26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

UKWELI BADO UNAHITAJIKA KUTUMBULIWA MKURUGENZI TANESCO

5r5a2366

NA HELLEN KIJO BISIMBA,

WATANZANIA wenzangu naona tumeshauanza mwaka. Wiki hii tayari ni ya pili na kabla hatujajua itakuwa ya tatu na kisha ya 52 na hatimaye mwaka umeisha.

Wiki iliyopita hoja ilikuwa ni kuhusu Tanesco na Ewura kutokana na suala la  bei ya umeme kutaka kupandishwa na baadaye kutumbuliwa kwa Mkurugenzi wa Tanesco.

Swali kubwa ilikuwa je, mkurugenzi huyo alitumbuliwa kwa kuwa ametoa  pendekezo la kupandisha bei au kuna jambo jingine? Baada ya makala ya wiki iliyopita nilipata watu kadhaa walionipigia simu na wengine waliniandikia ujumbe mfupi wa maneno.

Sikuwa na nia ya kuendeleza mjadala lakini kutokana na yale yaliyoletwa mbele yangu, nimeona ninaweza kuangalia upya hoja  lakini kwa kujaribu kuona mifumo yetu na inavyofanya kazi na dhana ya utawala wa sheria pamoja na mamlaka waliyonayo viongozi, lakini pia uelewa wa wananchi kuhusu mambo hayo.

Kwa wale walionijibu kwa njia mbalimbali wapo waliokuwa na maswali kama mimi na wapo waliokuwa na baadhi ya majibu, au ufafanuzi zaidi na wapo waliokerwa na hoja niliyoiibua.

Nikianza na aliyekerwa yeye alinitahadharisha kuwa huenda ninatumiwa. Na pia aliona kuwa mimi naongea tu sijui hata maisha ya huko vijijini na mwisho alisema niwe mwangalifu, kwani kazi yangu ni kubwa sana nisiichanganye na siasa.

Kusema ukweli nakubaliana na huyu ndugu kuhusu kazi yangu kuwa ni kubwa sana, ila kwamba ninatumiwa nasikitika kuwa hajaelewa maana ya kuwa na kazi kubwa sijui utatumiwa na nani.

Lakini pia kwamba nisichanganye kazi na siasa, nilihitaji kujua mstari wa kazi hii kubwa na siasa uko wapi? Ukiwasikiliza wanasiasa wanaongea sana habari za maisha yetu mojawapo ikiwa ni  maendeleo kama vile kuwapo na umeme hadi vijijini, nchi ya viwanda, elimu, sanaa na kadhalika.

Pale wanasiasa wanaposhughulikia haya na nikawa na hoja navyo kwa vile ndio maisha yetu, inakuwa ni kuongea siasa au kuongea maendeleo yetu? Suala la utawala wa sheria nililolizungumzia wiki iliyopita halikuwa hewani, lilihusu maendeleo ya nchi na ndio siasa zenyewe ambazo haziepukiki kwa vile wanaotuongoza ni wanasiasa na wanayoyashughulikia ni sehemu ya siasa kwani tu viumbe vya siasa.

Kwa wale waliojaribu kunisaidia katika maswali yangu, yupo aliyeongeza swali kwa kusema kuwa: ‘Pia mimi nilifika mbali zaidi kwa kujiuliza, hivi haikutosha kwa Rais kusitisha bei mpaka amfukuze? Bila shaka kuna mgongano wa kimasilahi’.

Sikujua mgongano wa kimasilahi ni kwa vipi, lakini hilo ndilo lilikuwa wazo la huyu ndugu. Mwingine alinielezea anavyoelewa vizuri mchakato mzima wa kuongezeka kwa bei ya umeme na bidhaa nyingine za mafuta na gesi ambazo zinasimamiwa na Ewura.

Alieleza kuwa katika suala lililoleta shida katika pendekezo la kuongezwa bei si Ewura wala Tanesco waliokosea, kwani hakuna kinachotoka Tanesco kisifike kwa Katibu Mkuu wa Wizara husika.

Lakini alinikumbusha kuwa katika hili la ongezeko la bei isingewezekana kutangazwa bei bila wizara husika kujua kama si kwa waziri moja kwa moja basi ni kwa katibu mkuu wake.

Vile vile alielezea kuwa palikuwa na mkutano wa wadau kama sheria inavyodai na hii ni kama njia ya kuhitimisha pendekezo la kupandisha bei ambapo wadau mbalimbali walikutana na kujadili na ndio maana pendekezo la awali ambalo lilikuwa ni kuongeza bei kwa asilimia karibu 18 lilirejeshwa na kufikia asilimia nane tu.

Nimeshukuru kupata huu mrejesho lakini  ninaona kuwa bado tuna shida kubwa ya uwazi katika nchi yetu. Pasingekuwa na  maswali na majibu iwapo mamlaka husika zingeweka bayana ilivyokuwa hadi bei ya umeme ikapandishwa na ni kwa vipi mamlaka zilikiukwa hadi ikabidi Waziri wa Nishati aingilie kati.

Pia ingeelezewa ni kwa vipi sheria zimekiukwa na hivyo inabidi waliokiuka sheria wawajibishwe. Kinyume cha hapo inabidi tujiulize maswali na kujijibu wenyewe. Pia zipo sheria ambazo pia kila mtu anaweza kuangalia kufanya tafsiri yake.

Kumbe pangekuwa na uwazi wa masuala haya yasingetupa shida. Sisi wananchi kama nilivyosema wiki iliyopita tunaweza kufurahia bei kutopanda lakini baadaye tukalipa maradufu, iwapo hatuelezwi vilivyo kwanini mamlaka husika itake kupandisha bei na kwanini Serikali ikatae?

Je, hii mamlaka ilikuwa inataka kutuhujumu wananchi na Serikali yetu ikatuhurumia wananchi wake? Kwanini iwe hivyo? Unaona maswali yanazidi kuongezeka kwa sababu ukweli haukuwekwa bayana.

Uwazi unasaidia sana kuondoa minong’ono isiyo sahihi na inaondoa hali ya sintofahamu. Pia wananchi wataweza kuielewa vyema Serikali yao pale wanapoelewa utendaji wake.

Inaweza ikaonekana kuwa wananchi wakaifurahia Serikali au wakailaumu kwa kutokujua pale wanapojua ukweli ni vyema sana, kwani wana mchango mkubwa pia jinsi nchi inavyopaswa kuendeshwa na matunda ya wao kuichagua Serikali yao inayowaletea maendeleo.

Tuliongea kidogo kuwa masuala yasipokuwa wazi pia huweza kujenga hofu kama ambavyo baadhi ya watu walioongea nami walisema nisije nikawataja. Mtu anapohofia kutajwa wakati anaongea suala la kweli na la haki hili ni  tatizo kubwa. Pale mtu anaposema ukweli hana sababu ya kuogopa kwa vile hata neno la Mungu linasema ukiijua kweli itakuweka huru.

Na Rais wa nchi yetu hii hupenda  kusema mara nyingi kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Inatubidi kama jamii ya watu tutafute kupewa ukweli tusikubali kujiuliza maswali na kujijibu wenyewe.

Tukiujua ukweli tuuseme kwa uwazi. Historia ina tabia ya kutoa hukumu kwa wale wasiotaka kuwa wakweli kwenye yale ya kweli. Na ndio maana hadi sasa ukweli kwenye suala hili wanaujua waliotenda na pengine wale waliotendewa.

Sisi wananchi wanufaika tungependa kuupata ukweli ili wanaoifurahia Serikali wajue wanachofurahia na wanaoishangaa Serikali wajue kinachowashangaza.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles