25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ukawa: Hatutaruhusu mamluki uchaguzi wa meya K’ndoni, Ilala

MWITAVeronica Romwald na Koku David, Dar es Salaam

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimesema vipo tayari kushiriki uchaguzi wa mameya kwa Manispaa ya Ilala na Kinondoni, lakini havitakubali kuruhusu wasiohusika (mamluki) kushiriki uchaguzi huo.

Awali uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na mgogoro ulioibuka baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutuhumiwa kuingiza wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar pamoja na mawaziri walioteuliwa na Rais Dk. John Magufuli na kusababisha uchaguzi uliopangwa kufanyika awali kuvunjika.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, alisema Ukawa wamejiandaa kushinda katika uchaguzi huo, lakini pia wamejiandaa kuwazuia mamluki wa CCM iwapo watajaribu kuingia tena.

“Ukawa tumejiandaa vilivyo kushinda uchaguzi wa umeya wa Ilala na tumejiandaa vile vile kuwakabili mamluki wa CCM kama watawaleta tena kuja kushiriki, tunawafahamu wale wote wenye vigezo vya kushiriki walioko ndani ya CCM, lakini wakiwaleta wasio na vigezo hiyo kesho tutawadhibiti,” alisema.

Naye Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alisema uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa kesho saa nne katika ukumbi wa Karimjee na kuongeza kuwa uchaguzi huo ni mwendelezo wa ule uliositishwa.

“Vyama vyote vimepelekewa ujumbe juu ya uchaguzi huo, vinatakiwa kuhakikisha kwamba wale wenye vigezo ndio wanaoshiriki uchaguzi huo na si vinginevyo,” alisema Tabu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, alionya kwamba iwapo Mkurugenzi wa Kinondoni atashindwa kusimamia ipasavyo uchaguzi huo kwa kutimiza agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene atapaswa kujiuzulu.

Alisema katika agizo hilo Simbachawene alisema uchaguzi huo uwe umekamilika hadi kufikia Januari 16.

“Uchaguzi wa meya umekuwa ukikwama kutokana na wenzetu wa CCM kuwaleta mamluki wao kutoka maeneo mengine ili waje kupiga kura, sisi hatukubali jambo hili na watasababisha mgogoro kuendelea na kama uchaguzi hautafanyika mkurugenzi atakuwa ameshindwa kutimiza agizo la Waziri Simbachawene, hivyo atapaswa kuwajibika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles