28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ulega akerwa na uvuvi wa kutumia gesi

Anna Potinus

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema ugomvi mkubwa walio nao na wavuvi haramu kwa sasa ni utumiaji wa gesi ambao unaleta madhara makubwa ikiwamo kuharibu mazingira ya baharini ambayo ni mazalia na makulia ya samaki pamoja na kusababisha ulemavu kwa wavuvi.

Ulega amesema hayo wakati akijibu swali bungeni leo Jumanne Novemba 5. Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan King aliyetaka kujua gesi ina madhara gani katika uvuvi wa kuzamia.

“Kwenye kina kirefu cha maji inawezekana nyavu ikakwama kule chini hivyo mvuvi anaweza akatumia gesi kuzamia na kitu kingine kwa baharini maji yanaweza yakakifika hata kwa miguu lakini haja ya gesi inakuwepo pale maji yanapojaa sasa chupa inaharibu kitu gani kwasababu mabomu yanaweza yakategwa bila hata ya chupa,” amehoji.

Akijibu swali hilo Ulega amesema utafiti walioufanya umebainisha kuwa wavuvi wanaofanya uzamiaji wengi wao wanaambatana na shuguli za uvuvi haramu ndiyo maana serikali ikasema itazuia zoezi hilo isipokuwa kwa wale wenye kibali maalumu.

“Ugomvi wetu siyo chupa bali ni matumizi yanayotokana na matumizi ya gesi, tunafahamu katika bahari umbali kwa maana ya kina kilomita 40 mvuvi ni lazima atafute namna ya kumfanikisha kufanya shughuli yake lakini kwa utafiti wetu hapo nyuma ilionekana wazi kwamba waliokuwa wanafanya uzamiaji walikuwa wanaambatana na shuguli za uvuvi haramu ndio maana serikali ikasema itazuia zoezi hilo isipokuwa kwa wale wenye kibali maalum.

“Wavuvi haramu wanaotumia milipuko hutumia mitungi ya gesi kuzamia kwaajili ya kukusanya samaki waliowaua kutokana na milipuko hiyo, athari za milipuko ni pamoja na kuharibu matumbawe na mazingira ya baharini kwenye maji ambayo ni mazalia na makulia ya samaki pamoja na viumbe wengine na hivyo kuhatarisha uendelevu wa rasilimali za uvuvi nchini,” amesema Ulega.

Ameongeza kuwa kwa sasa serikali iko katika kuboresha sheria na kanuni za uvuvi na kwamba wamesikia kilio cha wavuvi wazamiaji na hivyo wanakifanyia kazi endepo sheria hizo zitapitishwa na wanaamini katika mambo yatakayoenda kuboreshwa hilo ni mojawapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles