ELIZABETH HOMBO Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
NI ukweli mchungu. Ndivyo unavyoweza kusema, hasa baada ya Rais Dk. John Magufuli, kukutana na wafanyabiashara huku kila mmoja akieleza vikwazo na ushauri kwa Serikali.
Kutokana na hoja hizo zilizoibuliwa Rais Dk. Magufuli, amejibu mapigo huku akisema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati yake teule yamebaini kuwapo viwanda hewa vilivyokuwa vinaagiza sukari ya viwandani.
Mkuu huyo wa nchi, alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati akihitimisha mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, ambapo wafanyabiashara hao kutoka sekta mbalimbali walitoa maoni yao na changamoto zinazowakabili pamoja na mapendekezo ya kuimarisha biashara hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema Machi 14, mwaka huu alipokea ripoti yenye idadi ya viwanda 30 huku viwanda vinane tu ndiyo vikibainika kuwa na taarifa za kweli katika uagizaji wa sukari.
Alizitaja kampuni zilizoagiza sukari bila kudanganya taarifa zake ni pamoja na kiwanda cha kiwanda cha kutengeneza kinywaji maarufu cha Coka Cola cha Bonite Bottlers, Nyanza Bottling Company Limited (NBCL) na viwanda vya kuzalisha unga wa ngano vya Bakhresa.
Kauli hiyo wakati wa mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, uliobeba maudhui ya ‘Tanzania ya Viwanda na Ushiriki wa Sekta Binafsi nchini’.
“Viwanda vilivyokuwa vinaagiza industrial sugar (sukari ya viwandani) kihalali ni vinane tu, viwanda vingine 22 vimebainika kuwa na makosa, vinaagiza kuliko mahitaji yake.
“Mfano kuna kiwanda ambacho bado hakijakamilika lakini kimeagiza tano 500,000, kumbe kuna viwanda hewa, nilikuwa najua kuna wafanyakazi hewa tu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mahitaji ya sukari ni tani 590 kwa mwaka, mahitaji ya viwandani nchini ni tani 135 huku inayotumika kwa matumizi mengine ni tani 455.
Katika matokeo ya ripoti hiyo Rais Magufuli, alitolea mfano katika uwekezaji wa soko la mafuta nchini, akisema hakuna umuhimu wa kuagiza mafuta nchini ilihali kuna uwezo wa kuzalisha ndani.
“Mahitaji ni tani 150,000 ya mafuta kwa mwaka, uwezo wa kuzalisha ni tani 135,000, mahitaji yanayobakia tunatumia dola kuagiza mafuta hayo nje, ambayo wakati mwingine quality yake ni ya chini, hasara tunayopata ni kupoteza fedha za kigeni ambazo zingefanya kazi nyingine, kupeleka ajira nje na kuua kilimo cha zao hilo,”alisema Rais Magufuli.
“Kwanini tangu uhuru tunaagiza mafuta nje? Why tusiwe na uwezo kuzalisha wenyewe hapa ndani?” alihoji.
Alisema hapa nchini tunazalisha pamba, karanga na mazao mengine yatokanayo na mafuta lakini bado yanaagizwa nje ya nchi na viongozi wa serikali hawalioni hilo.
“Ndani ya Serikali hili hawalioni na hata ndani Bunge kwa sababu kipindi cha mikutano ya Bunge, wafanyabiashara wanahamia Dodoma na kufanya lobbing na bia zitanywewa, mimi nilikuwa mbunge kwa miaka 20 hivyo nafahamu.
“Ndugu zangu kwa kufanya hivi tunaliua taifa letu na ndiyo maana nilipotembelea kiwanda cha mafuta Singida, nililiona hili hivyo mawaziri serikalini wahakikishe wale wanaoagiza mafuta nje wapigwe bei kubwa, ili tuwadiscourage kuwa wanaagiza nje ili viwanda vyetu vya humu vipate soko, atakayenishtaki anishtaki kwa mtu yeyote, Mungu atanisaidia ili wakulima wapate mahali pa kuuza mazao yao,”alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia kuhusu dawa, alisema Tanzania ingekuwa na viwanda vya kutengenezea dawa ingekuwa fursa kwa wafanyabiashara lakini hivi sasa kila kitu kinaagizwa nje.
“Sasa hivi kila kitu tunaagiza hata pampers ambazo pamba tunazo tunaagiza, hawa ndiyo wafanyabiashara tulionao lakini ni wepesi kulalamika kuwa serikali haitengenezi mazingira ya wafanyabiashara,”alisema.
Rais Magufuli pia alizungumzia kuhusu mabomba na nondo ambayo yanatengenezwa hapa nchini, lakini bado pia pale wahandisi kutoka nje wanapokuja nchini kusaini mkataba wa ujenzi anaeleza kuwa atavileta vitu hivyo kutoka nje.
“Unakuta mabomba yanatengenezwa hapa, waziri anasaini mkataba, sasa contractor atayekwenda kuchimba mabomba ya maji atasema atatoa mabomba nje wakati hapa tunayo na yamethibitishwa na TBS.
“Ni safi lakini watu wetu wa serikali hawataki hata kulazimisha kwamba bidhaa zote zitoke Tanzania yaani ‘they are so ignorant’ , hawataki kuconsider kwamba bidhaa zitoke hapa halafu ikikosekana ndiyo waende kuagiza nje,”alisema.
Aliwataka mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni ya wafanyabiashara na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ndani ya wiki moja ili Serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
“Nataka kuwaambia kwa dhati kabisa, Serikali ninayoiongoza haiwachukii wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi” alisema Rais Magufuli.
AGUSIA KIWANDA CHA DANGOTE
Rais Magufuli alisema zipo taarifa kwamba kiwanda cha Dangote kinachotengeneza saruji kimefungwa jambo ambalo si la kweli na kwamba mashine ndiyo imeharibika.
“Katika biashara taifa lolote likiwa linaenda vizuri lazima ipigwe vita, leo (jana) nilikuwa nasoma gazeti mahali fulani la jirani zetu inaelezea dangote amefunga kazi na ameacha kuwekeza kwenye kiwanda cha saruji ni mambo ya ovyo tu, lakini ukweli si hivyo mashine yake ya kutengeneza imeharibika.
“Kwa hiyo katika biashara yoyote kuna vita hata ndani ya familia huwa kuna vita au ukoo, pia taifa na taifa kunaweza kuwa na vita inayohusiana na biashara, hivyo mimi nataka niwaambie Watanzania na wafanyabiashara wengine kutoka nje Tanzania ni mahali pazuri pa kuwekeza,”alisema.
Pia aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge).
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.