30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

UKITAKA KUBADILI MAISHA YAKO, ANZA KUBADILIKA WEWE KWANZA – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

KULALAMIKA kuwa maisha ni magumu wakati hakuna juhudi zozote unazofanya kuhakikisha unakabiliana na hali hiyo ni mawazo mfu.

Utaishia kulia tu, lakini hakuna cha maana utakachofanya kwenye maisha yako. Wengi waliofanikiwa kwenye maisha yao walijaribu kufanya vitu ambavyo wengine walidhani haviwezekani nao wakafanya na kuwatajirisha.

Kuishia kurusha lawama kwa wazazi kunakusaidia nini? Ni suala la kuchukua hatua.

 

TAZAMA FURSA KWA JICHO PANA

Mwenye kutaka kufanikiwa, hutazama fursa kwa jicho pana. Haangalii tu afanye nini ili afanikiwe, bali hutazama zaidi ya wengine. Ukitazama walipoishia wengine itakuwa rahisi zaidi kufanikiwa.

Mfano, leo hii wapo vijana wanaookota makopo ya plastiki barabarani na kuyauza. Unaweza kufikiri zaidi kwa kutafuta masoko, lakini pia ukaanzisha kituo chako cha kukusanya makopo hayo kwa bei kubwa zaidi ya wengine ili nawe ukayauze.

Maana yake ni kwamba, ikiwa wanauza kwa watu wengine kwa bei fulani, ukaongeza bei kidogo, bila shaka wengi watakusaka popote ulipo kwa sababu ya ongezeko la bei.

Unaweza kuidharau biashara hiyo, lakini kwa kuangalia kwako kwa jicho la ziada, utaweza kuongeza kipato chako.

 

GEUZA MATATIZO KUWA FURSA

Wakati fulani matatizo huwa chanzo cha mapato. Acha kuhuzunika na kutazama changamoto mbalimbali kama maumivu kwako, umizwa na matatizo kwa kuchukulia kama fursa kwako.

Wakati mwenzako anaangalia kwa jicho la huruma, watu fulani wanaoteseka kwa kukosa viatu, wewe tumia fursa hiyo kwa kutengeneza viatu vya oda kwa bei nafuu kisha nenda katatue tatizo hilo kwa kupata faida.

Wapo watu vijijini mpaka leo hii wanavaa nguo za hovyo, nyingine zimechanika ni kwa sababu wananunua kwa bei mbaya. Shtuka. Kwako iwe fursa. Nenda kakusanye nguo za mitumba za bei rahisi na uzipeleke, utatengeneza fedha.

 

ANGALIA MATUMIZI YAKO

Unaweza kuwa unawaza sana, hivi kwanini sipigi hatua? Hivi ni kwanini sifanikiwi? Ndugu zangu hata kama unalipwa kiasi kidogo kwa kiwango gani, kama hutakuwa makini na matumizi yako ni kazi bure.

Kanuni za mafanikio zinatutaka kuwa makini katika kiwango cha juu kabisa kuhusu matumizi yetu. Je, unayajua matumizi ya muhimu ni yapi? Unajua matumizi ambayo si ya lazima?

Ndugu zangu, lazima ujue mahitaji muhimu ya kila siku na yale ambayo utayafanya tu pale unapokuwa na fedha za ziada.

Mfano lazima ule, unywe maji, uvae, ulipe kodi ya nyumba, nauli za usafiri na mengine kama hayo. Manunuzi ya nguo, saa, manukato na vitu vingine vinapaswa kufanyika kwa utaratibu maalumu.

Usiwe mtu wa kununua vitu kwa sababu tu umeviona, kila kitu kifanywe kwa mipango. Heshimu mipango yako. Usikurupuke kununua kitu kwa sababu tu umekiona.

Fedha usipoiheshimu, kwa hakika hata wewe haitakuheshimu kabisa na badala yake itakuharibia maisha. Anza na kuheshimu fedha.

 

UAMINIFU NI SILAHA

Kuna watu mpaka leo hii hawajui kuwa uaminifu ni silaha kubwa ya mafanikio. Unaweza kujiona mjanja, pale mtu anapokukopesha fedha zake na kuanza kumzungusha, lakini ujue unaharibu maisha yako mwenyewe.

Watu wakishajua kuwa wewe si mwaminifu, sifa hiyo itasambaa na wengine hawataweza kukusaidia kwa sababu tayari wanajua kuwa huaminiki. Kamwe usikubali kujiweka kwenye hali hiyo.

Heshimu mali za wengine, wanaokusaidia ni muhimu sana. Kumbuka huishi kwenye dunia ya peke yako. Maisha ni watu. Si wewe peke yako. Utaweza kubadili maisha yako kwa wewe kuanza kubadilika.

Nakutakia mafanikio mema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles