23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa kumfikisha Magufuli The Hague

James Mbatia
James Mbatia

Na Kulwa Mzee, Dodoma

MWENYEKITI Mwenza wa wabunge wanaounda Umoja wa Katiba (UKAWA), James Mbatia amesema wanaendelea kukusanya ushahidi vitendo vya ubakaji demokrasia na haki za binadamu   kumfikisha Rais Dk. John Magufuli katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (The Hague).

Mbatia alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na wabunge wengine wa Ukawa kuhusu vitendo vinavyoendelea   Unguja na Pemba.

“Tunamfikisha Rais Magufuli katika Mahakama ya Kimataifa  kujibu makosa hayo maana tunaamini matendo hayo ya huko Zanzibar na yale yanayotokea Tanzania Bara yana baraka zake kamili.

“Tunatoa wito kwa Rais Magufuli kutimiza wajibu wake mkuu wa kwanza wa katiba nao ni kuhakikisha usalama wa raia wa Jamhuri ya Muungano. Pia kuhakikisha   vikosi vya usalama vinatimiza kazi yao kuu ya kuwalinda na siyo kuwaonea raia,”alisema.

Alisema Ukawa wanapenda kusikia kauli ya wazi ya Rais Magufuli juu ya uonevu unaodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari na kuheshimiwa haki zao za binadamu ikiwa ni pamoja na zile za kujikusanya, kujiunga na maoni.

“Tunaendelea kukusanya taarifa hizi za vitendo vya ubakaji demokrasia na haki za binaadamu  kupata ushahidi wa kutosha wa kumfikisha Dk. Magufuli katika Mahakama ya Kimataifa akajibu makosa hayo maana tunaamini matendo hayo ya huko Zanzibar na yale yanayotokea Tanzania Bara yana baraka zake kamili.

“Ukawa inamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba afanye ziara ya haraka Pemba na kisha Unguja na apate taarifa juu ya matendo hayo ya polisi kwa kukutana na wananchi walioathirika katika matukio tuliyoyataja na Ukawa iko tayari kumsaidia kuwapata watu hao,”alisema Mbatia.

Ukawa pia inamtaka IGP, Ernest Mangu kwanza atoe amri ya kuachwa matendo hayo, lakini pili achukue hatua dhidi ya polisi ambao wamekuwa wakionea na kutesa raia ili kurudisha imani ya jeshi hilo kwa wananchi hasa wa Pemba.

Mwingine ambaye Ukawa inambebesha mzigo wa lawama ni Kamishna Hamdan Omar wa Zanzibar kwa kunyamazia matendo hayo na kumtuma Kamishna wa Upelelezi (DCI), Salum Msangi kwenda Pemba kusimamia vitendo hivyo huku askari kadhaa kutoka Tanzania Bara wakipelekwa Pemba kipindi hiki   kuzidisha vitendo hivyo haramu.

“Ukawa inawataka wananchi wa Unguja na Pemba kuikataa Serikali haramu iliyopo madarakani huko Zanzibar kwa njia za amani  na pia wadumishe utaratibu walionao hivi sasa wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya kukinzana na sheria.

“Ukawa inaamini usiku hauwezi kuwa mrefu wa kuzuia alfajiri na asubuhi isifike,” alisema na kuongeza kwamba tamko hilo limepata baraka na wabunge wote wa Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles