31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali yaua 19

Ajali ya basi la Morobest iliyotokea mkoani Dodoma
Ajali ya basi la Morobest iliyotokea mkoani Dodoma

Debora Sanja, Dodoma na Fadhili Athumani, Mwanga

WATU 19 wamepoteza maisha na wengine 64 wamejeruhiwa katika ajali mbili zilizotokea katika mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro.

Habari kutoka mkoani Dodoma zinasema watu 17 wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 2 asubuhi, katika eneo la Pandambili, lililoko Barabara ya Dodoma-Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Moro Best lenye namba za usajili T 258 AHV, ambalo lilikuwa likitokea Mpwapwa kwenda Dar es Salaam.

“Basi hili lilikuwa likiendeshwa na Said Lusogo, liligongana na lori lenye namba za usajili T 820 CKU lilokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma likiendeshwa na Gilbert Nemanya, ambaye alifariki katika ajali hiyo.

“Katika ajali hii watu 17 wamepoteza maisha, kati yao wanaume ni 12 na wanawake watano,” alisema.

Alisema watu 56 waliojeruhiwa walipata majeraha mbalimbali na wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Wilaya ya Kongwa.

“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kutokuwa na tahadhari kwa magari yaliyokuwa yanakuja mbele yake, wakati analipita gari lingine na kwenda kugongana na basi hilo,” alisema.

Alisema dereva wa lori ndiye aliyeonekana alikuwa na makosa kwa sababu alishindwa kuchukua tahadhari.

Alisema hadi jana mchana marehemu 11 walikuwa wametambuliwa na ndugu zao.

Alitaja majina ya waliotambuliwa kuwa ni Melina Maliseli, mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Christina, Wilson Suda, Mark Massawe, Gabriel Mejachiwipe na Justine Makasi, ambao wote ni wakazi wa Mpwapwa.

Wengine ni Nassib, aliyetambulika pia kwa jina moja, mkazi wa Kongwa, dereva wa lori Lemanya, dereva wa basi, Lusogo, kondakta wa wa basi hilo, Omar Mkubwa na utingo wa lori, Mikidadi Zubeir.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya, alisema hadi jana mchana hospitali hiyo ilikuwa imepokea majeruhi 21 na kwamba kati yao, wawili walifariki.

“Hadi sasa majeruhi waliobaki ni 19, lakini wawili hali zao si nzuri,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa abiria aliyenusurika katika ajali hiyo, Bahati Mwagoha, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa lori.

“Dereva wa lori alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi, hali iliyosababisha ashindwe kukata kona kulifuata basi na kuligonga,” alisema.

Kwa mujibu wa shuhuda mwingine aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed, alilalamikia mwendo kasi wa dereva wa basi.

Alisema kumekuwepo na tabia ya basi la Moro Best na Al-Saedy ambayo yamekuwa yakifukazana kila siku na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.

“Kwa leo (jana) Alsaedy liliondoka saa 12 alfajiri na hili la kwetu (Moro Best) liliondoka saa 12.10, wakati ajali inatokea mimi sikusikia kitu, badala yake nimejikuta nipo hospitali,” alisema.

KILIMANJARO

Huko mkoani Kilimanjaro, watu wawili wamefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa katika ajali mbaya ya gari iliyotokea juzi katika eneo la Kisekibaha, wilayani Mwanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba lilitokea juzi saa 4:30 asubuhi.

Alisema gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, mali ya Shule ya Sekondari Kandoto, ikiendeshwa na Sekunde Philbert (39), likitokea Kilomeni kuelekea Kisangara Juu, liliacha njia na kupinduka.

“Gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop, mali ya Shule ya Sekondari Kandoto, Jimbo la Same, liliacha njia na kupinduka ambapo watu wawili walipoteza maisha na wengine nane wakajeruhiwa,” alisema Kamanda Boaz.

Aliwataja marehemu kuwa ni kikongwe mwenye umri wa miaka 80, William Mlacha na Mary Zablon (40), ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kilomeni, wote ni wakazi wa kijiji cha Sofe-Kilomeni.

“Watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni William Mlacha, ambaye ana umri wa miaka 80, huyu ni babu, mwingine ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kilomeni, Mary Zablon ana umri wa miaka 40,” alisema.

Alisema majeruhi wote nane, akiwemo Muuguzi wa Zahanati ya Kilomeni, Serafia Msophe, wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same ambapo hali zao zinaendelea vizuri.

“Majeruhi wengine nane wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same, taarifa tulizonazo ni kwamba majeruhi hawa wanaendelea vizuri,” alisema Kamanda Boaz.

Wakati huo huo, taarifa kutoka katika eneo la tukio ambazo MTANZANIA ilifanikiwa kuzipata kutoka kwa Diwani wa Kata ya Kilomeni, Mohammedi Mgala (CCM), watu hao walikuwa wanakwenda Kisangara Juu kwa ajili ya mazishi ya shangazi yake Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Same, Jacob Koda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles