30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UKUTA WAMUUA MAMA YAKE KIBATALA

Na MWANDISHI WETU -MOROGORO

ANNA  Mayunga ambaye ni mama mzazi wa wakili maarufu, Peter Kibatala amefariki duniani baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba yake.

Akiongea na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Wakili Kibatala alisema mama yake alifikwa na umauti wakati akikagua eneo la nyumba yake iliyoko eneo Fokoland, SUA mjini Morogoro.

“Baada ya mvua ilinyesha leo (jana) asubuhi saa mbili aliamua kukagua nyumba kwa kuizunguka ili kuona kama maeneo yetu yamepata madhara, ghalfla ukuta wa nyumba ulianguka na kupoteza uhai wa mama,” alisema Kibatala kwa ufupi

Taarifa zaidi zilizopatikana kutoka Morogoro zilieleza kuwa mvua hizo zilibomoa  nyumba kadhaa huku nyingine zikizingirwa na maji katika maeneo ya Kata ya Mafisa na Kihonda zilizo katika Manispaa ya Morogoro.

Ilielezwa kuwa mvua hizo zilisababisha adha ikiwamo kuziba njia kadhaa mkoani humo pamoja na mafuriko na hivyo baadhi ya wanafunzi walishindwa kwenda shule.

Baadhi ya wakazi maeneo mbalimbali ya mkoani humo walieleza kuwa mafuriko hayo yaliyakumba zaidi maeneo ya Kichangani, Mazimbu, Chamwino, Mbuyuni, Kilakala, Boma na sabasaba.

“Mvua imesababisha shughuli za biashara na hasa maduka katikati ya Manispaa kufungwa  baada ya maji kuingia ndani na kusababisha uharibifu wa bidhaa mbalimbali.

“Madhara mengine ni kuharibika kwa miundombinu ya barabara baada ya kujaa maji. Wananchi walilazimika kuvushwa kwa kubebwa mgongoni kwa Sh1,000

Diwani wa Kata ya Mafisa, Daud Salumu (CCM), alisema nyumba mbili zilizo kwenye kata yake zimebomoka  na nyingine zimezingirwa na maji.

Alisema kila mwaka kata yake inakumbwa na mafuriko hivyo ipo haja kwa halmashauri  kuangalia namna ya kuepuka mafuriko hayo.

Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura), Mkoa wa Morogoro,  Lusingi Mashashi alisema wanashirikiana na halmashauri ya manispaa ya Morogoro kuhakikisha miundombinu yote ya barabara inarekebishwa kwa wakati.

Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Inspekta Shomary Sala alisema eneo la Kihonda polisi walimuokoa mwanafunzi aliyekuwa amesombwa na maji wakati akivuka mto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles