Aveline Kitomary, Dar es Salaam
Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa soko la Samaki la Feri jijini Dar es salaam limekumbwa na uhaba wa samaki hali inayopelekea bei ya bidhaa hiyo kupanda.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo Alhamis Desemba 27, Ofisa Uvuvi wa Soko hilo, Ahmed Mbaruku amesema kutokana na upepo wa kaskazi kuvuma hali imebadilika dagaa wanapatikana usiku kutokana na mbalamwezi huku samaki wakubwa wanapatikana kwa mshipi huku bei ya samaki kubadilika kulingana na upatikanaji wake.
Amesema asilimia 90 ya dagaa mchele wanapatikana usiku kwasababu sasa hivi ni majira ya kiangazi,samaki wakubwa wanapatikana wachache kwa kuvuliwa na mishipi.
“Bei imepanda ndoo ya dagaa mchele inauzwa Sh. 8,000 kwa sasa wakati mwanzo ilikuwa Sh. 5,000 huku Nguru kilo Moja ni Sh. 15,000 kutoka Sh. 8,000,Changu kwa kilo ni Sh. 9,000 kutoka Sh. 4,500 hivyo bado kunauhitaji mkubwa wa samaki,”amesema Mbaruku.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Wavuvi Wadogowadogo Amiri Nsoko, amesema uhaba wa vifaa pia unachangia upatikanaji mdogo wa samaki kwani wavuvi wengi wanatumia mtumbwi na maboti madogo.
“Licha ya mabadiliko ya hali ya hewa pia zana zisizoendana na teknolojia ya kisasa zinachangia samaki kuvuliwa wachache,kwani samaki waliopo bahari ya Hindi wakivuliwa vizuri wanaweza hata kutumika nchi nzima,”amesema Nsoko.
Kwa upande wake mmoja Wafanyabiashara wa Samaki Jafari Miraji amesema hali ya biashara sio nzuri sana kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo hivyo kusababisha kutokuwapo kwa bei maalumu ya kuuzia kwani hubadilika kila siku kulingana na upatikanaji wake.