24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SAINTPAULIA; UA LA KIPEKEE DUNIANI LINALOPATIKANA TANZANIA

Na MWANDISHI WETU
TANZANIA inatajwa kuwa nchi ya pili duniani kuwa na vivutio vingi vya utalii, ikitanguliwa na Brazil.
Vivutio hivyo ni pamoja na hifadhi za taifa, hifadhi za misitu na uoto wa asili, mapori ya akiba, mapori tengefu, fukwe za kitalii, maeneo ya urithi wa dunia na wanyama pori.
Kupitia sekta ya utalii, hutoa mchango mkubwa katika pato la taifa kwa kuchangia asilimia 17.5 ya vyanzo vyote vya mapato.
Pamoja na mambo mengine, Tanzania imebarikiwa kuwa na ua linalojulikana kwa jina la Saintpaulia katika milima ya Usambara. Ua hili lipo kwenye kundi la hifadhi ya misitu na uoto wa asili, ni kivutio cha pekee katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Amani, lenye rangi ya zambarau asili lakini likipandwa sehemu nyingine yoyote duniani hubadili mwonekano wake.
Pia huota katika baadhi ya maeneo machache ya milima ya Tao la Mashariki, kama Milima ya Kilindi. Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira ya Asili ya Amani, Mwanaidi Kijazi anasema ua la Saintpaulia huwa linapatikana kuanzia Februari hadi Mei, kipindi ambacho watalii hutembelea katika Hifadhi ya Asili ya Mazingira ya Amani.
Anasema kwa kawaida Mei kipupwe huanza hivyo maua ya Saintpaulia hupukutika yote na kuacha majani tu.
“Ua hili hustawi na kushamiri vizuri mno, uhusishwa na wakati wa mfungo wa Kwaresma, pale ambapo Wakristo hukumbuka mateso ya Yesu miaka 2000 iliyopita.
“Katika makanisa ya asili ya zamani, mfano Kanisa Katoliki, Anglikana, Lutheran na mengineyo, kipindi cha Kweresma ni cha rangi ya zambarau, inayoshabihiana na vazi alilovalishwa Yesu Kristo wakati wa mateso na kwa imani zao huiita rangi ya ukombozi,” anasema.
Anasema kuwa Saintpaulia lina umuhimu mkubwa katika mila na desturi za Wazungu, katika nchi za Ulaya, Marekani ya Kusini na Magharibi katika masuala ya kutia moyo au kufariji, huzuni, misiba, changamoto za kifamilia na kutoa pole pindi mtu anapotoka katika mateso.
Kijazi anasema: “Kutokana na uzuri na hali halisi ya ua hilo, tafiti mbalimbali zimefanywa ikiwamo kujaribiwa kupandwa nchi za Ulaya kama Ujerumani, Chuo Kikuu cha Edinburg Uingereza, lakini linapoota hubadilika rangi na kubadili mwonekano wake wa asili ikilinganishwa na lililopo milima ya Usambara. Kutokana na upekee huo, hutumika kama nembo ya Hifadhi ya Mazingira ya Asili ya Amani.
Naye mtafiti wa masuala ya sera mbalimbali kutoka nchini Marekani, Rachel Manguels anasema ua hilo huthaminiwa kutokana na rangi yake, ambayo ni adimu kupatikana kwenye maua mengine.
“Ni muhimu Tanzania ikafanya utafiti wa kutosha kujua ni wapi wanaweza kupata soko ili mtakapo hamasisha wakulima wenu kujikita katika uzalishaji mjue nani mnamuuzia,” anasema Rachel.
Anasema kibiashara ua hilo linaweza kuanza kuuzwa hapa nchini katika makanisa na maeneo mengine ili kujenga soko la ndani kwanza.
Rachel anasema ameona maua kutoka Ulaya mkoani Arusha na jijini Moshi mkoani Kilimanjaro na kuhoji kwanini watu wasilime maua ambayo yapo hapa Tanzania kwa uasilia baada ya kufanya utafiti.
“Maua ya aina hii mengi, lakini familia hii ya Usambara inatofauti na inaumuhimu wake katika jamii zetu, hii rangi ya ua la Usambara ni ya kipekee katika kumtia mtu moyo na kuonesha upendo wa dhati wakati wa huzuni, majonzi au kifo,” anasema Rachel.
Kijazi anataja gharama za kutembelea hifadhi ya Amani kwa mtalii mmoja kutoka nje ya nchi kuwa ni dola za Marekani 10 wakati kwa Mtanzania ni Sh 10,000 huku gharama za watembeza watalii wa nje ikiwa ni dola za Marekani 15.
Anataja kivutio kingine katika hifadhi hiyo kuwa ni mashine ya kusaga unga iliyokuwa ikitumia nishati ya nguvu ya kusukumwa na maji ya mwaka 1986 katika kijiji cha Kisiwani na mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji iliyotumiwa na wakoloni wa Kijerumani katika kijiji cha Chemka.
Kwa upande wake Ofisa Misitu wa hifadhi hiyo, Isack Bob anataja idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo na mapato yaliyopatikana akisema mwaka wa fedha 2015/16 watalii 545 walitembelea hifadhi hiyo na kuingiza Sh milioni 50.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17 watalii 121 wametembelea hifadhi hiyo na mapato yaliyopatikana ni Sh milioni 7.3,” anasema Bob

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles