NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta juzi alikiri kuwa anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga katika harakati za kutetea kiti chake cha urais.
Kutokana na sababu hiyo, Kenyatta aliwataka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura, akisema hilo ni pekee linaloweza kumuokoa.
“Nasaka kura za urais lakini kuna mtu, ambaye kila mara ananihangaisha. Vijana mkishindwa kujiandikisha kuwa wapiga kura nitapata shida sana,” Rais Kenyatta alisema mjini Maua, Kaunti ya Meru.
Baada ya kutoa kauli hiyo Rais Kenyatta alianza kuzungumza kwa lugha ya Kikuyu, na kuuliza: “mtakubali kuniangusha.”
Kwa ishara ya mikono yao, umati ulikubali kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kumpigia kura Rais Kenyatta.
Kenyatta alipopitia katika baadhi ya maeneo ya Igembe na Tigania umati uliimba “PNU” na “Munya” baada ya msafara wa rais kupita.
Gavana Peter Munya ndiye kiongozi wa Chama cha PNU kilicho mshirika mkuu wa muungano wa Jubilee, alitoa changamoto kwa chama hicho kuvutia wapigakura.
Hata hivyo, katika mkutano wa Kianjai umati haukuweza kuchangamka wakati Rais alipowataja Seneta Kiraitu Murungi na Mwakilishi wa Wanawake Florence Kajuju waliokuwa kwenye msafara wake.
Badala yake umati ulimfurahia mshauri wa Rais Kilemi Mwiria ambaye ametangaza kuwania kiti cha ugavana wa Meru.