26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yafungua milango uwekezaji sekta ya maji

Profesa Jumanne Maghembe
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe

Na Gabriel Mushi, Dar es Salaam

WIZARA ya Maji imetoa wito kwa wawekezaji binafsi kuwekeza kwenye sekta ya maji nchini ili kuisaidia Serikali katika mikakati ya kupunguza tatizo la maji nchini.

Wito huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara Maji, Bashiru Mrindoko, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo kwenye ushiriki wa maonesho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika Juni 23, mwaka huu.

Alisema Serikali kwa kupitia wizara hiyo imefungua milango kwa sekta binafsi kuwekeza, hata ikiwezekana kwa kutumia maji ya bahari.

“Sera na sheria zipo wazi kabisa, tunawakaribisha… ila changamoto kubwa tunajua ni gharama za uwekezaji, hizi ni gharama ambazo wawekezaji lazima wazirudishe, hivyo ni vyema kutazama pande zote mbili kwa kuwa jambo la muhimu ni kumaliza tatizo la maji nchini.

“Hadi sasa asilimia 86 katika sehemu za mijini wanapata maji safi na asilimia 49 ni vijijini, hivyo bado jitihada zinahitajika,” alisema.

Akizungumzia wiki ya utumishi wa umma, Katibu huyo alisema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuonesha ubunifu wa hali ya juu katika sekta ya maji.

Alisema wizara hiyo ilishinda zawadi hiyo kwa kuonesha ubunifu katika kurahisisha kutoa huduma ya maji.

“Hii ilitokana na ubunifu katika kutumia mifupa ya ng’ombe kuchuja madini ya fluoride uliogunduliwa na Kituo chetu cha Utafiti wa Madini cha Ngurdoto, kilichopo mkoani Arusha.

“Pia ubunifu wa kutumia teknolojia ya kompyuta katika kufuatilia miradi ya maji vijijini,” alisema.

Akifafanua kuhusu ubunifu wa kuondoa madini ya fluoride kwenye maji, alisema wizara hiyo sasa imeweka mikakati ya kutengeneza vifaa na kusambaza teknolojia hiyo katika mikoa ya ukanda wa kaskazini ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na madini hayo.

Alisema madini hayo yakizidi viwango vinavyotakikana kwenye maji husababisha meno kuwa na rangi ya udongo, kuwa na matege pamoja na kichwa kikubwa.

“Madhara haya huwapata hasa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na viwango vinavyotakiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni miligramu 1.5 na kwa upande wa Tanzania imeamua kutumia miligramu 4.

Alisema kwa kuwa teknolojia hiyo ni rahisi, itasambazwa kwa kaya ili ziweze kutengeneza mitambo hiyo kwa ajili ya matumizi ya kuchuja maji ya kunywa na ya kupikia pekee kwa sababu madini hayo hayana madhara katika shughuli nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles