24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukweli makontena Bandari

Madeni-KipandeNa Masyaga Matinyi, Dar es Salaam

UTOROSHAJI wa maelfu ya makontena katika Bandari ya Dar es Salaam  ulianza kugundulika miezi ya mwisho ya 2014 ukihusisha bandari kavu (ICDs) na vituo vya kuhifadhia magari yanayoingia nchini (CFS).

Habari za uhakika zinaonyesha utoroshaji huo unatajwa kusababishwa na uamuzi wa kuondoa majukumu ya kushughulikia mizigo kutoka menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam na kuyakabidhi kwa kamati ya watu watano kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), hatua ambayo ilitoa mwanya wa utoroshaji.

Uamuzi huo ulifanywa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA,  Madeni Kipande, kupitia barua yake ya Februari 5, 2013, kumbukumbu namba DG/3/3/06, yenye kichwa cha habari ‘KUSIMAMIA TICTS, ICD’s na CFS’.

Wateule wa Kipande watano waliochukua majukumu ya Bandari ya Dar es Salaam wakati huo ni Mkurugenzi wa Ulinzi, Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Teknohana, Mkurugenzi wa Utekelezaji na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Mtanzania inazo kutoka vyanzo ndani ya bandari, Desemba 29, 2014, aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe, alimwandikia barua Meneja Ukaguzi wa Ndani wa bandari hiyo akimtaka kuzifanyia ukaguzi wa kina ICDs na CFS zote.

Barua hiyo ambayo nakala zilikwenda kwa Meneja Mapato, Meneja Masoko, Meneja Kitengo cha Makontena, Meneja wa Operesheni na Ofisa Mkuu wa Takwimu, ilisisitiza uharaka wa ukaguzi huo  sehemu ya barua hiyo ikisomeka; “Please give this assignment high degree of urgency.”

Baada ya ukaguzi huo, ilibainika kuwa baadhi ya wafanyakazi wa TPA walihusika na utoroshwaji wa makontena, wafanyakazi ambao majina yao yalitajwa   na taarifa nyingine muhimu.

Katika barua ya Februari 17, 2015 kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kwenda kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, wafanyakazi waliotajwa kuhusika walikuwa J. Azaar na S. Mtui (makontena 1,877), Joseph Kavishe (270), Lidya Kimaro na Happy-God Naftali (284),   jumla yakiwa makontena   2,431.

Idadi hiyo ya makontena 2,431 ndiyo iliyotajwa kugundulika wakati Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, alipofanya ziara ya kushitukiza bandarini Dar es Salaam, mwishoni mwa mwaka jana.

Baada ya kupewa ripoti hiyo ya ukaguzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Awadh Massawe, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya  i Kipande kung’olewa, alitoa maelekezo siku iliyofuata Februari 18, 2015 juu ya hatua za kuchukua.

Sehemu ya dokezo kuhusu hatua za kuchukua inasema; “Wahusika wote wasimamishwe kazi mara moja, aidha chukua hatua mara moja kwa wizi huu. Kesi za nidhamu zianze mara moja na nipate taarifa.”

Mbali ya kuchukua hatua hizo na nyinginezo, Agosti 10, 2015, Massawe alitengua uamuzi wa Kipande baada ya kubaini kuwapo usimamizi mbovu.

Katika barua yake ya Agosti 15, 2015 kwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam yenye kumbukumbu namba DG/4/3/02, pamoja na mambo mengine, Massawe alisema: “Itakumbukwa kwamba katika waraka huo (wa Kipande) ilielekezwa kuwa jukumu la usimamizi wa shughuli za siku hadi siku za  utekelezaji katika vituo hivyo utafanywa na kamati maalumu ya Makao Makuu.

“Moja ya majukumu ya kamati hiyo maalumu ilikuwa ni kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji, utendaji na kukusanya mapato. Katika kufuatilia utendaji katika vituo hivyo imegundulika kuwa kamati iliyoteuliwa ikihusisha Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Teknohama, Mkurugenzi wa Utekelezaji, Mkurugenzi wa Sheria na Mkurugenzi wa Ulinzi haikutimiza majukumu yake kama ilivyokusudiwa.

“Kutokana na hali hiyo, ofisi yako inaelekezwa kuendelea mara moja na usimamizi wa vituo hivyo ikiwamo kusimamia shughuli zote za  utekelezaji makusanyo na mapato na shughuli nyingine zote za  utendaji kufuatana na mikataba iliyopo.

“Inasisitizwa kwamba kwa sasa Makao Makuu itahusika na masuala ya  sera na ushauri wa  sheria katika kusimamia vituo hivyo.”

Mapato yanayokusanywa na TPA

Mamlaka ya Bandari Tanzania ina majukumu ya kusimamia na kukusanya mapato ya aina tatu, huku shughuli nyingine zote za ukusanyaji mapato bandarini zikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Aina ya kwanza ya mapato inaitwa Stevedoring, ambayo ni mapato yanayotokana kupakuliwa mzigo kutoka kwenye meli na kuwekwa nchi kavu.

Aina ya pili ni  Shore handling ambayo ni mapato yanayotokana na  kutoa mzigo uliopakuliwa kutoka melini na kuupeleka sehemu ya kuhifadhi (yard).

Aina ya tatu ni wharfage, ambayo ni gharama inayolipwa kutokana na thamani ya mzigo.  Hapa  mteja hutakiwa kuwasilisha nyaraka za mzigo (bill of landing),  kabla ya    taratibu za TRA kufuata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles