26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Uhusiano kati ya Tanzania na Mataifa mengine umeimarika-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine umeendelea kuimarika kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambae ameendelea kufanya ziara katika nchi mbalimbali sambamba na viongozi wakuu wa nchi hizo na Mashirika ya Kimataifa kuzuru Tanzania.

Amesema katika kipindi kifupi ziara zilizofanywa na Rais zimeiwezesha Nchi kupata manufaa makubwa ikiwemo kuingiwa kwa makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali kama vile miundombinu, nishati, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, michezo, kilimo na uwekezaji.

”Pamoja na mafanikio yote hayo ya kiuchumi, Tanzania imefanikiwa kuzishawishi Nchi Wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa Februari 18, 2022) wakati akiahirisha Mkutano wa sita wa Bunge la kumi na mbili (12) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema  lugha ya Kiswahili hainabudi kuwa chachu ya kukuza ajira kwa wakalimani, walimu wa ngazi zote, mauzo ya vitabu, filamu na aina nyingine za sanaa.

Nitoe wito kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Balozi zetu nje kuja na mikakati maalumu ya kukiendeleza Kiswahili hususan nje ya mipaka ya Tanzania ikiwemo kufungua madarasa ya kufundisha kiswahili na kuimarisha ushirikiano na wadau binafsi wenye kuendesha vituo vya kiutamaduni vya kufundisha Kiswahili,” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewaeleza waheshimiwa wabunge kuwa Serikali imekuwa na utekelezaji mzuri wa bajeti hadi kufikia asilimia 86.2 ambapo fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha Sh trilioni 5.19 ya fedha za ndani na Sh bilioni 167.1 ya fedha za nje na Sh bilioni 443.7 ni fedha za Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa Wananchi.

Aliongeza kuwa, utekelezaji huo wa bajeti umeenda sambamba na kukua kwa makusanyo ya kodi ambapo katika mwaka huu wa fedha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliweza kuvunja rekodi ya makusanyo ya kodi kwa kukusanya jumla ya Sh trilioni 2.3, sawa na asilimia 103.1 ya lengo, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa na TRA kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Majaliwa amesema kuwa kwa upande wa matumizi, ridhaa ya matumizi iliyotolewa katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020 ni Sh trilioni 16.50 sawa na asilimia 90.5 ya lengo.

“Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 11.14 ni fedha za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 96.9 ya lengo na Sh trilioni 5.36 ni fedha za maendeleo, sawa na asilimia 79.6,” Alisema na kuongeza.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa tuna kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwenendo huo mzuri katika utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2021.”

Aliongeza kuwa mafanikio ya makusanyo na utekelezaji wa bajeti yametokana na Jitihada za Mheshimiwa Rais katika kuvutia uwekezaji, kuhamasisha utalii, biashara na kusimamia ukusanyaji wa mapato zimechangia kuongezeka kwa makusanyo ya mapato ya kodi na kuimarika kwa uchumi hapa nchini.

Akitoa pongezi kwa Utendaji wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Waziri Mkuu amewasihi Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwa nia ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

“Waswahili hunena mwenye macho haambiwi tazama. Sote tu mashuhuda wa mafanikio hayo sambamba na maeneo mengine ambayo kiuhalisia yanaakisi kazi nzuri inayofanywa na Nitoe wito kwa Watanzania wote kuendelea kumuunga mkono kwa moyo wa dhati ili aweze kutimiza azma yake ya dhati ya kujenga uchumi imara, shindani na endelevu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watendaji wa TARURA kusimamia  kwa karibu na kwa umakini kazi zinazofanywa na wakandarasi kwa ajili ya kubaini mapema na kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa mujibu wa mikataba na kutaka Ufuatiliaji ufanywe mara kwa mara ili miradi ikamilike katika muda uliopangwa na kwa ubora stahiki.

“Watumishi wa TARURA jiepusheni na kazi zenye mgongano wa maslahi. Kwa mantiki hiyo, ikiwa unataka kufanya biashara na Serikali wakati wewe ni mtumishi wa umma ni vyema ukaacha kazi ili ufanye biashara yako kwa ufanisi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles