30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Wasiwasi watawala uchaguzi ujao urais  nchini Kongo

UCHAGUZI wa urais Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo  Desemba 23, mwaka huu unaonesha huenda ukafanyika bila ya kuwapo msisimko mkubwa kwa vile kati ya wagombea katika kinyang’anyiro hicho hatakuwamo mwanasiasa yeyote aliye mashuhuri sana.

Vigogo wa upinzani walikutana wiki iliyopita huko Geneva, Uswisi na mwishowe walikubaliana kumchagua mbunge asiyejulikana sana, Martin Fayulu, aliye mkuu wa chama kidogo cha Ecide, kuwa mgombea wao wa pamoja.

Waliamua kwamba Fayulu ashindane na Emmanuel Ramazani Shadary, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na ambaye ni mgombea wa urais kwa tiketi ya kambi ya Serikali ya Rais Joseph Kabila. Kwa hivyo, ilidhihirika wazi kwamba vigogo wote wa siasa za Kongo hawatakuwamo katika mchuano huo.

Mwenyewe Rais Kabila hatowania tena. Hasimu wake aliyetazamiwa atachuana naye vikali, Gavana wa zamani wa Mkoa wa Katanga, Moise Katumbi, anaishi uhamishoni na hajaruhusiwa kuikanyaga ardhi ya Kongo. Mtu mwingine wa pili ambaye alitazamiwa angempa kibarua kigumu Kabila pindi angelazimisha kushiriki katika uchaguzi, mbabe wa zamani wa kivita, Jean-Pierre Bemba, hajaruhusiwa kushiriki kutokana na ile kesi aliyokabiliana nayo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai huko The Hague.

Mtu aliyebaki na aliyetazamiwa atashiriki tangu mwanzo katika mchuano wa Desemba 23 ni Felix Tshisekedi, Mkuu wa Chama  cha UDPS ( Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamiii) na ambaye baba  yake, Marehemu Etienne Tshisekedi, alimenyana na Kabila katika uchaguzi wa mwaka 2011 na akapata asilimia 32 ya kura.

Wiki iliyopita huko Geneva, Felix Tshisekedi, Katumbi, Bemba, Fayulu na mtu aliyeshikilia nambari ya tatu katika uchaguzi wa 2011, Vital Kamerhe, pamoja na viongozi wa vyama viwili vingine vya upinzani walikutana kujaribu kupata mwafaka wa kuwa na mgombea wa pamoja kwa niaba ya vyama vyao. Walitambua fika kwamba ni tu pale upinzani utakapoungana ndipo itawezekana kumshinda Emmanuel Shadary na kuyaondoa kabisa mabaki ya urithi wa Kabila.

Mkutano huo wa Geneva uligharimiwa na Wakfu wa Kofi Annan na kuongozwa na Mwanadiplomasia wa Kiingereza, Alan Doss, ambaye ni mkuu wa zamani wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Kongo. Habari kutoka mkutano huo zilisema kwamba wanasiasa hao saba walipata taabu kufikia makubaliano. Katumbi alimuunga mkono Tshisekedi, huku Bemba akiwa upande wa Kamerhe. Kila kambi kati ya hizo mbili ilihoji kwamba ina nafasi zaidi ya kushinda kuliko kambi nyingine, hali ambayo ilimsaidia mtetezi mdogo watatu na hivyo kumwezesha Martin Fayulu mwishoni ashinde, tena kwa mshangao wa watu wengi.

Punde baada ya Fayulu kutangazwa kwamba atapeperusha bendera ya upinzani, mpasuko ulionekana. Si kwamba Fayulu hajulikani kabisa na Wakongomani. Yeye anakiongoza chama kilichompigia debe Tshisekedi katika Uchaguzi wa 2011 na baada ya hapo kikawa kinafanya maandamano mjini Kinshasa dhidi ya Serikali ya Kabila.

Umaarufu wa Fayulu haujasambaa nje ya Kinshasa na mkoa wa huko kwao wa Bandundu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 61 na ambaye katika mtandao wake anajitaja kama mwanajeshi wa umma, ameshawahi kuwekwa ndani kutokana na siasa zake kali. Lakini historia ya maisha yake ni yenye kung’ara. Mwaka 1984/2003 alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya mafuta ya Kimarekani, Mobil, huko Ethiopia.

Kuna tetesi kwamba Fayulu anajigamba tu kuwa ni mwanasiasa mwenye siasa kali ilhali ana maingiliano ya kutia mashaka na baadhi ya watu, jambo linaloweza kuichafua tamaa yake ya siku moja kuwa Rais wa Congo. Wanachama wa (UDPS) wanaoongozwa na Felix Tshisekedi waliposikia kwamba kiongozi wao alitia saini huko Geneva kukubali Fayulu awe mgombea wa pamoja wa urais walikuja juu na kuubisha uamuzi huo. Baadaye Felix Tshisekedi alikuwa hana njia isipokuwa kutangaza kwamba anaiondosha hiyo saini yake aliyoiweka Geneva na sasa yeye mwenyewe ataipeperusha bendera ya chama chake kuwania urais.

Sasa kambi ya upinzani imegawika tena kama ilivyokuwa hapo kabla. Nayo kambi ya Serikali ya Kabila inapiga vigelegele na kushangilia. Katibu Mkuu wa chama tawala cha PPRD (Chama cha Umma cha Ujenzi Mpya na Maendeleo), Tunda ya Kasende, alisema Fayulu ni tu mgombea wa kipande cha Upinzani. Timu ya uchaguzi ya Shadary sasa inasema kwamba Fayulu ni mtetezi wa mataifa ya kigeni na pia anabishwa na wapinzani wenyewe.

Jamii ya kimataifa inazidi kuwa na shaka juu ya vipi mambo yatakavyokuwa katika uchaguzi huo wa urais na Bunge hapo Desemba 23. Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki la nchi hiyo, Cenco, lenye ushawishi mkubwa, limeitaka Serikali ya Kinshasa ihakikishe mambo yanakwenda vizuri na kwamba kutakuwapo usalama wakati wa uchaguzi. Rais wa Cenco, Marcel Utemi, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kisangani, alisema kwamba kuna hatari uchaguzi huo usifanyike katika hali ya usalama, akionya kwamba pindi hali hiyo itatokea au uchaguzi utaahirishwa, basi mambo yatasababisha yasiweze kudhibitiwa na mtu yeyote.

Ni miaka miwili sasa tangu kipindi cha urais wa Kabila kimalizike rasmi Desemba 2016. Uchaguzi mpya haujaweza kufanywa tangu wakati huo kutokana na kutokuwapo matayarisho ya kutosha. Cenco ilijaribu kuituliza hali ya mambo, huku Kabila akiendelea kutawala. Desemba 2016 mwafaka ulitiwa saini baina ya Serikali na upinzani ukitaka uitishwe uchaguzi huru ifikapo mwisho wa 2017. Mapatano hayo yaliahirishwa tena na ikatajwa kwamba uchaguzi utafanyika mwisho wa 2018.

Katibu Mkuu wa Cenco, Abe Donatien Nshole, alisema kwamba Wakongomani hawatalikubali jaribio lolote la kuuahirisha tena uchaguzi. Pia alisema Wakongomani hawataki uchaguzi wa hovyo, utakaokuwa na matokeo si sawa, si ya haki na ambayo baadaye hayatatambuliwa, kwani baadaye kuna hatari ya kutokea machafuko.

Kwamba uchaguzi huu utafanyika kwa njia huru na matokeo yake kutambuliwa na Wakongomani wengi pamoja na jamii ya kimataifa si hakika. Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba kati ya majina ya watu milioni 40 yaliokuwamo ndani ya Daftari la Wapiga Kura, milioni sita kati yao ni wapiga kura wapya na alama za vidole vyao haziko ndani ya vitambulisho vyao. Upinzani unadai kwamba kuna wapiga kura feki au hewa ambao wanakusudiwa kuuhakikisha ushindi upande wa serikali. Cento inataka majina hayo milioni sita yawekwe hadharani na pia Daftari la Wapiga Kura lichunguzwe na watu wasiopendelea upande wowote.

Tume ya Uchaguzi ya Kongo haitaki upigaji kura ufanywe kwa karatasi, lakini kwa mashine za elektroniki, kwa vile kwa nchi kubwa kama Kongo isiyokuwa na miundombinu, kutumia karatsi katika upigaji kura ni kazi ngumu sana. Hata hivyo, upinzani na Cenco wanasema kwamba kwa vile alama za vidole zinahitajika pale unapotumiwa mtindo wa mashine za elektroniki na sasa hakuna wakati wa kutosha kupata alama hizo, basi inafaa mtindo wa kutumia karatasi usonge mbele.

Hadi sasa kanisa ndio taasisi pekee katika nchi hiyo iliyo huru na iliyo na mtandao mpana wa nchi nzima kuweza kuhakiki vipi uchaguzi utakavyofanyika. Wachunguzi wa uchaguzi 40,000 wa kutoka makanisa hadi sasa bado hawajapewa vitambulisho. Kuna mbinyo wa kimataifa unaozidi na pia kutoka Cenco kwamba Serikali ya Kabila iruhusu kuwapo uhuru wa vyombo vya habari na uheshimu haki za binadamu wakati wa uchaguzi na pale matokeo yatakapokuwa yanatangazwa.

Hali ya mvutano baina ya Dola na Kanisa Katoliki la Kongo imekuwapo kwa muda mrefu, lakini  alipoihutubia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni, Rais Kabila alisisitiza kwamba zoezi la uchaguzi litasonga mbele kwa vyovyote hapo Desemba 23, mwaka huu tena uchaguzi huo utaendeshwa kwa usalama  na matokeo yake yataaminika.

Aliwalaani watu wa nje wanaoingilia  mambo ya ndani ya Kongo kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu. Pia alitaka Majeshi ya Usalama ya Umoja wa Mataifa yaondoke Kongo.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba kivuli cha Kabila katika utawala wa Kongo hakitaondoka hata kama Emmanuel Shadary atachukua nafasi yake. Utakuwa tu ni  sawa na mchezo wa danganya toto alioucheza wakatii fulani Rais Vladimir Putin wa Urusi.  Yeye alimpisha Waziri Mkuu wake, Dmitry Medvedev, achukue nafasi yake, naye Putin akachukua nafasi ya uwaziri mkuu. Baada ya miaka mitano wakabadilishana tena, mwenyewe Putin akarudi kuchukua wadhifa wa urais aliye na nguvu. Mchezo huu utakuwa ni kupoteza tu wakati, fedha na nguvu. Haunogi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,702FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles