24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aishtukia ripoti ya Uchumi BoT

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe

Na TOBIAS NSUNGWE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amehoji taarifa ya Benki Kuu (BoT) kuhusu kile ilichodai kuongezeka kwa kasi ya ulipaji wa deni la taifa pasipo kueleza kasi ya ukopaji wake.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana Zitto ambaye ni mchumi kitaaluma na Mbunge wa Kigoma Mjini alidai hakuna haja ya kushangilia kuhusu kasi ya ulipaji wa deni hilo kwani taarifa zinaonesha hadi Juni mwaka huu deni la ndani lilikuwa limeongezeka kwa asilimia 35 ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia Sh. trilioni 10.7.

Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, juzi alitoa Ripoti juu ya hali ya uchumi katika kipindi cha nusu mwaka  ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kuongezeka kwa kasi ya ulipaji wa deni la taifa lakini hakueleza kiasi ambacho serikali imekopa kwa kipindi hicho.

Kwa mujibu wa Zitto inawezekana Gavana alikua akificha kitu.

“Taarifa ya BoT (Monthly Economic Review) ya mwezi Julai ndiyo iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu hadi sasa inaonyesha kuwa deni la taifa linaongezeka hadi kufikia USD 16 bilioni mwezi Juni, (mwisho wa ripoti ya pili ya mwaka 2016)  kati ya mwezi Mei na Juni  deni liliongezeka kwa USD 74 milioni, Nyongeza ya mwaka mzima ya 2015 hadi Juni mwaka huu ni USD 890 (2 trilioni ) sasa Gavana anaposema kuwa serikali imelipa halafu hasemi deni lililoongezeka ndani ya mwaka mmoja ana maana gani?” alihoji Zitto

Zitto anasema kulipa zaidi kwa kukopa zaidi sio jambo la kujivunia.

“Deni la ndani liliongezeka kwa asilimia 35 ndani ya mwaka mmoja  hadi 10.7 trilioni mwisho wa Juni mwaka huu sasa hii ya kulipa madeni  kwa kukopa zaidi ndio jambo  la kusheherekea? Kwanini madeni yaongezeke wakati mapato ya TRA  yameongezeka? Huoni changa la  macho hapo?” alihoji.

Katika ripoti iliyotolewa juzi na Ndulu, imeeleza kuwa Rais John Magufuli amelipa Sh. bilioni 99 za deni la ndani na pia amelipa dola za Marekani milioni 90 za deni la nje katika muda wa siku 90.

Rekodi hiyo mpya ya ulipaji madeni inadaiwa haijawahi kufikiwa na Serikali ya awamu ya nne katika kipindi chote cha miaka 10.

Msomi na mtaalamu wa mambo ya kodi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Hadley Mafwenga, alisema nidhamu katika ulipaji wa deni ni muhimu ili kuipa thamani miradi inayoendeshwa na fedha za mikopo ambayo Serikali ilichukua huko nyuma.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Profesa Mafwenga alisema ulipaji wa deni la taifa ni muhimu kama nchi inataka kuweka mazingira ya kuweza kukopesheka siku zijazo na kupunguza athari (risk) zinazotokana na kuchelewa kulipa madeni hayo.

Kwa mujibu wa Profesa huyo kadiri nchi inavyochelewesha deni, riba inaongezeka hivyo ni busara kulilipa mapema.

Kwa mujibu wa BoT hadi sasa deni la taifa linafikia Sh trilioni 51.

Pamoja na hayo, Profesa Mafwega alisema wale wanaofananisha ulipaji wa deni la taifa kati ya Magufuli na Serikali ya Kikwete wana mtazamo wa kisiasa zaidi kwani deni liko ‘linked’ na nchi si rais aliyeko madarakani.

Profesa Mafwenga katika maelezo yake alisisitiza kwamba hakuwa ameisoma kwa kina ripoti ya profesa Ndulu na kuahidi kuchambua zaidi pindi atakapoisoma.

Profesa huyo alizungungumzia pia hali ya kukua kwa uchumi nchini akisema inatokana na kukua kwa wigo wa uzalishaji.

Alieleza kwamba, pia hali ya mfumuko wa bei inaendelea kushuka na kuzidi kuifanya shilingi yetu kuimarika.

Gavana Ndulu alisema mwenendo wa ukuaji uchumi kwa nusu mwaka kuanzia Januari hadi Juni 2016, umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 5.7 katika kipindi hicho hicho mwaka 2015.

Profesa Ndulu alizitaja sekta zinazochangia ukuaji wa uchumi kuwa ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo, uchimbaji madini na gesi, mawasiliano na sekta ya fedha.

Wachumi wengi wamekuwa wakiitaka Serikali iongeze kasi ya ulipaji wa deni la taifa ili kuwapunguzia wananchi mzigo na kuiwezesha nchi kukopesheka tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles