28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

UHURU AWATAKA AKINA RAILA KUFUATA SHERIA KUPINGA MATOKEO

NAIROBI, KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka wanasiasa wote walioshindwa na kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumanne wiki iliyopita, kuchukua hatua za kikatiba ili malalamiko yao yashughulikiwe.

Pia amewataka maofisa wa polisi kuwa makini wanaposhughulika na maandamano ya amani kwa vile waandamanaji wanafanya kwa mujibu wa sheria kutokana na kutofurahishwa na matokeo.

Akizungumza kutokea Harambee House jana, Kenyatta alisema: “Nawaomba wale wote waliokataa matokeo watambue kwamba wote ni Wakenya, nanyoosha mkono wa amani na urafiki kwao.

“Polisi wako tayari kutoa ulinzi wakati wa maandamano ya amani na wale wasiokubali matokeo hawahitaji ruhusa yangu au ya chama cha Jubilee kuendesha maandamano hayo ya amani.”

Hata hivyo, alionya kwamba Serikali haitavumilia upotevu wowote wa maisha na uharibifu wa mali unaotokana na maandamano yanayoambatana na ghasia.

Kenyatta alionya zaidi wale wanaopora na kuharibu mali katika baadhi ya maeneo ya nchi, ambako maandamano ya baada ya uchaguzi yaliripotiwa.

“Wakenya wengi wanatamani kurudi katika maisha ya kawaida. Hawataki maandamano ya vurugu,” alisema.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Agosti 8 baada ya kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura.

Mpinzani wake mkuu, Raila Odinga wa muungano wa NASA, alipata kura 6,762,224.

Lakini Raila, ambaye alikataa matokeo hayo, akisema uchaguzi ulijaa udanganyifu, licha ya waangalizi wa kimataifa kuusifu, tayari amesisitiza kutoenda mahakamani badala yake watachukua hatua nyingine.

Raila ambaye juzi aliwahimiza wafuasi wake kutoenda kazini jana ili kuomboleza watu waliouawa wakati wa maandamano, leo huenda akatangaza hatua hizo kama alivyoahidi juzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles