26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

UKATA WATOA ASILIMIA 30 YA MABASI BARABARANI

*Mengine yadaiwa kusajiliwa nje ya nchi kufanya biashara


Na EVANS MAGEGE

WAKATI ikiwa imebaki miezi mitatu mwaka wa fedha 2016/17 ufike ukingoni, biashara ya usafiri wa mabasi ya abiria yanayoenda katika mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi, imeelezwa kuwa mbaya.

Kutokana na kuyumba huko kwa biashara, takribani asilimi 50 ya wamiliki wa mabasi, wameelezwa kutoa magari yao barabarani, kuyahamishia nchi jirani na wengine kupunguza safari.

Yote hayo, chanzo chake kinaelezwa ni kupungua kwa abiria kwa kiasi kikubwa.

Matokeo ya hali hiyo, wafanyabiashara wa mabasi ambao wengi huendesha shughuli zao kwa mikopo ya benki, wanadaiwa kuwa katika wakati mgumu kwa kushindwa kurejesha mikopo yao.

Pia inaelezwa kwamba mabasi mengi huendeshwa kwa wamiliki kukopa mafuta, vipuri na vitu vingine ambavyo hulipwa kwa makubaliano maalumu.

 

HALI HALISI

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA, umebaini baadhi ya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani, baadhi yanatoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, Dar es Salaam yakiwa na abiria 20 ama 30 badala ya 50 ama 60.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Enea Mrutu, anasema asilimia 30 ya kampuni za mabasi, zimesitisha huduma kwa sababu ya hasara inayotokana na uendeshaji.

Mrutu anasema hali ya biashara imeporomoka kwa kasi kuanzia katikati ya mwaka jana na imeendelea kudhoofika hadi sasa.

“Ndugu yangu usafirishaji kwa njia ya mabasi umefika katika hatua ambayo haijawahi kutokea ndani ya nchi hii, idadi ya abiria imeshuka kwa kasi, fedha hakuna,” anasema Mrutu.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara, wameamua kupeleka mabasi yao nchi jirani.

Nchi ambazo mabasi hayo yamepelekwa ni pamoja na Kenya, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Msumbiji, Malawi na Zambia.

Mrutu anataja baadhi ya kampuni zilizohamishia magari yake nchi jirani kwamba ni pamoja na ile ya RATCO.

 “Wapo waliopeleka mabasi yao nje ya nchi, kuna kampuni kama RATCO wamepeleka gari Kongo, Taqwa nao wako Kongo na Kenya, yaani kwa kweli hali imekuwa ya ovyo sana kibiashara,” anasema.

Anasema taratibu za kuhamisia huduma ya usafirishaji nje ya nchi zinawahusu wamiliki wenyewe ambao hujisajili katika nchi husika.

 “Ukifika huko lazima wakusajili ili kukuruhusu kuendesha biashara hiyo,” anasema.

Wakati kupungua kwa abiria kukitajwa kuwa ni moja ya sababu ya biashara hiyo kuyumba, utitiri wa faini zinazotozwa na polisi wa barabarani – trafiki, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na mizani za barabarani, vinatajwa kuwa ni vitu vinavyoongeza mzigo katika biashara hiyo.

“Kuna mambo mengi yanayotukwaza katika biashara hii, gari unanunua kwa bei juu na unapolifikisha hapa nchini unatozwa ushuru ambao ni nusu ya bei uliyonunulia, na ukianza kuendesha biashara yenyewe unakukutana na vikwazo vingi sana.

“Kwa mazingira ya ugumu huu wa biashara hapa nyumbani, lazima utafute sehemu nyingine ambayo unaona itakunufaisha,” anasema mmiliki mmoja wa mabasi ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.

 

KUPAKI MABASI

Mrutu anasema wapo pia wamiliki ambao wameamua kupaki magari yao kutokana na kupata hasara.

Kwamba wafanyabiashara hao, wako katika wakati mgumu kutokana na kushindwa kurejesha madeni ya benki walikokopa ili waweze kuendesha biashara.

Anasema pia kwa asili ya biashara hiyo, wamiliki wa mabasi hukopa mafuta katika vituo vya mafuta na kulipa kwa wiki ama mwezi kutokana na makubaliano watakayoingia.

Kutokana na kuzorota huko kwa biashara, Mrutu anasema sasa wamiliki wengi wanashindwa kulipa madeni hayo.

Anasema pia hata vipuri vya magari na matairi, wengine huchukua kwa mkopo, lakini kwa sasa wamejikuta na mzigo mzito wa madeni ambayo kwa hali ya biashara sasa hayalipiki.

“Wapo wengi tu nimeambiwa wamepunguza magari yanayoingia barabarani, wengine wameamua kupaki kabisa ili kuangalia biashara nyingine.

“Si unajua mazingira ya kibiashara baba, unakuta mtu amechukua mkopo benki akanunua mabasi 100, halafu katika operesheni yake ya kila siku anajikuta basi linaambulia kubeba abiria 20 hadi 30 badala ya 60, unadhani hapo mkopo ataweza kuurejesha?

 Kwa kweli biashara hii kwa sasa inaumiza kichwa,” anasema Mrutu.

Kwa upande wake, Njoka Elimboto, ambaye pia ni mtumishi wa Taboa, anasema umoja huo una wanachama 900 ambao wanamiliki takribani mabasi 8,000.

Elimboto anasema kupungua kwa abiria kunatokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutosafiri sana kwa watumishi wa umma kwa sababu ya kupunguzwa semina.

Anasema pia kupigwa marufuku kwa biashara ya mitumba kumewaathiri hadi wao kwani kulikuwa na watu kutoka mikoa mbalimbali waliokuwa wakisafiri kila siku kwenda Dar es Salaam kununua nguo hizo.

 “Ingawa bado tunaendelea kutathmini mwenendo wa biashara inavyokwenda, lakini kuzuiwa kwa biashara ya mitumba kumetupotezea wateja wetu wengi. Huwezi amini basi linaweza kusafiri kutoka Dar hadi Mwanza likiwa limebeba abiria 30 tu kwa sasa, sasa hapo ndiyo machungu ya biashara hii unaanza kuyasikia.

“Kutokana na kushuka kwa idadi ya abiria wanaosafiri kila siku, tumeamua kuweka utaratibu wa kusafiri kwa zamu, kwa mfano kama safari ya Mwanza yalikuwa yanakwenda mabasi 40 kwa siku, inabidi yaende 20 na lengo kuu ni kutoa unafuu kwa kila basi walau lipate abiria wa kutosha,” anasema Elimboto.

Mbali na hatua hiyo, baadhi ya kampuni zilizokuwa zikisafiri sana kwenye njia za Dar es Salaam – Morogoro na Dar es Salaam – Dodoma, zimepunguza mabasi kwa takribani asilimia 50.

Bila kuzitaja kwa majina kampuni hizo, mtoa taarifa mmoja kutoka Taboa anadokeza kwamba kwa sasa kampuni hizo zinatumia mabasi saba hadi manane kwa siku kusafirisha abiria tofauti na ilivyokuwa awali.

Anasema kampuni moja imelazimika kupunguza mabasi yake kutoka saba hadi matatu, huku kampuni nyingine imepunguza mabasi yake manane hadi kufikia mawili kwa siku.

“Kuna kampuni moja huwa ina mabasi mengi yanayosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, zamani kabla ya mwaka jana ilikuwa inatumia mabasi 30 kwenda na kurudi, lakini kutokana na kupungua kwa abiria, sasa kampuni hiyo imelazimika kutumia mabasi 20 hadi 15 kwa siku.

“Pia usisahau njia ya Dar es Salaam – Arusha, kuna kampuni moja nimepewa taarifa mwezi uliopita mmiliki wake ameamua kuyapaki mabasi yake yote na sasa anatafakari kufanya biashara nyingine.

“Vivyo hivyo hata njia ya Tanga na Mbeya nako baadhi ya wamiliki wamepunguza idadi kubwa ya mabasi yanayofanya huduma ya usafirishaji kila siku,” anadokeza mtoa taarifa huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles