NA SHARIFA MMASI
MSANII wa Bongo Fleva nchini, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, amewataka wasanii wa kike wanaoibuka katika soko hilo kutobweteka na kutegemea mteremko ili wasonge mbele.
Shilole anayeendelea kutamba na wimbo mpya wa ‘Sitoi Kiki’, alisema muda mfupi aliokaa kimya bila kusikika, hakufulia kama inavyosemekana, badala yake aliwapa nafasi wasanii chipukizi wa kike ili nao wajitangaze sokoni.
“Kuna muda nilikaa kimya sokoni haikuwa na maana ya kwamba nilifulia kutoa ngoma mpya, badala yake niliwapa nafasi wasanii wa kike wanaoibukia sasa ili nao wajitangaze kwenye soko la Bongo Fleva.
“Binafsi bado sijaridhishwa na kazi zao, kwa sababu huwa napenda kusikiliza kazi za wenzangu kwa kuamini kwamba na wao wanazisikiliza za kwangu pia, lazima wakaze buti ili waendane na mahitaji ya soko la muziki huu,” alisema.