Na Mwandishi wetu-Dar es Salaam
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kijamii na Taasisi za Kidini, itaanza kufanya uhakiki wa jumuiya na taasisi hizo awamu ya nne.
Uhakiki huo utahusisha mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Simiyu, Kagera na Shinyanga kuanzia Oktoba 7 hadi 18.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu, ilisema uhakiki katika mikoa hiyo utafanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
“Katika uhakiki huo, Jumuiya na Taasisi husika zinapaswa kuwasilisha nyaraka mbalimbali, huu ni mchakato endelevu ambao unahusisha mikoa yote nchini,” alisema.
Alisema nyaraka hizo ni cheti halisi cha usajili na kivuli cha cheti hicho, stakabadhi ya mwisho ya malipo ada iliyolipwa hivi karibuni na katiba ya jumuiya au taasisi husika.
Katiba hiyo ni ile iliyopitishwa na msajili, barua ambayo inathibitisha uwepo wa jumuiya au taasisi husika kutoka kwa ofisa mtendaji wa mtaa, kata mahali ilipo ofisi ya jumuiya au taasisi, taarifa ya mkutano mkuu wa mwaka na fedha ya mwaka.
“Fomu ya uhakiki inapatikana katika tovuti ya wizara hiyo sambamba na kwenye kituo cha uhakiki,” alifafanua.
Meja Jenerali Kingu alisema taasisi ambazo zitashindwa kuhakikiwa kwa mujibu wa ratiba ya eneo husika, zitalazimika kwenda Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma kwa ajili ya uhakiki na kama zitashindwa kufanyiwa uhakiki kwa muda uliopangwa, zitaondolewa kwenye daftari la msajili.
Alisema taasisi za dini na jumuiya ambazo hazijasajiliwa zinatakiwa kufika wakati wa uhakiki ili ziweze kupewa utaratibu wa kupata usajili.