NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta ana uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa kwa mara ya pili kama rais wa Kenya.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti mpya wa Centre for African Progress (CAP), Uhuru angeshinda kwa asilimia 53 ya kura, huku mpinzani wake, Raila Odinga akipata asilimia 42.
Baadhi ya waliomuunga mkono Rais Uhuru, walimsifu kwa utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya kiwango cha Standard (SGR), matibabu bila malipo kwa wajawazito na mradi wa laptop kwa watoto wa darasa la kwanza.
Waliomuunga mkono Raila Odinga walimsifu kwa mchango wake katika kuundwa kwa barabara kuu ya Thika.
Kati ya waliohojiwa, asilimia 85 walithibitisha kuwa watashiriki uchaguzi wa Agosti 8, huku asilimia 10 wakisema kuwa hawatoshiriki.
“Ukitumia kiwango ambacho kila mgombeaji angepata kama ni wapigakura asilimia 85 tu watakaojitokeza, Uhuru atapata kura 7,971,630, Raila akitarajia kupata 6,289,426,” ulisema utafiti huo.
Aidha asilimia 56 ya waliohojiwa walisema kuwa wanaamini Tume Huru ya Uchaguzi na Mipakan (IEBC) itaendesha uchaguzi kwa njia ya huru na haki.