NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta alijibu maswali ya mashabiki katika ukurasa wake wa Facebook juzi asubuhi, ambapo pamoja na mambo mengine alitetea rekodi ya serikali yake akisema haijaachwa nyuma na Tanzania linapokuja suala la usafiri wa umma.
Ikiwa ni siku moja kabla ya mdahalo wa urais, ambao awali timu yake iliashiria kutohudhuria kabla ya baadaye jana kufuta ratiba ya kampeni katika eneo la Samburu, Rais Kenyatta siku hiyo alichagua kuzungumza na mashabiki, tukio lililotangazwa moja kwa moja na vituo vya KBC na K24 TV.
Mkuu huyo wa taifa alijibu maswali yaliyotumwa kabla na ambayo yeye na timu yake walichagua ya kujibu.
Maswali hayo yaliangazia masuala ya uchumi, rushwa na chaguzi zijazo na maendeleo ya miundo mbinu.
Kenyatta aliwataka mashabiki wake milioni tatu wa Facebook pamoja na wafuasi kuombea amani uchaguzi mkuu ujao huku akiwasihi wampe nafasi nyingine ya kuongoza Kenya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akifahamu kuwa asilimia 51 ya wapiga kura milioni 19.6 ni vijana wa miaka kati ya 18 na 35, Rais Kenyatta alitengeneza majibu yake yaliyowalenga vijana akieleza kwanini serikali yake ndiyo jibu la matatizo yao.
Alitolea mfano wa miradi ya reli ya kiwango cha Standard Gauge (SGR), barabara, umeme kuwa itatengeneza mamilioni ya ajira kwa ajili yao.
“Tuna mpango wa kujenga mtandao mwepesi wa reli kwa ajili ya usafiri wa umma jijini Nairobi, kuipanua SGR hadi Naivasha, Narok, kisha Kisumu,” alisema, akijibu swali la mtumiaji mmoja wa Facebook aliyekosoa Kenya kuachwa nyuma na Tanzania linapokuja suala usafiri wa umma.
“Na wala hatujaachwa nyuma, bali tuko katika ratiba,” alisema.
Kuhusu Ufisadi, Rais Kenyatta alitetea rekodi yake akisema dhamira ya serikali yake kupambana na rushwa iko wazi.
“Serikali yangu ni ya kwanza kuanzisha mpango unaohusisha mashirika mbalimbali kushughulika na ufisadi. Na kutokana na hilo nimepoteza marafiki wa karibu, mawaziri.”
Ushirika wa upinzani National Super Alliance (Nasa) ukiongozwa na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga wameufanya ufisadi kuwa ajenda kuu ya kampeni yao.