24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Uhusiano wa mtoto kunyonya kidole, kinga dhidi ya mzio

kidole

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ASILIMIA 80 ya watoto huanza kunyonya kidole kuanzia wiki ya 13 akiwa tumboni kwa mama, japo wazazi huanza kugundua hilo pindi mtoto anapofikisha miezi miwili hadi mitatu. Pia wapo watoto ambao huanza tabia hii pindi wanapozaliwa.

Mara nyingi huendelea kunyonya kidole mpaka wanapofikisha umri wa miaka mitatu hadi sita.

Hata hivyo, wazazi wengi hupenda kuona watoto wao wakinyonya vidole, ambapo asilimia kubwa hupendelea kunyonya kidole gumba au vidole viwili kwa pamoja, cha shahada na cha kati.

Sababu kubwa ya wazazi kupenda watoto wanaonyonya vidole ni kwamba huwa wapole – hawana tabia ya kulia lia ovyo.

Kwanini mtoto ananyonya kidole?

Kwa mujibu wa madaktari, watoto wengi wananyonya kidole kama mbadala wa kula chakula, au kumbelezwa na wakati mwingine ni kujiweka au kujisikia salama, ni kama tabia tu ambayo mtoto alikuwa nayo tangu akiwa tumboni kwa mama yake, ambapo wanasema hali hii huletwa na hisia.

Madhara

Kunyonya kidole kuna madhara kwa baadhi ya watoto watakaoshindwa kuacha pindi wanapofikisha umri wa miaka minne.

Moja kati ya madhara hayo ni meno kutojipanga vizuri na kuota huku yakiwa yamepanda juu hivyo kushindwa kung’atana.

Wataalamu wanasema kunyonya vidole pia humfanya mtoto kupata tatizo la matamshi na viungo vya mdomo kama ulimi kutoka nje wakati wa kuongea.

Jinsi ya kumsaidia mtoto kuacha

Daktari wa watoto kutoka hospitali binafsi iliyopo Yombo Vituka, Dk. Samil Mohammed, anasema kuwa wazazi huwa wanapata wasiwasi mapema pale mtoto anaposhindwa kuacha kunyonya kidole. Inashauriwa kuwa usimfanye aache kunyonya kidole akiwa na umri chini ya miaka minne isipokuwa tu pale utakapoona kuna tatizo linalojitokeza kwa sababu ya kunyonya kwake kidole.

Anasema kuwa mara nyingi watoto huwa wanaacha wenyewe lakini ikitokea hajaacha hushauriwa kupendelea kumpatia michezo mbalimbali ambayo itaufanya huo mkono anaonyonya wakati wote uwe na shughuli ya kufanya.

Njia nyingine ni wakati akiwa amelala mzazi unapaswa kumtoa kidole chake polepole mdomoni bila kumwamsha.

“Pia unaweza kumpa mifano ya marafiki zake walioacha kunyonya kidole, ili kumtia moyo na yeye aache,” anasema na kuongeza:

“Wakati mwingine unapaswa kuzungumza naye juu ya bakteria wabaya waliopo katika mazingira ya nje ambayo kupitia kidole chake anaweza kuwapata.”

Anasema pia mzazi anaweza kutumia vitu kama ‘bandage’, kumuwekea vitu vichungu au pilipili kwenye kidole anachonyonya huku ukimuelewesha kuwa hiyo si adhabu bali unamsaidia ili meno yake na sura visiharibike.

Anashauri kuwa zoezi hilo linapaswa kufanywa kila siku asubuhi na kabla ya kulala ili atakapoweka mdomoni akutane na ladha mbaya hatimaye kuacha kabisa.

Anasema kuwa njia hii inapaswa kuambatana na zawadi pale atakapoacha ili isiwe kama adhabu kwa mtoto.

Anashauri kuwa mzazi asitumie njia ya kumtisha au kumwogopesha, kwa kuwa kunyonya kwake kidole inaweza kuwa ni tatizo la kihisia au anakuwa na mawazo hivyo anahitaji kufarajika.

Hivyo basi, ni bora kutafuta suluhisho la tatizo alilonalo kabla hujamlazimisha kuacha kunyonya kidole.

Anasema iwapo hivyo vyote vitashindikana, mzazi au mlezi asisite kuwaona madaktari wa afya ya meno ya watoto au daktari yeyote wa meno kwa msaada zaidi.

Wazazi wenye watoto wanaonyonya vidole

Mwantumu Shabani, mama mwenye watoto wanaonyonya kidole anasema watoto wake hufanya hivyo pindi wanapokwenda kulala.

“Mimi nina watoto wawili mapacha wote wananyonya kidole. Hiyo ndio njia yao ya kujibembeleza wakati wa kulala,” anasema Mwantumu.

Naye Mishi Kassim anasema kuwa ana mtoto mwenye miezi 11 ambaye ameanza kunyonya vidole tangu akiwa na miezi miwili.

Mishi anasema kuwa suala la kunyonya kidole ni gumu mno kulijadili kwa sababu mtoto wa

mdogo wake pia alikuwa na tabia hiyo lakini alipofikisha miaka mitatu aliacha mwenyewe.

“Athari aliyoipata mtoto huyo ni kwamba alipoanza kuzungumza alikuwa na kithembe (kutoa ulimi nje wakati wa kuzungumza).
“Kwa kuwa hakuna mtu anayemtuma mtoto kunyonya kidole, nadhani ni vema kumuacha mpaka atakapoamua kuacha kuliko kuingilia saikolojia yake,” anasema.

Mishi anasema kuwa uzuri wa watoto wanaonyonya kidole huwa ni watulivu wakati wote, hawalii ovyo hata wanapokuwa na njaa au usingizi.

Naye Magdalena Joseph, ambaye mwanawe alikuwa akinyonya kidole hadi alipofikisha umri wa miaka saba, anasema kuwa aliacha baada ya kuvalishwa kifaa maalumu cha kumzuia asiendelee.

Anasema mwanawe alikuwa akinyonya kidole muda wote lakini hakuwahi kumkataza akidhani kuwa siku yoyote anaweza kuacha.

“Nilipoona umri unazidi kwenda bila kuacha, nikaanza kumwambia kuwa si vizuri ili aache, lakini ikashindikana.

“Wakati mwingine alikuwa akinyonya kidole akiniona anatoa haraka, lakini sasa ameacha baada ya kuvalishwa hiko kifaa hospitalini,” anasema.

Kwa upande wake Joyce Malima anasema kuwa kunyonya kidole si tatizo lakini mtoto atakapokuwa akinyonya hadi miaka kumi na kuendelea, anaweza kuwa mjinga darasani.

“Iwapo mtoto akiendelea kunyonya kidole hadi miaka kumi huko ni dhahiri kwamba atakuwa mjinga darasani, wengi huwa hawafanyi vizuri kwa sababu anakuwa ‘busy’ na kidole badala ya kumsikiliza mwalimu kwa makini.

Tatizo hilo halihusiani na kukosa akili darasani

Wataalamu wanasema kuwa tatizo hilo halihusiani na mtoto kukosa akili au kupunguza umakini kwenye masomo kama wanavyoamini baadhi ya kina mama.

Pia kitendo hicho hakipunguzi saizi ya kidole kama inavyoaminiwa na wengi, bali hufanya ngozi ya kidole kusinyaa na kuwa ngumu ama nyeusi lakini hali hiyo huisha pindi tabia inapokoma.

Watoto wanaonyonya kidole au kula kucha zao huwa na uwezekano wa kupata kinga dhidi ya mzio unaosababishwa na mazingira .
Watoto wanaonyonya kidole au kula kucha zao huwa na uwezekano wa kupata kinga dhidi ya mzio unaosababishwa na mazingira .

Utafiti watoto wanaonyonya vidole

Utafiti uliofanywa nchini New Zealand, umebaini kuwa watoto wanaonyonya vidole au kung’ata kucha zao kwa meno huenda wasipate uzio (allergy) unaotokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani.

Kwa mujibu wa waandishi katika jarida la Pediatrics, kitendo hicho hujulikana kama usafi dhanio, kwa kuwa kuna vitu vitokanavyo na baadhi ya wadudu ambao huimarisha mfumo wa kinga ya mwili.

Utafiti huo unasema kuwa unyonyaji wa kidole gumba na ung’ataji wa kucha umeonekana kuzuia baadhi ya uzio (allergy).

Katika utafiti huo, watu 1,000 wenye umri wa kati ya miaka mitano hadi 32, walifanyiwa uchunguzi kwa muda nchini New Zealand.

Hata hivyo, umefafanua kuwa tabia hii ya unyonyaji vidole na ung’ataji kucha haisaidii watu wenye pumu au mtu anapopata homa kali.

Uchunguzi huo ulifanywa na kurekodiwa kwa watoto wenye umri wa kati ya miaka mitano na 11; na wengine waliofanyiwa vipimo ni wenye umri kati ya miaka 13 na 32.

Theluthi moja ya watoto hao walikuwa ni wale wanaonyonya vidole mara kwa mara au hung’ata kucha zao. Katika vipimo walivyofanyiwa walionekana kuwa wana kiwango kidogo cha kuathirika kutokana na mazingira hewa au kula vyakula fulani.

Imebainika kuwa watoto wanaoweza kupata uzio unaotokana na vitu kama vumbi kutoka majumbani, manyoya ya paka au mbwa, kama wananyonya vidole gumba na kung’ata kucha hawawezi kuathirika.

Tabia za watoto wanazoonyesha baada ya kuzaliwa

Dk. Mohammed anasema kuwa kuanzia miezi 0-1; watoto huweza kufanya matendo yasiyo ya hiari ambayo hajafundishwa. Mfano; kunyonya maziwa ya mama, kufumbua na kufumba macho.

Pia katika umri huu lugha kuu anayotumia huwa ni kulia pindi anaposikia njaa na kutabasamu au kucheka pindi anapofurahi.

Anasema mwezi mmoja hadi minne huwa anapenda kurudia kufanya vitu ambavyo anaona vinamfurahisha kama kunyonya kidole kwa mara ya kwanza bila kukusudia, lakini baada ya muda anarudia kwa sababu aligundua kuwa anapata raha pindi anaponyonya vidole vyake.

“Miezi mitatu hadi nane, huwa na tabia ya kurudia jambo kwa makusudi ili kujua matokea ya kufanya kitendo hicho.

“Mtoto anaweza kujaribu kuinua kifani (toy) cha kuchezea na kujaribu kuweka mdomoni ili aone kama kinaweza kumpa raha kama anaponyonya ziwa la mama au kidole chake,” anasema.

Daktari huyo anasema kuwa kuanzia miezi nane hadi 12 mtoto huwa na tabia ya kufanya utafiti katika mazingira yanayomzunguka.

Pia huiga vitendo au tabia anazoona kwa watu wengine au watoto wenzake pindi anapocheza. Hapo ndipo hugundua vitu mbalimbali na tabia zake.

Anatoa mfano kuwa mtoto anaweza kugundua kuwa akiangusha kijiko kinatoa mlio kinapofika kwenye sakafu, hivyo atajaribu kuangusha vitu vingine zaidi kama vikombe ili kujua kuwa navyo vitatoa sauti au la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles