22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru anapowaweka karibu Ruto, Raila

ISIJI DOMINIC

RAIS Uhuru Kenyatta, anaongoza kwa mfano akijaribu pia kuondokana na utamaduni uliozoeleka na wanasiasa kutumia misiba kujiendeleza kisiasa.

Hivi majuzi, Taifa la Kenya lilikumbwa na misiba miwili mizito kufuatia kifo cha Gavana wa Kaunti ya Bomet, Dk. Joyce Laboso na Mbunge wa Kibra, Ken Okoth. Wanasiasa hawa wawili ambao walisifika kwa uchapakazi wao waliaga dunia baada ya kuugua saratani.

Rais Uhuru aliongoza Wakenya katika kuaga mwili wa Laboso na kama ilivyotarajiwa, baadhi ya wanasiasa walipopewa nafasi kutoa risala za rambirambi, walipiga siasa iliyozunguka fedha zilizotengwa kwa kaunti na mswada wa thuluthi mbili ya wanawake bungeni na pia uteuzi serikalini na sekta za umma.

Hata hivyo, Rais Uhuru alikwepa kujibu hoja hizo tena kwenye mazishi na badala yake kusisitiza Serikali yake itaimarisha vituo vya afya maeneo mbalimbali nchini Kenya ili kupambana na ugonjwa wa saratani unaoondoa uhai wa watu wengi ukizingatia pia gharama za matibabu yake yapo juu.  

Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, alimkumbuka marehemu Dk. Laboso kwa namna alivyoendesha siasa za ukomovu zilizolenga kuwaunganisha wananchi.

Ni kauli ambayo pia iliungwa mkono na Naibu Rais William Ruto, ambaye alitumia fursa hiyo mbele ya bosi wake, Rais Uhuru, kumhakikishia Raila kufanya naye kazi licha ya hapo awali mara kadhaa kupinga ushirikiano kati ya Raila na Uhuru.

Ruto amekuwa akipinga mapatano kati ya Uhuru na Raila ambayo inasadikiwa kuleta mpasuko ndani ya Chama cha Jubilee na alishawahi kumshutumu Raila kuwa na nia mbaya ya kuihujumu chama tawala.

“Nataka nikuhakikishie kaka yangu Raila Odinga kwamba, tutafanya kazi pamoja chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kuunganisha nchi yetu,” alisema Naibu Rais.

Muda mchache tu baada ya kumzika Dk. Laboso, Rais Uhuru, naibu wake Ruto na Raila kwa pamoja walifanya ziara ya kushutukiza kwa mara ya kwanza katika bandari kavu ya Kisumu kukagua maboresho ya ujezi yanayoendelea kabla ya uzinduzi wake unaotarajiwa kufanyika mwezi huu.

Watatu hao inadaiwa bila kutumia magari rasmi ya serikali na wakiwa na kikosi kidogo cha walinzi, walikutana katika moja ya hoteli za kifahari jijini Kisumu kupata chakula, ambapo pia walizungumza masuala kadhaa yanayogusa mahitaji ya taifa.

Je, kitendo hiki kitaashiria hususan Ruto na Raila sasa kuwacha kujibizana hadharani na kushughulikia maendeleo ya taifa ikiwamo utekelezaji wa ajenda nne kuu alizoainisha Rais Uhuru?

Wawili hawa wanatajwa kuwania urais 2022 na wapopimana ubavu kwenye majukwaa ya siasa linapokuja suala la vita dhidi ya ufisadi, mara nyingi wanaziweka mamlaka husika katika wakati mgumu.

Raila amejikuta akipata sapoti kutoka sehemu ya wanasiasa wa Jubilee waliopachikwa jina la Kieleweke, wanaounga mkono umoja kati ya Raila na Uhuru, wakati kundi jingine linaloitwa Tanga Tanga linalohusishwa na Naibu Rais linadai Raila anampango wa kufuta ndoto za Ruto urais 2022.

Lakini Ruto anaonekana kuchukua njia tofauti akiwashawishi wanasiasa waliyopo Tanga Tanga na Kieleweke ndani ya Chama cha Jubilee kuacha siasa ya kugawanya kwa lengo la kuelekeza nguvu zao kwa miradi ya maendeleo na pia kumuunga mkono Rais Uhuru.

“Nataka niwashawishi Wakenya na hususan viongozi wa Jubilee kuacha kugawanyika kwa sababu sisi ni timu moja, tunaye kiongozi mmoja na manifesto moja hivyo, tuungane kutekeleza ahadi za Rais alizotoa kwa Wakenya,” alisema Ruto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles