33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UHAMIAJI: UHABA WA WATUMISHI, FEDHA UNATUKWAMISHA


FEBRUARI mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Anna Makakala kuongoza Idara ya Uhamiaji ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mwandishi Wetu Nora Damian amefanya naye mahojiano akielezea changamoto, mikakati na matarajio yake.

Swali: Wakati unaapishwa Rais Dk. Magufuli alikuagiza ukaisafishe Idara ya Uhamiaji je, sasa hivi hali ikoje?
Jibu: Tumeondoa dhana ya kufanya kazi kwa mazoea, tumejitahidi kufanya mabadiliko ya kimfumo kwa kuangalia wale waliofanya kazi muda mrefu sehemu moja. Kwa sasa hata sura na utendaji wetu umebadilika.
Mbali ya kufanya mabadiliko ya rasilimali watu, pia tumefanya mabadiliko ya kimfumo ili kuongeza tija katika utendaji.

Tunabadilisha mfumo wote kwa kuangalia taaluma ya mtumishi na uwezo wa kazi husika na wale tuliowahisi kujihusisha na vitendo vya rushwa tumefanya uchunguzi, kuna watu wamepoteza kazi zao kwa sababu ya rushwa.
Kuna ambao tumewapeleka Takukuru na kesi zao zinaendelea kwa hiyo si kitu cha siri. Kuna mamlaka mbalimbali zinawachunguza na taratibu za mashtaka zinaendelea.

Tumejaribu kuelimisha wananchi kwamba siku hizi hatutumii wakala kutoa huduma zetu badala yake mwananchi hupata huduma za uhamiaji pindi anapofika katika ofisi zetu na kufanya malipo au kwa njia ya mtandao.

Hivyo, ile hali ya kusema ukija unapanga foleni na kuzungushwa hadi anajiingiza kwenye rushwa hilo halipo tena.
Vilevile kuna watu ambao walikuwa na vibali feki pia wametoa ushirikiano mzuri kwamba walivipata wapi na baada ya uchunguzi tulishika ofisi na mitambo.

Kuna kesi mbili ambazo watumishi wetu walitajwa kushiriki kutoa vibali feki na zenyewe zinaendelea huku nyingine zikiwa zipo chini ya Takukuru.
Katika kundi la watu wengi, kuna wachache wanaojihusisha na vitendo vya rushwa hivyo lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe.

Wito wangu tufanye kazi kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za uhamiaji bila kutoa upendeleo au kuonea watu wengine, tutumie nafasi zetu kwa manufaa ya Taifa na kudumisha umoja wetu.
Changamoto zipi zinaikabili idara kwa sasa?
Jibu: Ziko changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yetu. Tuna uhaba wa watumishi, fedha, vitendea kazi kama vile magari, pikipiki na boti kwa ajili ya doria katika maeneo ya majini.
Changamoto hizi zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbalimbali ili tuweze kuongeza ufanisi katika kuimarisha usalama wa nchi.

Swali: Tatizo la wahamiaji haramu likoje?

Jibu: Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu. Tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ambapo taarifa zao zimesaidia kuwakamata wahamiaji haramu.

Kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu tumewakamata zaidi ya wahamiaji haramu 5,700 na kuwaondosha nchini.

Idadi hii ni kubwa na hawa tumewapata kupitia misako na doria tunazozifanya ndani ya nchi, tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano hasa kwa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu kwa sababu Tanzania imezungukwa na nchi jirani nyingi na mipaka ni mikubwa hivyo udhibiti wake unahitaji nguvu za ziada.

Pia tumepokea maombi kutoka kwa wakuu wa wilaya na mikoa mbalimbali ya kufunguliwa ofisi katika maeneo yao kwa lengo la kudhibiti wahamiaji haramu.

Swali: Mfumo upi unatumika kutoa vibali vya ukaazi?
Jibu: Masharti ya kupata vibali hivyo ni lazima mwombaji apewe kibali cha kazi kutoka idara ya kazi isipokuwa kwa makundi maalumu ambayo yameruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Tumeanzisha mfumo wa kuhakiki vibali vya ukaazi kwa wageni kwa njia ya kielektroniki na kwa kiasi kikubwa utasaidia kudhibiti vibali feki.

Kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, Tumetoa vibali 11,369 na kati ya vibali hivyo, 1,047 ni hati za ukaazi daraja A, 6,681 hati za ukaazi daraja B, 3460 hati za ukaazi daraja C, 178 vibali vya wanafunzi na vibali vitatu vilitolewa kwa wageni walowezi.

Swali: Kwanini kufufua hati ya kusafiria kunaleta usumbufu kama mtu anaomba upya?

Jibu: Mtumiaji analazimika kujaza fomu na kuwasilisha nyaraka upya kwa lengo la kujiridhisha kwa sababu uhakiki kwetu ni kitu muhimu.
Hati ya kusafiria ina uhai wa miaka 10 si kwamba hatuna kumbukumbu lakini kwa ajili ya kujiridhisha huwa tunamtaka mtu alete nyaraka upya.
Watu wasione kama tunawasumbua, kuna ambao waliwahi kupata hati lakini baada ya kufanya verification (uhakiki) unakuta kuna vitu vingine vilifanyika na mara ya pili unaweza kumshika.

Swali: Mna mkakati gani wa kukabiliana na tatizo la hati feki za kusafiria?
Jibu: Tupo mbioni kuanzisha hati mpya za kusafiria za kielektroniki zinazoitwa ‘Pasport mtandao’ zitakazokuwa na kadi zenye taarifa za mtumiaji husika.

Uamuzi wa kuanzisha hati hizi umetokana na makubaliano yaliyopitishwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuimarisha ulinzi na usalama.
Kuna mabadiliko ya kiteknolojia katika dunia na ukiangalia katika nchi zilizoendelea tayari wenzetu walishaanza muda mrefu.

Hati hizi ni salama zaidi, zina vigezo vikubwa vya ulinzi na ndani kutakuwa na kadi ambayo ikiingizwa kwenye mashine taarifa zote za mtumiaji zitaonekana hivyo, mtu hawezi kufanya ujanja wowote na akijaribu atakuwa ameiharibu hati.

Hati hizi zinatarajiwa kuanza kutolewa miaka miwili ijayo na matumizi yake yataenda sambamba na hati za sasa hadi hapo za zamani zitakapomalizika.

Pia tayari idara imeanza mchakato wa kubadilisha mfumo wa utoaji viza ambapo sasa itatoa viza za kielektroniki (e-viza) ili kudhibiti mapato yanayotokana na mfumo wa utoaji viza katika viwanja vya ndege.
Tulikuwa tunatumia benki lakini sasa watu wanatumia ‘credit card’ hizi ni hatua za muda mfupi, kutakuwa na viza mtandao ambayo itaondoa haya mambo yote.

Swali: Utekelezaji wa agizo la kuwataka wastaafu warejeshe hati za kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia ukoje?
Jibu: Hadi sasa zaidi ya vigogo 100 wastaafu wamerejesha na takwimu hizo ni kwa hati zilizorejeshwa Makao Makuu ya Uhamiaji kwa sababu kuna wengine wamerejesha kupitia ofisi zetu za wilaya na mikoa.

Sheria ya Pasport ya mwaka 2002 inataja watu wanaopaswa kupata hati zenye hadhi ya kidiplomasia na baada ya kustaafu muhusika anatakiwa airejeshe kwani kuendelea kukaa nayo ni kinyume cha sheria.
Swali: Je, utaratibu upi unatumika kuzuia ukiukwaji wa sheria?
Jibu: Tumeimarisha udhibiti wa kanzidata ya wageni, wanaoingia na kutoka na wanaoishi na kuhakikisha tunawafungulia mashitaka wageni wote wanaokwenda kinyume na taratibu na sheria za nchi.

Swali: Watanzania watarajie nini kutoka kwako?

Jibu: Tumejipanga kuimarisha zaidi mfumo wa utoaji huduma ili kuifanya idara kuwa miongoni mwa taasisi za serikali zinazotekeleza kwa vitendo malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa ya kuondokana na mfumo wa kianalojia na kuekelea kwenye mfumo wa kidigitali tutaweza kuzikabili changamoto mbalimbali na usumbufu kwa wateja utapungua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles