23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo yanayoweza kumvutia mwanamume kwa mwenzi wake

Couple embracing

Na Christian Bwaya,

WANAWAKE wengi wanaotamani kuwa na uhusiano wa kudumu na wanaume, hupenda kujiuliza ni sifa zipi hutafutwa na wanaume kutoka kwao. Kwamba mambo yapi hasa yanayoweza kumvutia mwanamume pale anapoanzisha uhusiano na mwanamke?

Ingawa zipo tofauti ndogo ndogo miongoni mwa wanaume, kwa ujumla, uchambuzi wa tafiti mbalimbali za uhusiano unabainisha mambo kadhaa yanayowaunganisha wanaume wengi kimahitaji. Tuyatazame katika mfululizo wa makala hizi.

Kutambuliwa uwezo wake

Mwanamume anatamani kujisikia ni shujaa asiyeshindwa. Fahari ya mwanamume siku zote ni uwezo anaoamini anao unaomfanya mara nyingine awe tayari kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha maisha yake kwa lengo tu kuthibitisha kuwa wanaweza. Ndio kusema kutambuliwa uwezo wake ni hitaji la msingi.
Kama unatamani mwanamume umpendaye aanze (aendelee) kuvutiwa na wewe, chukua hatua ya kubaini vitu vya pekee alivyonavyo na onesha  kwa dhati kuwa unavitambua. Kwa kawaida kila mwanamume anayo maeneo yake anayoyaweza vizuri kuliko wengine.

Inawezekana ikawa ni uwezo fulani wa kipekee ambao si wanaume wengi wanao. Huenda ni tabia fulani maalumu ama ujuzi, maarifa na sifa nyingine za kipekee unazojua anazo. Inawezekana ni uaminifu wa muda, kujali familia yake, kuwahi nyumbani na kushiriki kazi za ndani, ufuatiliaji wa mambo kwa karibu, bidii ya kazi, ucha Mungu na mengineyo kama hayo. Chukua hatua ya kumfanya afahamu unauelewa uwezo alionao.

Katika mazingira yetu ya Kiafrika, wakati mwingine tunaogopa kuwatambua watu kwa sifa zao nzuri hata kama tunazitambua sifa hizo. Wakati mwingine tunafikiri kile chema anachokifanya mtu ni wajibu wake usiostahili kutambuliwa.

Hata haivyo, ni vyema mwanamke ujifunze kusema wazi kwa moyo wa dhati, kwa kurudia rudia, kuwa unatambua uwezo wa mume wako. Ukifanya hivyo utamfanya ajiamini zaidi, awe na moyo wa kuchangamka zaidi na atajaa nguvu za kufanya vizuri zaidi ili awe shujaa wako.

Anahitaji kuheshimiwa
Heshima ni hitaji kubwa kwa binadamu yeyote anayejitambua. Tunapenda watu watufikirie katika hadhi ya juu. Ndio maana mtu yeyote anayetufanya tujione hatuna hadhi tunazozitaka, ni rahisi kutofautiana naye. Hii ni hulka ya kawaida ya binadamu.

Kwa mwanamume hitaji la kuheshimiwa ni kubwa zaidi. Tunapozungumzia heshima kwa mwanamume, katika mazingira yetu, tunamaanisha hali ya kutamani kujiona ana hadhi ya juu, ana mamlaka zaidi pengine kuliko mwanamke. Kinyume chake ni kudharauliwa, kuwekwa katika mazingira ya kujiona hana hadhi, hana mamlaka, asiye na kauli wala uwezo wa kufanya lolote bila mwongozo wa mwanamke.

Kwa wanaume wengi, heshima ni namna unavyoongea naye, maneno unayoyatumia katika kueleza mawazo yako, ishara za mwili wako katika mazungumzo, kumpa nafasi ya kwanza katika maamuzi na mambo kama hayo.

Heshima, vile vile ni kumstahi mwanamume unayempenda hata anapokosea. Kosa linapotumika kama sababu ya kufanya vitendo vinavyodhalilisha hadhi yake ni kujipunguzia alama. Ndio kusema, staha ni kuongea naye kwa nidhamu hata katika mazingira ambayo ni dhahiri yeye ndiye mkosaji.

Kadhalika, heshima ni kuwa tayari kumtunzia hadhi yake kwa watu wengine. Kumjengea taswira inayomwongezea thamani yake kwa watu unaojua anawaheshimu. Kuonesha fahari yako kwake unapoongea na watu wengine kwa kauli, matendo na hisia kunaongeza alama za sifa anazozitafuta.

Itaaendelea…

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles