Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Ujenzi wa daraja la Mto Majoka linalounganisha Mitaa ya Kifuru na Kibaga katika Kata ya Kinyerezi umefikia asilimia 60.
Daraja hilo linalogharimu Sh milioni 650 fedha kutoka Serikali Kuu lilianza kujengwa Juni 2023 na linatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu.
Akizungumza Oktoba 5,2023 Mhandisi kutoka Tarura Wilaya ya Ilala, Legnard Mashanda, amesema ujenzi utakamilika kabla ya muda uliopangwa.
Mashanda alikuwa akizungumza baada ya Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kufanya ziara kukagua ujenzi wa daraja hilo.
“Tumeendelea kumsimamia mkandarasi na tulitarajia daraja likamilike Desemba 26 lakini kwa kasi iliyopo tutakamilisha hata kabla ya muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Mashanda.
Amesema kazi zilizobaki ni kuendelea kuufungua mto, kuchonga barabara na kuziwekea vifusi na ujenzi wa mitaro ya pembeni.
Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mgitu, amesema daraja hilo litakuwa na manufaa makubwa kwa kuunganisha mitaa ya Kifuru na Kibaga na kudhibiti mafuriko yaliyokuwa yakitokea awali.
Kwa upande wake Bonnah amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi na kuiomba Tarura kuangalia uwezekano wa kuruhusu watembea wa miguu wakati wakiendelea kukamilisha ujenzi huo.
“Daraja hili tumelipambania na mheshimiwa diwani na wajumbe ambao walikuwa wanapaza sauti zao, niwashukuru watu wa Tarura ujenzi unakwenda haraka,” amesema Bonnah.