NA, OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI
IKIWA Â ni wiki saba tangu kuuliwa Jamal Khashoggi, Mwandishi wa Habari wa Saudi Arabia aliyekuwa mpinzani wa serikali ya nchi yake, Ujerumani imeamua kuzuia kabisa kusafirisha silaha katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Pia imewapiga marufuku kuingia Ujerumani Wasaudi 18 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo. Kutokana na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Berlin na kwamba 15 kati ya watu hao ni wa kikundi kilichoendesha mauaji hayo na wengine watatu walishiriki kusaidia kuandaa mauaji yenyewe. Mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, hayumo katika orodha ya watu hao waliotajwa.
Kwa hivyo, ina maana Ujerumani sasa inazuia kabisa kusafirisha silaha Saudi Arabia. Hapo kabla Ujerumani ilisema itaacha kutoa vibali vipya vya kuiuzia silaha nchi hiyo ya jangwa. Lakini jana Wizara ya Uchumi huko Berlin iliweka wazi kwamba hata ruhusa zilizokwisha tolewa kwa ajili ya kuipelekea Saudi Arabia silaha zitafutwa. Msemaji wa wizara hiyo alisema kwamba kutoka sasa silaha hazitapelekwa Saudi Arabia. Haijatajwa wingi wa silaha ambazo zitakuwamo katika mkumbo huo wa vikwazo dhidi ya Riyadh.
Bila shaka kiwanda cha kutengeneza meli cha Wolgaster Lürssen hapa Ujerumani kitaathirika na ambacho bado kilitakiwa kiipatie Saudi Arabia boti za doria 20. Inasemakana mbili ya boti hizo zilikuwa tayari zimeshapatiwa ruhusa ya kusafirishwa. Pia kiwanda cha meli kilichopo Mecklenburg-Vorpommen kilishaanza kutengeneza boti nyingine nane.
Haijulikani hatua hiyo  ya Ujerumani kuelekea Saudi Arabia itadumu hadi lini, lakini nafasi za kazi 300 zilitegemea uhondo huo wa kandarasi ya Wasaudi.
Ujerumani imejaribu kuzishawishi baadhi ya nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zichukue hatua kama iliyochukua, lakini hadi sasa haijafanikiwa. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekataa kuipinga hatua hiyo ya Wajerumani. Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani, Haiko Maas, alitangaza jana pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba uamuzi wa nchi yake wa kutowaruhusu maafisa wa vyeo vya juu wa Saudi Arabia kuingia Ujerumani.
Alisema “Kama ilivyokuwa kabla, hivi sasa kuna maswali mengi zaidi kuliko majibu katika kuupata uwazi wa mkasa huu. Watu gani walikuwa nyuma ya mkasa huu? Alisema kwamba hata hivyo, Ujerumani kama ilivyokuwa Marekani, hivi sasa inachukua hatua kutokana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa hadi sasa.
Na uchunguzi huo unasema kwamba Jamal Khashoggi, aliyekuwa anaishi uhamishoni Marekani, aliuliwa Oktoba 2, mwaka huu ndani ya jengo la ubalozi wa nchi yake (Saudi Arabia) mjini Istanbul, Uturuki. Khashoggi alikwenda kwenye jengo hilo kuchukua hati ambazo zingemuwezesha amuowe mchumba wake wa Kituruki.
Baada ya kuwepo mbinyo wa kimataifa, watawala wa Riyadh baadaye kabisa walikiri kuuliwa kwa Khashoggi aliyekuwa mwandishi wa makala katika gazeti la Kimarekani la “Washington Post”
Mwendeshaji mashtaka wa Saudi Arabia amewatuhumu baadhi ya maafisa wa vyeo vya juu katika serikali ya nchi hiyo kwamba walitoa amri ya kutumwa kikundi cha watu 15 kwenda Istanbul kufanya mauaji hayo. Mwendeshaji mashtaka huyo ametaka watano kati ya watu walioshiriki katika mauaji hayo wapewa hukumu ya adhabu ya kifo. Watu walioshtakiwa walikuwa 11.
Haijulikani bado nchi ngapi za Mkataba wa Schengen  (ambazo zina mfumo wa pamoja wa uhamiaji na forodha) zitafuata mfano wa Ujerumani wa kuiwekea vikwazo Saudi Arabia.