wa uzeeni.

Kuna wengi miongoni mwao waliokubali kurejeshewa fedha walizochangia katika bima ya uzeeni walipokuwa wanafunga ndoa katika miaka ya 50 na 60.

Ili kuweza kugharimia harusi mwanamke ndie aliyekuwa akirejeshewa fedha kutoka mfuko wa uzeeni.

Sabine Graf,  ambaye ni Naibu kiongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Ujerumani, katika jimbo la North Rhine Westfalia, anasema ingawa wanawake wengi wanaendelea kufanya kazi, hata hivyo bado wanakabiliwa na kitisho cha kuishia katika hali ya umaskini.

“Sehemu kubwa ya wanaokumbwa na hatari ni wanawake, ambao mishahara yao ni haba, kwa hiyo wanachangia kidogo pia katika bima ya uzeeni.

“Mpaka sasa bado mshahara anaopokea mwanamume ni zaidi ya asilimia 20 ya mshahara wa mwanamke.

“Kwa hiyo, mchango haba katika mfuko wa bima ya maisha ya uzeeni ndio chanzo cha malipo haba ya uzeeni,” anasema.

Anasema kuwa wao ndio wanaokabiliwa na hatari ya kuangukia katika hali ya umaskini.

Lakini hata watu wanaojituma wenyewe, wanaohama kutoka mradi mmoja hadi mwingine, wanaofanya kazi za muda mfupi na vibarua wanakabiliwa na hatari ya kuangukia katika hali ya umaskini, sawa na watu wenye familia kubwa au wale wanaowalea watoto wao peke yao.

Sabine Graf anasema wanakadiria theluthi moja ya wastaafu, wake kwa waume watajikuta wakiishi katika hali ya umaskini siku za mbele nchini humo.

“Hicho ni kishindo kwa nchi kama hii ya Ujerumani na balaa kubwa kwa wahusika,” anasema.

Suchan kwa upande wake anaamini atakapokuwa mzee hatoweza kumudu kujilipia gharama za kuhudumiwa katika kituo kama afanyacho kazi.

Hadi atakapostaafu, anaamini Ujerumani haitakuwa tena pengine na uwezo wa kugharimia vituo vya kuwatunza wazee.

Anasema katika vituo kama hivi katika Mkoa wa Ruhr, marafiki zake wanakofanya kazi, asilimia 60 mpaka 70 ya wazee wastaafu wanaishi kwa kutegemea msaada wa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles