25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Uhaba wa maji unavyowatesa wananchi Misenyi

Dumu moja la maji linauzwa kati ya Sh 500 hadi 700.
Dumu moja la maji linauzwa kati ya Sh 500 hadi 700.

Na Kulwa Mzee, aliyekuwa Kagera

WILAYA ya Misenyi ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Kagera ambayo ilianzishwa mwaka 2007 kutokana na maeneo ya Wilaya ya Bukoba Vijijini.

Wilaya hiyo imepakana na Uganda upande wa Kaskazini, Ziwa Viktoria upande wa Mashariki na Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera uko upande wa Kusini.

Eneo la wilaya liko upande wa Magharibi ya Ziwa Viktoria. Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 202,632.

Kata zilizopo katika wilaya hiyo ni Bugika, Bugorora, Buyango, Bwanjai, Gera, Ishozi, Ishunju, Kakunyu, Kanyigo, Kashenye, Kassambya, Kilimilile, Kitobo, Kyaka, Mabale, Minziro, Mushasha, Mutukula, Nsunga na Ruzinga.

Mkoa wa Kagera umekumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu kupoteza maisha pamoja na kukosa makazi ya kuishi Septemba mwaka huu.

Watanzania wanaitambua adha iliyowakumba wakazi wa mkoa huo na jitihada mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha waliokosa makazi wanapata na wale ambao nyumba zao zimepata nyufa zinarudi katika hali ya kawaida.

Pamoja na adha ya tetemeko wananchi wa mkoa huo hasa maeneo ya vijijini wako hatarini kupata maradhi mbalimbali ya milipuko kwa sababu ya ukosefu wa maji safi na salama.

Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Dk. Diodorus Kamala, kwa kutambua adha wanayokumbuana nayo wapigakura wake alifanya ziara kusikiliza kilio cha wananchi katika vijiji mbalimbali.

Wananchi katika maeneo hayo wako zaidi ya 10,000 lakini wenye uwezo wa kufanya kazi ni zaidi ya 3000, idadi iliyobakia ni wazee, wagonjwa na watoto.

Mtanzania ilifanya mahojiano na baadhi ya wananchi wanaokosa maji kwa nyakati tofauti ambapo mkazi wa Kijiji cha Kilimilile, Yusuph Ally, anasema alianza kuishi katika kijiji hicho tangu mwaka 1977 na tangu wakati huo tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa maji.

“Tunapata afya njema kwa sababu ya maji, Kilimilile badala ya kupata maji safi na salama tunapata maji taka, tunapoteza nguvu kazi kubwa kwa ajili ya kusaka maji.

“Siasa zimeshamalizika baada ya uchaguzi tusubiri miaka mitano ijayo, Serikali inashindwa kusimamia miradi ya maji inayokabidhi, wananchi tunataabika kwa kukosa maji,”anasema.

Mkazi huyo anaomba wachimbiwe mabwawa mawili ili kupunguza adha ya ukosefu wa maji.

Mkazi mwingine Esther George, anasema ili mtu aweze kupata maji lazima anunue dumu moja la lita 20 ambalo huuzwa kati ya Sh 500 hadi Sh 700.

“Kwa hali hii utanunua madumu mangapi yaweze kutosheleza mahitaji ya familia, ugumu wa fedha unatufanya tushindwe kumudu kununua maji ya kutosha,” anasema Esther.

Anasema visima vipo lakini havitoi maji kwa sababu mbalimbali ikiwemo pampu kushindwa kufanya kazi.

“Maisha yetu na watoto yako hatarini, hatuwezi kuwa na afya njema bila kuwa na maji na kama hali hii ikiendelea hatujui tutafika wapi.

“Tunahitaji msaada wa Serikali pamoja na Mbunge wetu, wataalamu wa maji hatuelewi wanafanya nini,”anasema.

Diwani wa Kilimilile, Victor Mngoda, anasema siasa zilishamalizika lakini bado kuna watu wanafanya siasa badala ya maendeleo.

“Gharama za kuendesha mradi wa maji ni kubwa kwa sababu mashine iliyofungwa ni kubwa, mradi unatakiwa uwe wa kuongeza kipato,” anasema Mngoda.

Anasema aliingia madarakani na kuikuta hali hiyo lakini kwa kushirikiana na wapenda maendeleo jitihada mbalimbali zinafanyika kuhakikisha maji yanapatikana japo jitihada hizo hazijazaa matunda.

Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Dk. Kamala anasema tatizo kubwa katika miradi ya maji ni wataalamu wanaosimamia ambao uwezo wao ni mdogo.

Anasema miradi yote inashughulikiwa na wataalamu wa wilaya na matatizo yapo katika miradi yote.

“Nimejiridhisha kwamba watalaamu ndio wanaokwamisha miradi, kuna haja ya kutumbuliwa,”anasema Dk. Kamala.

Anasema hakuna ubishi kwamba maji ni muhimu na bila maji hakuna kinachoweza kufanyika lakini suluhisho la tatizo la miradi ya maji ni kuwatumbua wataalamu wenye uwezo mdogo wanaokwamisha miradi.

Dk. Kamala anasema tatizo la maji ni kubwa kwani katika vijiji alivyotembelea malalamiko yalikuwa ni ukosefu wa maji hivyo hatua za kumaliza tatizo hilo zinatakiwa kuchukuliwa haraka.

Tetemeko

Pamoja na shida hiyo ya maji hawakuacha kuzungumzia athari waliyopata kutokana na tetemeko na kuweka wazi mapendekezo yao kwa Serikali.

Abdul Kazimshala anasema baada ya tetemeko walipokea mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule ambayo hata hivyo haitoshi.

Tunaomba mfuko wa jimbo usaidie katika ujenzi wa shule ili wananchi wasisumbuliwe na michango kwa sababu hawana uwezo wa kuchangia kutokana na madhila yaliyowakuta.

“Jamii haitakuwa na uwezo wa kujenga nyumba za walimu kwa sasa, wanatengeneza nyumba zao, kiasi cha uchangiaji kilichowekwa kwa ajili ya wananchi hakitakuwepo hivyo huo upungufu uchangiwe na Serikali.

“Misaada inayopelekwa kwa wananchi iangaliwe kwa umakini kwani hakuna mwananchi aliyekumbwa na tetemeko la tumbo kiasi cha kuwafanya watoa misaada wasambaze biskuti, watu wanaacha kulima wanakwenda kupokea msaada wanapewa pakiti moja ya biskuti,”anasema.

Naye Elias George anasema wanavyo vifaa lakini fedha za kujengea nyumba ikiwamo kuwalipa mafundi hawana hivyo wanaomba wawezeshwe kupata fedha.

Anasema hakuna nyumba ambayo haikuathirika kwa tetemeko, nyumba 550 Kilimilile ziliathiriwa na tetemeko ambapo nyumba nne zilianguka, 48 zilianguka upande na nyumba na 498 zilipata nyufa.

Dk. Kamala anasema tetemeko lilianzia Kijiji cha Minziro saa 9:27 na kwamba waliokufa katika Wilaya ya Misenyi ni watu wawili.

Anasema nyumba zote zilizoathiriwa na tetemeko zinaorodheshwa na hakuna kiongozi yoyote wa juu aliyeamuru mwenye nyumba zaidi ya moja zisiorodheshwe.

“Kama mtu ana nyumba tatu ziorodheshwe zote, tusiingize siasa katika masuala ya tetemeko, tathimini haiangalii nani mwenye uwezo na nani hana uwezo.

“Taarifa za kujua madhara yaliyotokea ni kiasi gani zilichukuliwa, wananchi wanashukuru misaada waliyopewa lakini walitarajia kupata misaada ya vifaa vya ujenzi,”anasema Dk. Kamala.

Dk. Kamala anasema kauli zinazotolewa na viongozi haziratibiwi na kwamba kila mmoja anatoa kauli yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles