WASIOKUWA NA VYOO IGUNGA KUKAMATWA

Na Abdallah Amiri-Igunga


 

chooMKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora,  John Mwaipopo amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani hapa kuwasaka na kuwakamata wananchi wote wasiokuwa na vyoo katika nyumba zao.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani hapa, wakati akizungumza na wananchi baada ya uzinduzi wa Kituo cha Afya Choma pamoja na jengo la upasuaji, ambapo alisema wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakijisaidia kwa kuchimba mashimo mafupi, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Alisema kitendo hicho kimekuwa kikisababisha kuenea kwa ugonjwa wa matumbo.

“Kuanzia sasa kila mtendaji wa kijiji na kata anatakiwa kuwakamata watu wasiokuwa na vyoo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na mtendaji atakayeshindwa kutekeleza agizo hili hatua kali zitachuliwa dhidi  yake,” alisema DC Mwaipopo.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga,  Godfrey Mgongo alisema jengo hilo la upasuaji lilianza kujengwa mwaka 2012 na Kampuni ya Lukolo Construction Ltd ya jijini Dar es salaam na kukamilika 2015.

Alisema ujenzi wa jengo hilo umefadhiliwa na Benki ya Afrika kupitia mradi wa kupunguza vifo kutokana na uzazi (Maternal Mortality Reduction).

Mgongo alisema uwepo wa jengo hilo litawawezesha akinamama wanaohitaji huduma ya upasuaji kupata huduma papo kwa hapo badala ya kwenda Hospitali ya Mission ya Nkinga au hospitali ya wilaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here