32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

UINGEREZA NAO KUISOMA NAMBA

Sir Ivan Rogers
Sir Ivan Rogers

NA LAMECK KUMBUKA, Geneva, Uswisi

KITENDO cha wananchi wa Taifa la Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya kimeleta madhara makubwa. Kama wasemavyo vijana wa siku hizi muziki wa ‘Brexit’ sasa si wa kitoto na hakika umeleta dhahama huko Uingereza.

Tunaweza kuazima msemo uliopo kwenye wimbo wa CCM  ‘wataisoma namba’ ndicho ambacho kinawakuta wananchi wa Uingereza. Waingereza walipopiga kura ya kujiondoa katika Jumuiya ya Ulaya (European Union), waliangalia kwa jicho chongo, hawakufikiria kwa kina athari zake.

Januari 4, mwaka huu, Sir Ivan Rogers, Mwanadiplomasia nguli wa Uingereza amejiuzulu cheo chake kama balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya (EU). Kwa maana nyingine kitendo hicho ni kama ameshtukia dili.

Mjadala juu ya biashara kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya umegubikwa na sintofahamu. Wachambuzi wa mambo wanasema inaweza kuchukua zaidi ya miaka 10 kufikia mwafaka.

Wahenga walisema ukibana vyako usitegemee utakula vya wengine kirahisi. Sir Ivan Rogers kwa lugha nyingine amesema, hawezi kukabiliana na mzigo mzito wa kujitoa EU kwa kuwa alishawatahadharisha mapema. Mwanadiplomasia huyo ametangaza kujiuzulu na kuitaka Uingereza itafute mtu mwingine aiwakilishe.

Nafahamu wengi watasema suala hilo lilikuwa la kidemokrasia na wengi ndio walioshinda. Kimsingi dhana ya wengi wape imekuwa na maswali mengi kuhusu kuhalalisha demokrasia.

Je, kiongozi bora au maamuzi bora ni yale ya wengi au ni yale yanayowakilisha makundi yote yatakayoguswa na hayo maamuzi? Je, kama wengi hao uwezo wao wa kufikiria ni mdogo bado watatoa maamuzi sahihi kisa ni wengi?

Masuala haya yalisababisha Marekani kuja na mfumo ule wa upigaji kura wa wawakilishi wa majimbo (Electoral Vote). Hii inamaanisha kuwa kura za wananchi (Popular/Majority Vote) yaani kura za wengi haziakisi maamuzi au kiongozi bora. Mfumo wa Electoral Vote hupewa kipaumbele kwani ni kura zinazoakisi wawakilishi sehemu tofauti majimbo tofauti yanayoguswa na maamuzi haya.

Ndiyo maana mgombea wa Chama cha Democrat, Hilary Clinton, akapata kura nyingi lakini hakuwa rais. Simaanishi kuwa mfumo wa Marekani ni bora au hutoa viongozi bora ila najaribu kuelezea sintofahamu na mkanganyiko juu ya dhana ya wengi wape na dhana ya demokrasia.

Mantiki ya Electoral Vote kwa Wamarekani ni kuwa kama wingi wa kura utaakisi maamuzi bora au kiongozi ni kwamba tutajikuta katika siasa za ukabila na rushwa.

Mfano, kabila lenye watu wengi huweza kujikuta linatoa kiongozi au wanasiasa wanaligombania kuhonga na kuligombania wakati wa kampeni.

Tushukuru Mungu Tanzania tuna neema, la sivyo dhana hiyo ya wengi wape ingesababisha kila kiongozi kutoka Kanda ya Ziwa kwani kwa kuwa Wasukuma ni wengi basi anayekubalika na Wasukuma angekuwa moja kwa moja kiongozi au maamuzi yanayoungwa na watu wa Kanda ya Ziwa yangepita.

Je, watu wa Kanda ya Ziwa au Wasukuma wakitaka kitu au wakimtaka fulani basi ndio sahihi? Haya ni maswali. Unaona Mungu alivyotujalia tumekuwa na marais kutoka makabila madogo sana ambao hata si maarufu maadamu wanakubalika na wote.

Ona dhana ya wingi inavyoitafuna jirani Kenya. Waluo na Wakikuyu wamekuwa na msuguano miaka nenda miaka rudi hadi kukitishana huo msuguano baba yake Raila Odinga, Oginga Odinga, alipambana kamwachia kijana bado anaendelea.

Pia, dhana ya wengi wape ni hatari kwa nchi ambazo hazijaendelea kama wale wengi ni mbumbumbu. Kwa lugha nyingine maamuzi ya wajinga yanakuwa maamuzi ya taifa zima.

Sina nia ya kubeza dhana ya wengi wape ila najaribu kukueleza athari ya dhana ya wengi na mantiki ya demokrasia. Hii ndiyo inaitafuna Uingereza kwenye sakata la kujitoa EU yaani Brexit.

Mojawapo ya masuala yaliyopeleka Brexit ni uhamiaji. Waliamini kuwa wahamiaji wanachukua kazi na fursa za wazawa Waingereza. Pia wahamiaji wengi hupitia huko Italia na suala la kubeba msalaba (Burden sharing) ndani ya Jumuiya ya Ulaya hujikuta wanabeba mzigo usio wao.

Kuna suala huwa linashangaza Ulaya na nchi za Magharibi, wazee na watu wa vijijini ambako hata hakuna mhamiaji au mgeni anayeishi huko ndio wanaochukia wahamiaji. Kwa lugha nyingine chuki yao ni ya kinadharia na kibaguzi.

Ni sawa na mtu anamchukia mtu ambaye hata hamjui. Nimekuwa nikiishi hapa Geneva, ni jiji kubwa ambalo limejaa wageni kutoka nchi mbalimbali ila wazawa wa jiji hilo huwa hawapigi kura kufukuza wageni.

Hapo ndipo kuna wageni wengi kuliko sehemu nyingine nchini Uswisi. Vijijini ambako wageni hawapo huwa wanaandamana kupinga wahamiaji hayo ndiyo maajabu.

Kwa Marekani, Mmarekani mweusi ambaye hakusoma atamchukia sana Mnigeria au Mghana mhamiaji daktari au mwanasheria aliyebobea eti kamchukulia kazi kana kwamba huyo daktari asingefanya hiyo kazi huyo Mmarekani mweusi anayeshinda anavuta bangi magetoni angefanya hiyo kazi.

Vijana wengi watu wa mjini na wasomi huwa wana uwezo wa kupambanua na wako wazi kimawazo. Kwa bahati mbaya watu hao hao huwa hawako tayari kupanga mstari kwa saa mbili au tatu kupiga kura kutetea yale maamuzi yao.

Watu wa vijijini wazee na wale wasio na elimu maamuzi yao mara nyingi ni ya uzoefu na ya kale ambayo wakati mwingine hayaakisi hali halisi ya maisha tuliyonayo wengi.

Lakini kundi hilo ndilo watu ambao wako tayari kupanga mstari saa tatu huku mvua ikinyesha kupiga kura kwani huwa ni wanazi wa kile wanachokiamini, si wapembuzi. Yaani kama ni kwa soka ndio wale wabongo wanapigana kisa ubishi wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Ndiyo maana siku ya kura ya Brexit mvua ilinyesha na watu wa jiji la London waliotegemewa kura yao iongee hawakupiga kura kwa wingi kisa mvua. Hayo ndiyo maajabu ya siasa, aliye makini ni mvivu wa kupiga kura na humwachia asiye makini aamue hatima ya maisha yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles