25.4 C
Dar es Salaam
Thursday, January 9, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

UKUTA MIRERANI WANG’OA KIGOGO

Na Masyaga Matinyi – Manyara      |     


IKIWA ni wiki moja sasa tangu gazeti hili lichapishe habari ya uchunguzi, ikibainisha udhaifu wa udhibiti katika migodi ya madini ya vito ya Tanzanite eneo la Mirerani, ambalo Rais Dk. John Magufuli aligiza ujengwe ukuta, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Rashid amesimamishwa kazi.

Ingawa sababu za Rashid kusimamishwa kazi hazijaelezwa, lakini taarifa zisizo rasmi zimedai kuwa miongoni mwa mambo yaliyosababisha ni pamoja na suala la udhibiti wa ulinzi kwenye ukuta huo na kutoa leseni kwa wafanyabiashara wa madini (brokers) kinyume cha utaratibu.

Kabla ya Rashid kusimamishwa kazi na kukabidhi rasmi ofisi juzi, jijiji Arusha, gazeti hili linazo taarifa kuwa aliitwa Dodoma Jumatano iliyopita kujieleza.

Katika uchunguzi wake, MTANZANIA Jumapili lilibaini hakuna udhibiti makini wakati wa kuingia na kutoka ndani ya eneo hilo, hasa kwa wale wanaotumia magari, wengi wao wakiwa ni wamiliki wa migodi (matajiri), wanunuzi wa madini na watendaji wa Serikali.

Zaidi gazeti hili lilibaini vifaa kama Scanner na kamera ambazo zingesaidia katika kuimarisha udhibiti hazijafungwa.

MTANZANIA Jumapili lilifanikiwa kuingia na kutoka ndani ya ukuta zaidi ya mara nane na hivyo kubaini upungufu mkubwa ambao pamoja na mambo mengine, unarahisisha utoroshaji wa Tanzanite na kwamba tatizo hilo limekuwapo kwa muda mrefu na kuliingizia taifa hasara ya mabilioni ya fedha.

Tatizo hilo ndilo lililosababisha Septemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli achukue uamuzi wa kuagiza ukuta huo ujengwe ili kudhibiti vitendo hivyo na baada ya ujenzi wake kukamilika, mapato ya Serikali yatokanayo na mrabaha katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, yaliongezeka na kufikia Sh milioni 714.6.

Mapato hayo ya miezi mitatu yaliyapiku yale ya miaka mitatu mfululizo (mwaka 2015 – Sh milioni 166.8, mwaka 2016 – Sh milioni 71.8 na mwaka 2017 – Sh milioni 147.1) na pengine kama udhibiti ungekuwa mkali zaidi bila shaka yangeongezeka zaidi.

Akizungumzia kusimamishwa kazi kwa Kamishna Msaidizi huyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, alisema: “Ni kweli tumemsimamisha kazi hadi pale suala lake litakapofanyiwa kazi na kukamilika.

“Lakini siwezi kutaja sababu za kumsimamisha kazi, haya ni masuala ya kiofisi zaidi, lakini amesimamishwa, na baadaye taratibu za utumishi wa umma zitafuata.

“Unajua ni lazima sasa watu wabadilike na waache kufanya mambo kwa mazoea, wajue kwamba nchi kwa sasa imebadilika.”

JWTZ  KUTUA

Wakati hali ikiwa hivyo, na pengine kile kinachoonekana ni kukabiliana na changamoto zilizoripotiwa kuhusu udhibiti katika eneo hilo, maofisa na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanatarajia kuwasili leo tayari kuanza kazi ya ulinzi kwenye ukuta unaozunguka machimbo ya madini hayo.

Ukuta huo wenye urefu wa kilometa za mraba 24.5 na urefu wa mita 3 kwenda juu, uliogharimu takribani Sh bilioni 6, ulizinduliwa Aprili 6, mwaka huu na Rais Magufuli.

Baada ya kuwasili leo, askari hao wa JWTZ wanatarajiwa kuanza rasmi majukumu ya ulinzi Jumanne, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli katika hotuba yake ya uzinduzi wa ukuta huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msanjila, alithibitisha kuwasili kwa JWTZ, na kwamba wataanza rasmi kazi ya ulinzi katika maeneo yote ya ukuta huo.

“Wanajeshi wetu watawasili rasmi Mirerani kesho kwa ajili ya ulinzi wa ukuta, ila kazi hiyo itaanza rasmi Jumanne, hata mimi Jumanne ijayo nitakuwapo Mirerani, mambo yapo sawa na tunakwenda vizuri.

“Sasa kama inavyozungumzwa, kuna baadhi ya watu ambao baada ya kukosa vielelezo muhimu ili waweze kuingia eneo la machimbo, wanapanga au kufikiria kuruka ukuta, wajue hilo halitawezekana kabisa baada ya vijana kuingia kazini,” alisema Profesa Msanjila.

 

HALI ILIVYO GETI LA UKUTA

Tangu MTANZANIA Jumapili liripoti kutokuwapo umakini katika ukaguzi getini hapo Jumapili iliyopita, kumekuwapo na ulinzi mkali na masharti kadhaa mapya ambayo hayakuwapo awali.

Miongoni mwa masharti hayo, ni pamoja na kila mtu anayeingia mgodini hapo kuonyesha kitambulisho cha taifa na kitambulisho kinachoonyesha sehemu anayofanya kazi (mgodi) na wamiliki kuonyesha vielelezo vya umiliki wa migodi.

Pia magari hayaruhusiwi kuingia ndani ya ukuta, hivyo watu wenye magari hulazimika kuyaacha nje ya ukuta na kutumia pikipiki au bodaboda zilizopo ndani ya ukuta kwenda kwenye migodi.

Hali hiyo imesababisha huduma mbalimbali za migodini kama maji na chakula kushindwa kuwafikia wafanyakazi wa migodi, hali ambayo inatishia shughuli za uchimbaji.

Katika kutafuta suluhu, Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Manyara (Marema), kiliitisha mkutano wa wadau wote Alhamisi iliyopita, uliohudhuriwa na idadi kubwa ya wamiliki na wachimbaji wa migodi.

Lakini wakati Katibu wa Marema, Aboubakary Madiwa, akianza kutoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano, askari polisi wa kituo cha Mirerani walifika na kutoa taarifa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amezuia usifanyike.

“Wanachama wetu na wadau wengine tunapaswa kutii mamlaka za utawala zilizopo, Mkuu wa Wilaya ameagiza mkutano huu usitishwe mara moja, hivyo tutawanyike mpaka tutakapopeana taarifa nyingine,” alisema Madiwa.

Akizungumza jana, Mhandisi Chaula, alisema ni kweli alitoa maagizo ya kusitishwa kwa mkutano huo kutokana na taarifa za kiintelijensia ambazo zilionyesha dalili za uvunjifu wa amani.

Miongoni mwa mambo ambayo mkutano huo ulikusudia kujadili ni pamoja na kudorora kwa shughuli za uchimbaji, hasa kutokana na hatua ya kuzuia watu wasiokuwa na vitambulisho vya taifa kuingia ndani ya ukuta, ilhali wakiwa na vitambulisho vya migodi wanayofanya kazi.

Lakini kwa siku ya jana hali ilikuwa tete zaidi, watu hawakuruhusiwa kabisa kuingia ndani ya ukuta, hata gari la wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walioitwa baada ya kutokea hitilafu ya umeme kwenye moja ya migodi katika kitabu D, nalo lilizuiwa.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Msanjila, alisema yeye asingependa kuizungumzia, na badala yake alishauri aulizwe Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini na Kamishna wa Madini, Profesa Shukuruni Manya.

Kuhusu gari la Tanesco kuzuiwa, alisema watu waliotoa taarifa walipaswa pia kuwasiliana na Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani kupata kibali cha kupita getini.

Kwa upande wake, Profesa Manya, alisema yupo jijini Dodoma, na kwamba isingekuwa busara kuzungumzia suala hilo, na kuelekeza aulizwe Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima.

Alipopigiwa simu, Ntalima alisema yeye ni Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, lakini si msemaji rasmi, hivyo hawezi kuzungumza lolote, kisha akakata simu.

WAMILIKI MIGODI WAZUNGUMZA

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wamiliki wa migodi ya Tanzanite, Sam Rugemalira, alisema suala la ukuta huo linapaswa kuwekwa wazi na kufafanuliwa zaidi, kwa sababu zimekuwapo taarifa nyingi za upotoshaji kabla na baada ya kujengwa.

“Unajua lazima tuambiane ukweli, matarajio makubwa iliyonayo Serikali katika ukuta huu yanaweza yasifikiwe kwa asilimia 100, na ili ukuta huu ufanye kazi vizuri, ni lazima kila mwenye leseni achangie walau Sh 50,000 kwa mwaka, lakini kugharamia shughuli za ukuta kwa kutegemea ‘production’, tutakwama.

“Uzalishaji umeshuka sana sana, jamani hakuna mawe kama watu wanavyodhani. Mathalan kwa miezi kadhaa sasa ni migodi miwili tu ambayo imetoa mawe (anawataja wamiliki), lakini kwingine kote tunafukia pesa tu kila siku tukiwa na matarajio, sasa Serikali inapaswa kutambua hali halisi ya Mirerani ya leo. Taarifa za uongo kuhusu hali ya hapa zimekuwa nyingi mno,” alisema.

Pia alisema utaratibu mwingine unaochangia utoroshaji wa mawe pale mgodi unapotoa, ni kitendo cha wathaminishaji kutoa makadirio makubwa kuliko uhalisia.

“Kuna watu wana Tanzanite, lakini mpaka hivi sasa tunavyoongea wameshindwa kuuza, kwa sababu unapata madini ya Sh milioni 50, lakini wathaminishaji wanakuandikia thamani ya milioni 200, kwahiyo hata siku ya kulipa mapato ya Serikali, watakukadiria kwa milioni 200, sasa inabidi mtu akae na madini yake.

“Sasa mazingira kama haya kwa kiasi kikubwa yanaweza kuwa kichocheo cha baadhi ya wachimbaji kuamua kuikwepa Serikali na kutorosha madini,” alisema Rugemalira.

Wakati hali ikiwa hivyo, viongozi wa wachimbaji jana kutwa walikuwa wakiendelea na vikao jijini Arusha kujaribu kupata suluhu ya haraka, ili shughuli za uchimbaji ziendelee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles