Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inakabiliwa na uhaba wa walimu katika baadhi ya vitengo vya wenye ulemavu hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kufikiwa.
Shule hiyo yenye wanafunzi 534 kati yao 114 wana ulemavu wa aina mbalimbali lakini katika kitengo cha wenye ulemavu wa akili na viziwi wasioona vina upungufu wa walimu na walezi.
Wakizungumza na Mtanzania Digital shuleni hapo kwa nyakati tofauti Mkuu wa Kitengo cha Wenye Uziwi Wasioona, Mwalimu Maura Adriano, amesema kina wanafunzi 15 na walimu watano wakati uwiano ni mwalimu mmoja kwa mwanafunzi mmoja.
“Athari yake ni kubwa kwa sababu mwalimu mmoja anaweza kumfundisha vizuri mwanafunzi mmoja, lakini wakiwa wanafunzi watatu na mwalimu mmoja unaweza kumfundisha mmoja lakini mwingine anaendelea na shughuli zake kwa sababu mikono yako inakuwa kwa mtu mmoja, utakapomuacha huyu na mwingine ataendelea na shughuli zake,” amesema Mwalimu Adriano.
Kwa kawaida wenye ulemavu wa kutoona na uziwi huwasiliana kwa kutumia lugha mguso ambayo inatumia ngozi kuwasiliana, ina mkono wa kusema na mkono wa kusikiliza.
Mwalimu huyo ameshauri Serikali ianzishe programu ya mafunzo ya ualimu wa viziwi wasioona ili kukabili upungufu uliopo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Wenye Ulemavu wa Akili, Mwalimu Ng’anzi Isihaka, amesema kitengo hicho ambacho kina wanafunzi 60 kina uhaba wa walimu 12 kwani kwa sasa kina walimu wawili na mlezi mmoja.
Amesema katika kitengo hicho uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano na kuiomba Serikali iwaongezee walimu na walezi.
“Watoto wenye ulemavu wa akili kuna ambao wana tabia ambazo ni ngumu kidogo kama kupigana na kuumizana, tuna mlezi mmoja na watoto ni wengi kwahiyo kuwamudu wote ni kazi. Walimu tumebaki wawili na tuna madarasa matatu ya hatua ya tatu, pili na ya awali kwahiyo hatutoshelezi,” amesema Mwalimu Isihaka.
Akizungumzia changamoto hiyo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema Serikali inaendelea kuajiri walimu wa elimu maalumu kukabili upungufu uliopo kwenye shule mbalimbali.
Kwa mujibu wa Ummy, kati ya walimu 6,749 wa shule za msingi na sekondari walioajiriwa Juni mwaka huu, 401 ni wa elimu maalumu.