SAIDI IBADA Na BOSCO MWINUKA (TUDARCo) – Dar es Salaam
UCHACHE wa magari ya kusomba taka Dar es Salaam unachangia kukithiri kwa uchafu, hususani maeneo ya masoko.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Soko la Shekilango, Manispaa ya Ubungo, David Mrisho, alisema changamoto kubwa ya usafi wa soko hilo ni uchache wa magari ya kusombea taka na kwamba gari hupita mara moja kwa wiki.
“Gari la kusomba taka hufika hapa mara moja kwa wiki hali inayosababisha mlundikano wa takataka na kuleta adha kwa wafanyabiashara na wateja,” alisema Mrisho.
Alisema Manispaa ya Ubungo ina magari mawili ambayo yanatumika kuzoa taka sokoni, hospitalini na mitaani.
Meneja Usafirishaji wa Masoko, Manispaa ya Ubungo, Saidi Mfinanga, alisema manispaa hiyo imepokea malalamiko hayo na inayafanyia kazi.
Alisema manispaa imeanza mazungumzo na mkandarasi mwingine kutokana na mzabuni wa awali kumaliza mkataba wake mwezi huu.
“Tupo kwenye mazungumzo na mkandarasi mpya ili tupate gari kubwa la kusombea taka katika manispaa yetu kwa kuhakikisha masoko yanakuwa safi kila siku,” alisema Mfinanga.
Pia aliongeza kuwa hivi karibuni wataongeza gari jingine la kusomba taka katika manispaa hiyo ili kupunguza mrundikano wa takataka katika maeneo yote.
“Tuna mpango wa kuongeza gari jingine ambapo tutaenda mara mbili katika soko la Shekilango kuzoa taka tofauti na sasa ambapo gari linaenda mara moja kwa wiki,” alisema Mfinanga.