24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa: Zitto usituingilie

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

Na Patricia Kimelemeta

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kuacha kuwaingilia kwenye mambo kwa vile hayamhusu.

Kauli ya Ukawa imekuja siku moja baada ya Zitto kusema hana uhakika na wala haamini kama umoja huo utakuwa endelevu hadi uchaguzi mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara ya kwanza vyama vya upinzani kuungana kisha kugawanyika.

Alisema siku zote Watanzania wanapenda kuwa na upinzani imara ambao watu wanaweka maslahi yao pembeni na kuungana dhidi ya chama kilichopo madarakani.

Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema haoni umuhimu wa kujibizana na mtu aliye nje ya umoja huo kwa sababu hawezi kujua dhumuni la kuungana.

“Hatuhitaji kuumiza kichwa wala kujibizana na mtu aliye nje ya Ukawa, kwa sababu hajui ulianzishwa kwa lengo gani, atabaki kutabiri kitu ambacho hana uhakika nacho, bali anazungumza kutokana na matakwa yake.

“Kwanza si msemaji wa Ukawa, tunashangaa hata kukaa na kuanza kujadili suala lisilomhusu, ni nani na ninyi waandishi wa habari mnapaswa kumuuliza maswali wakati akizungumza hayo,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Ukawa haufanyi kazi kwa kufuata maneno ya barabarani, bali wanafanya kazi kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kusikiliza maoni ya wananchi nini wanataka ili waweze kuyafanyia kazi.

Alisema tangu kuanzishwa kwa umoja huo, wamekwenda zaidi ya mikoa 17 na majimbo yake ili kusikiliza maoni ya wananchi ambayo wameyachukua na kuyafanyia kazi, hivyo basi hawana muda wa kukaa na kujadili kauli za watu zinazotolewa barabarani za kujadili masuala yasiyowahusu.

“Sisi tunafanya kazi na Watanzania, hatufanyi kazi na mtu mmoja mmoja, ndiyo maana tulikwenda mikoa 17 na majimbo yake kwa ajili ya kuwaelezea umoja wetu na mikakati tuliyopanga ndani ya umoja huu, hivyo basi hatuna nafasi ya kujadili kauli ya mmoja mmoja,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wa umoja huo hawawezi kuishi kwa imani, bali wanafanya kazi kwa vitendo ili wananchi waweze kuwahukumu katika uchaguzi ujao.

Alisema Ukawa haupo kwa ajili ya Katiba peke yake, bali ni kuangalia maslahi ya wananchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha wanaondokana na hali ngumu ya maisha na kupata mafanikio.

Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa vitendo ili wananchi wenyewe waweze kuwanyooshea vidole kwenye chaguzi zijazo.

Naye Katibu wa Ukawa ndani ya Bunge, Julius Mtatiro, alisema mawazo ya mtu yanapaswa kuheshimiwa, lakini umoja huo hauwezi kufanya kazi ya utabiri kama utaendelea au kuvunjika.

“Ukawa hauwezi kufanya kazi ya utabiri, kwa sababu tulipoungana tulikuwa na malengo ya dhati, ikiwa ni pamoja na kuondoa tofauti zetu na kuangalia maslahi ya wananchi na si kauli ya mmoja mmoja, japo naheshimu mawazo yake,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alitolea mfano kwa kusema kauli ya Zitto ni sawa na falsafa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo wamekuwa wakitangaza kila kona kuwa upinzani Tanzania unaelekea kufa wakati si kweli.

WAJUMBE

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuwasili Dodoma Agosti kwa ajili ya kuanza mkutano huo kama ulivyopangwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam na ofisi hiyo, ilisema Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuanza vikao vyake Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.

Taarifa hiyo ilisema Agosti 4 itakuwa siku maalumu kwa ajili ya mambo ya kiutawala, hivyo wajumbe wote wanapaswa kufika Ofisi za Bunge Dodoma kuanzia saa 4:00 asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles