31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

TMA yatoa tahadhari magonjwa, mafuriko, uhaba wa chakula

ANDREW MSECHU –Dar Es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya uwezekano wa kuibuka magonjwa ya milipuko, uhaba wa maji na chakula, na kutokea mafuriko katika baadhi ya maeneo kutokana na mvua za vuli zitakazonyesha Oktoba hadi Desemba.

Akizungumza wakati wa kutoa mwelekeo wa mvua za vuli, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema athari hizo zitatokea katika maeneo yatakayokuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani na yale yatakayopata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Dk. Kijazi alisema maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani ni yanayozunguka ukanda wa Ziwa Victoria, ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu Shinyanga na Mara, huku Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, mvua zikitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

“Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua nyingi, matukio ya magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza, kadhalika katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa maji safi na salama,” alisema.

Dk. Kijazi alisema athari nyingine zinazotarajiwa ni upungufu wa malisho, hasa maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani, ambayo ni mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, hali inayoweza kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Alisema hata hivyo, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

“Kwa hiyo, kutokana hali hii, sekta za kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanyamapori, maliasili na utalii, nishati na maji, mamlaka za miji, afya na menejimenti za maafa zinatakiwa kuweka mazngira ya kukabiliana na mwelekeo wa mvua hizi,” alisema.

MWELEKEO WA MVUA

Dk. Kijazi alisema mvua za vuli zinazoanza Oktoba hadi Desemba ni mahususi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki, Pwani ya Kaskazini na Visiwa vya Unguja na Pemba, Ukanda wa Ziwa Victoria na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Alisema kwa sasa tayari katika baadhi ya maeneo ya Kagera mvua za nje ya msimu zinaendelea tangu Agosti na zinatarajiwa kusambaa maeneo mengine ya Ziwa Victoria.

“Mvua hizo zinatarajiwa kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya tatu na ya nne ya Oktoba.

“Kiwango cha mvua kinachotarajiwa ni mvua za wastani hadi za juu ya wastani katika maeneo haya, msimu katika maeneo haya unatarajiwa kumalizika kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya Januari 2020,” alisema.

Dk. Kijazi alisema katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini, yaani mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu.

Alisema ukanda huo unatarajiwa kuwa na vipindi virefu vya ukavu na mvua chache, japokuwa mvua za kiwango cha wastani zinatarajiwa kuanza kunyesha kuanzia wiki ya pili ya Novemba na zitamalizika katika wiki ya nne ya Desemba.

USHAURI

Dk. Kijazi alisema kutokana na mwelekeo wa mvua hizo, kwa usalama wa chakula, mifugo na wanyamapori, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, wafugaji wanashauriwa kuvuna mifugo yao ikiwa bado katika hali nzuri kwa kuzingatia ushauri wa maofisa ugani.

“Sekta ya uvuvi katika maeneo hayo pia inaweza kuathiriwa, kutokana na uhaba wa maji katika mabwawa ya samaki, hivyo wafugaji wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya ufugaji kwa kuzingatia matumizi sahihi ya maji,” alisema.

Alisema upatikanaji wa maji unatarajiwa kuimarika katika maeneo yatakayokuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani, hivyo athari zinaweza kujitokeza katika miundombinu ya rasilimali za maji.

Dk. Kijazi alisema kutokana na hali hiyo, pia shughuli za uchimbaji madini migodi midogo zizingatie tahadhari zinazotolewa na wataalamu.

mwisho

Majaliwa aomba Japan kuendeleza madaktari bingwa nchini

Na Mwandishi wetu – Narita, japan

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa madaktari bingwa wa upasuaji na  wa magonjwa ya figo na moyo kutoka Tanzania ili kukidhi mahitaji ya madaktari hao nchini.

Majaliwa aliwasilisha ombi hilo juzi jioni wakati alipozungumza na mshauri maalumu wa masuala ya afya wa taasisi ya Tokushukai General Incorporated Association iliyo chini ya Serikali ya Japan, Akio Egawa, kwenye Uwanja wa Ndege wa Narita nchini Japan akiwa njiani kurejea nyumbani.

Alisema hivi sasa Tanzania ni kimbilio kwa nchi jirani katika tiba ya moyo na figo, hivyo madaktari bingwa wa upasuaji na wa magonjwa hayo wanahitajika sana.

Majaliwa alisema baada ya Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kufanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa saba chini ya ufadhili wa taasisi hiyo, nchi jirani pia zinategemea kupata huduma hiyo nchini, hivyo madaktari na vifaa tiba zaidi vinahitajika ili kujenga uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa ndani na nje.

Aliishukuru Serikali ya Japan kupitia taasisi hiyo kwa misaada ambayo kwa kiwango kikubwa imefanikisha kuanzishwa tiba ya upandikizaji figo Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Nashauri uandaliwe utaratibu wa kubadilishana wataalamu ili Watanzania waende Japan kutibu wagonjwa na Wajapani waje nchini kufanya kazi kwenye hospitali zetu, lengo likiwa ni kubadilishana ujuzi na kuongeza uzoef,” alisema.

Pia alimkaribisha Egawa Tanzania ili aweze kuona maeneo mengine ambayo taasisi anayoiongoza inaweza kusaidia ili kuifanya nchi yetu kuwa na uwezo katika tiba ya upandikizaji figo barani Afrika.

 Alisema amefurahi kufahamu Egawa ameishi Tanzania kwa miaka mitatu akifanya kazi ubalozi wa Japan uliopo Dar es Salaam, hivyo anaifahamu vizuri na anajua umuhimu na mahitaji ya huduma za afya nchini na anafahamu mikakati ya Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake, Egawa alimuahidi Majaliwa kuwa taasisi yake iko tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kwa kuendelea kusaidia Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuiimarisha na kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika huduma ya tiba ya figo na moyo. Alisema taasisi yake iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles