31 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wanunua ugomvi wa CUF

Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)Dar es Salaam jana la kutomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF.Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)Dar es Salaam jana la kutomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF.Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro.

* Wajiandaa kumshtaki Prof. Lipumba, wampachika jina la bwana yule

NA EVANS MAGEGE,

VIONGOZI wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana walitangaza maazimio nane ambayo watayatekeleza kukabiliana na ugomvi wa madaraka unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Maazimio hayo yaliafikiwa na kutangazwa jana katika kikao cha dharura cha viongozi wa Ukawa kilichofanyika Hoteli ya Protea Courtyard iliyopo See View, Upanga jijini Dar es Salaam. Vyama vinavyounda Ukawa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) NCCR-Mageuzi, Chama cha National League for Democracy (NLD) na CUF.

Akitangaza maazimio hayo kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alikuwa ameambatana na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi wa CUF, Julius Mtatiro na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamadi, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi.

Akisoma maazimio hayo, Mbowe alisema Ukawa wameazimia kutomtambua Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kama mwanachama, Mwenyekiti wa CUF na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa.

Alisema anapata shida kutambua kiwango cha elimu ya Prof. Lipumba katika muktadha wa kisiasa kwa kushindwa kutumia jina Profesa na badala yake akamuita bwana yule.

Mbowe alisema azimio hilo limetokana na kutambua kuwa Prof. Lipumba ni msaliti na amelenga kurudi CUF na Ukawa ili kuvisambaratisha.

“Hatushiriki kwa namna yoyote iwe katika shughuli ya kisiasa au kijamii itakayomhusisha ‘bwana yule’ katika kofia yoyote ya uongozi wa CUF,” alisema Mbowe.

Alilitaja azimio la pili kuwa ni kumtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro kama kiongozi halali na Katibu Mkuu wa chama hicho ni Maalim Seif Sharif Hamad.

“Kama viongozi halali wa CUF ni Mwenyekiti wa kamati ya muda, Julius Mtatiro na Katibu Mkuu ni Maalim Seif. Kwa maana hiyo tutawaelekeza viongozi wa vyama vyetu wa ngazi zote, wanachama, wafuasi na wapenzi wa vyama washirika wa Ukawa kuwapa viongozi hawa kila aina ya ushirikiano wanapotekeleza majukumu yao,” alisema Mbowe.

Azimio la tatu alilolitaja ni Ukawa kuwaelekeza viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa vyama washirika mahali popote walipo kuhakikisha hawatoi ushirikiano wa aina yoyote kwa Mwenyekiti Prof. Lipumba pamoja na kile alichokiita kikundi chake cha wasaliti.

Kwamba wanachama na mashabiki wa Ukawa washiriki kwa namna moja au nyingine shughuli yoyote ya kisiasa au kijamii itakayomhusu Prof. Lipumba au wafuasi wake.

Azimio la nne alilolitaja ni viongozi wa kuchaguliwa wa vyama washirika wa Ukawa kuanzia ngazi ya wenyeviti wa mitaa, vijiji, madiwani na wabunge kuendelea kushirikiana.

“Hapa tunamaanisha kwamba, wafanye hivyo katika maeneo yao na kwa vyovyote vile wasitoe ushirikiano wala kupokea maagizo au maelekezo ya aina yoyote kutoka kwa ‘bwana yule’ au wafuasi wake kuhusu shughuli zozote za kisiasa au kiserikali zinazohusu Ukawa,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema azimio la tano linatoa maelekezo kwa uongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, kuhakikisha wafuasi wa Prof. Lipumba ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanatengwa katika mambo yote yanayohusu Ukawa ndani ya kambi hiyo.

“Kambi rasmi ya upinzani bungeni ihakikishe kwamba wafuasi wa ‘ bwana yule’ ambao ni wabunge na ni viongozi ndani ya kambi rasmi, wanaondolewa katika nafasi zozote za uongozi walizonazo na kwa vyovyote wasishirikishwe katika shughuli yoyote ile inayohusu Ukawa au kambi rasmi ya upinzani bungeni ndani na nje ya Bunge,” alisema.

Azimio la sita alilolitaja ni masuala yote yanayohusu hali ya kisiasa kwa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushughulikiwa chini ya utaratibu wa Ukawa.

“Jitihada za kidiplomasia zinazoendelea za kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro wa kisiasa uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu halali Zanzibar na zinazohusu kupinga utawala wa kidikteta wa Rais John Magufuli, zitafanyika kwa ushirikiano na uratibu wa Ukawa.

“Azimio la saba ni mawakili wa vyama washirika wa Ukawa kuanzisha taratibu za kisheria za kufungua mashtaka dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa matumizi mabaya ya madaraka au ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kitendo chake cha kuingilia masuala ya ndani ya CUF na kujifanya mwamuzi wa masuala ya uongozi wa vyama vya siasa,” alisema Mbowe.

Azimio la mwisho alilolitaja ni mawakili wa vyama washirika wa Ukawa kuanzisha taratibu za kisheria za kufungua mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba na kundi lake kwa kitendo cha kuingia kwa nguvu na kijinai katika Ofisi Kuu za CUF Buguruni, kuharibu mali na kuendelea kuzikalia ofisi hizo kinyume cha sheria.

Aidha, Mbowe alisema mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni wa kisaliti na umetengenezwa na Serikali kwa lengo la kuchochea mvutano miongoni mwa wana-Ukawa pamoja na kuvuruga msimamo wa wana-CUF Zanzibar kupigania matokeo ya uchaguzi mkuu.

“Bwana yule katumwa kuja kuondoa hali ya utulivu na juhudi mbalimbali za kidiplomasia katika nyanja za kimataifa na kitaifa zinazofanywa na CUF pamoja na Ukawa kwa ujumla kuimarisha nguvu ya pamoja kupinga utawala ambao tunauona ni wa kidikteta wa Rais Pombe Magufuli.

“Na kibaya zaidi wanauona umoja huu unaimarika kwenda kwenye malengo mapana zaidi ya kusonga mbele katika kuikosoa Serikali kwa mwenendo wake wa sasa, pia wameona umoja huu ni tishio kwa Serikali ya Rais Magufuli kwenda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kwa sababu bado kuna sintofahamu katika siasa za Zanzibar,  bwana yule ametumwa katika mkakati mwingine kwamba hakumaliza kazi yake ya awali.

“Wamemwagiza kuwa aliyejaribu kumnyonga hakufa, rejea tena kama ilivyokuwa mwanzoni. Na kwa sababu bwana yule amekula vya mtu hawezi kukataa kwa sababu ni kweli ameendelea kuwa wakala wa CCM,” alisema Mbowe.

Awali, Maalim Seif aliulizwa jinsi Kamati ya Muda ya Uongozi ya CUF inavyofanya kazi wakati Ofisi Kuu ya Buguruni iko chini ya Prof. Lipumba na kujibu kuwa jambo hilo litatolewa ufafanuzi na wenyeviti wa Ukawa.

Akijibu swali hilo, Mbowe alisema CUF inaendelea na shughuli zake za kiutendaji kama kawaida kupitia kwa Kamati ya Muda ya Uongozi inayoongozwa na Mtatiro.

“Chama si jengo, unaweza kuendesha chama popote pale hata kama ni barabarani, kwa hiyo ndugu wanahabari CUF kinaendelea na utendaji wake kama kawaida na hakijakwama popote,” alisema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles