24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

UKWELI KUHUSU MAZOEZI NA LISHE

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.


WIKI chache zilizopita nimepata maswali mengi yanayolenga kufahamu uhusiano kati ya mazoezi na matumizi ya virutubisho lishe au nutrition lsuppliments. Hatuwezi kukataa ukweli kwamba katika siku za usoni matumizi ya virutubisho hivi yameongezeka kwa kasi sana. Licha ya kuwapo kwa matumizi na umuhimu wa virutubisho lishe katika masuala mengine, uzoefu na takwimu zinaonyesha kwamba upo uhusiano mkubwa kati ya mazoezi na matumizi ya virutubisho lishe.

Leo tutajadili mambo kumi tunayotakiwa kufahamu kuhusu virutubisho lishe na uhusiano wake na mazoezi.

 

Si lazima kutumia virutubisho lishe

Iko dhana inayojengeka katika jamii kwamba, matumizi ya virutubisho lishe ni lazima ili kuweza kufaidika na mazoezi. Dhana hii imejengeka zaidi katika kundi la watu wanaopenda kufanya mazoezi kwa nia ya kuongeza kiasi cha misuli mwilini. Licha ya ukweli kwamba viko virutubisho vyenye uwezo wa kumfanya mtu kuwa na nguvu hivyo kuweza kufanya mazoezi kwa kiwango cha juu, si lazima kutumia virutubisho hivyo ili kufaidika na mazoezi. Pata ushauri wa kitaalamu ili kupata mwongozo utakaokusaidia kufanya uamuzi sahihi.

 

Si virutubisho lishe vyote ni salama

Ukweli ni kwamba virutubisho lishe kama vile unga wenye protini (protein powder) na amino acids ni salama na husaidia kujenga misuli. Unga wa protini husaidia pia kutibu magonjwa mbalimbali yanayohusiana na utapiamlo. Lakini tunatakiwa kufahamu, si kila protein powder ni salama kutokana na ukweli kwamba, wakati mwingine huchanganywa na kemikali nyingine zisizo salama kwa mtumiaji. Ni muhimu kufahamu kila kitu kilichochanganywa kwenye unga wa protini kwa kusoma maelezo yaliyo andikwa katika kopo au paketi (nutritional information). Ni muhimu pia kuwa na ufahamu kuhusu kiasi cha virutubisho lishe kilicho salama kwa mwili wako.

Kuwa mwangalifu na virutubisho lishe vinavyotumika kuongeza nguvu (pre-workout)
Katika mazoezi virutubisho lishe huweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili. Vile vinavyotumika kabla au wakati wa kufanya mazoezi au pre-workout, na vile vinavyotumika baada ya kufanya mazoezi (post-workout). Nia kubwa ya pre-workout suppliments ni kukupa nguvu na uwezo wa kufanya mazoezi kwa muda mrefu, wakati mara nyingi post-workout suppliments husaidia kujenga misuli na kuchoma mafuta. Pre-work out suppliments nyingi huwa na kemikali kama vile caffeine, arginine na nitric oxide ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa watu wenye matatizo ya moyo na mzunguko wa damu. Lakini pia ni muhimu kuzingatia kiasi unapotumia virutubisho hivi.

 

Kwepa kabisa aina hizi za virutubisho

Wakati mwingine wanamichezo wanaoshiriki mashindano hushawishika na kujikuta wanatumia virutubisho kama vile testosterone, growth hormone na steroids ili kupata nguvu nyingi za ziada. Virutubisho hivi, vingi vikiwa vinatolewa kama sindano si tu haviruhusiwi na mabaraza mengi ya michezo, bali vina madhara chungunzima kiafya. Chukulia testosterone ambayo ni homoni au kichocheo cha kiume. Katika hali ya kawaida mwili hutengeneza kiwango cha kawaida cha kichocheo hiki. Licha ya miili ya wanawake pia kutengeneza testosterone, kiwango cha kichocheo hiki ni kidogo kwa wanawake.

Testosterone husaidia kujenga misuli na ni muhimu kwa afya ya uzazi kwa wanaume. Unapotumia testosterone kama kirutubisho maana yake unauzuia mwili wako kutengeneza testosterone ya asili. Ukitumia kwa muda mrefu mwili wako utashindwa kabisa kujitengenezea testosterone yake wenyewe.

Kwakifupi virutubisho lishe vinaweza kuwa muhimu hususani kwa watu wanaofanya mazoezi kwa kiwango kikubwa na muda mrefu. Virutubisho hivi huwasaidia kuurudisha mwili katika hali ya kawaida baada ya mazoezi na kuuandaa kwa kipindi kingine cha mazoezi. Lakini virutubisho lishe si lazima kwa kila mmoja wetu. Ni muhimu kuwa mwangalifu na kila tunachotumia na kufahamu undani na ufanyaji kazi wa virutubisho lishe vyote tunavyotumia. Nadhani ni muhimu kuwasiliana na wataalamu katika hili.

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia: namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles