Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade), imeendelea kuimarisha ulinzi katika viwanja vya Maonyesho ya 38 ya Sabasaba wameimarisha ulinzi katika viwanja vya maonyesho hayo ili kuondoa matukio ya uhalifu.
Katika viwanja vya sabasaba ambavyo kwa mwaka huu ukiingia unaanza kukaguliwa na askari maalumu wakiwa na vifaa vya kielektroniki vya ukaguzi.
Ikiwa ni sehemu ya maboresho katika kitengo cha ulinzi na usalama kwa mwaka huu, waonyeshaji na watu wanaoingia kwa ajili ya kuangalia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa ndani na nje ya nchi, wanaanza kukaguliwa getini kabla ya kuingia ndani ya viwanja.
Katika eneo la mlango wa kuingilia ambapo kuna askari wanne wawili kwa ajili ya kuwakagua wanawake na wawili wengine wanawakagua wanaume.
Askari wanawakagua wanawake kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumika katika maeneo mbalimbali, kwa ajili ya kulinda usalama kwa kuanza kukagua katika maeneo ya mwili.
Pamoja na kusachiwa mwili mzima pia askari hao wanaingiza mashine hiyo katika mapochi, kwa lengo la kuangalia kama kuna vitu vya hatari ambavyo anaweza akaingia nazo ndani ya uwanja huo.
Pamoja na mazingira hayo hivi karibuni Mkurugenzi wa Tantrade, Jacqueline Maleko alikaririwa akisema kuwa maonyesho ya mwaka huu yataongezwa ulinzi kwa lengo la kuyafanya kuwa ya kimataifa zaidi.
Maleko alidai kuwa moja ya mikakati ya Tantrade ni kuboresha maonyesho ikiwemo katika ngazi ya ulinzi, kuwa ya kimataifa zaidi uboreshaji utakaoenda sambamba na kubomoa baadhi ya mabanda na kuyajenga upya yawe na hadhi itakayofanana na maonyesho mengine katika nchi zilizoendelea.