Na Upendo Mosha, Moshi
HOSPITALI za mikoa ya Kanda ya Kaskazini, zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa damu salama kutokana na mwamko mdogo wa wananchi kujitolea kutoa damu ili kusaidia wagonjwa wenye mahitaji.
Hayo yamesemwa na Ofisa mipango wa damu salama Kanda ya Kaskazini, Faisal Abubakari, wakati wa utoaji wa damu salama kwa vijana zaidi ya 110 wa Kanisa la Adventista Wasabato waliojitokeza kujitolea kutoa damu ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji.
Alisema kumekuwapo na upungufu wa damu katika hospitali mbalimbali za Kanda ya Kaskazini kutokana na jamii kutokuwa na uthubutu wa kuchangia damu, jambo linalosababisha baadhi ya wagonjwa hususani wanawake wanaojifungua kufariki dunia kutokana na kukosa damu.
“Kwa sasa hospitali zetu za Kanda ya Kaskazini hazina damu kwani mwamko umekuwa ni mdogo wa jamii katika kujitokeza kuchangia damu, jambo hili limekuwa ni chanzo kikubwa cha wagonjwa wengi hususani wanawake wanaojifungua kupoteza maisha kutokana na kukosa huduma ya damu salama,” alisema.
Awali walijiwekea lengo la kukusanya damu kiasi cha lita 30,000 kwa mwaka 2016, lakini wameshindwa kufikia lengo hilo baada ya jamii kutokuwa na mwamko wa kuchangia.
Kwa upande wake, kiongozi wa vijana hao, Heriel Tumaini, alisema vijana wamehamasika kutokana na uhitaji mkubwa wa damu kwa wagonjwa hususani akinamama wanaojifungua na majeruhi wa ajali ambao wanakosa huduma hiyo ili kuokoa maisha yao.
“Tumeona tujitokeze sisi kama vijana kwa umoja wetu kuja kufanya matendo ya huru kwa kuwachangia wagonjwa damu, kwani naamini kuna wagonjwa wengi wanahitaji huduma hii lakini wameikosa na kusababisha vifo ambavyo si vya lazima,” alisema.
Baadhi ya vijana waliojitokeza kuchangia damu, walisema ni vema kila mtu mwenye afya njema akajitokeza kujitolea damu ili kuokoa maisha ya watu wenye matatizo ya uhitaji wa damu.
“Vijana ni vema tukajitokeza kuchangia damu kwani suala hili litasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu wengi iwapo tutakuwa na desturi ya kuchangia damu mara kwa mara, tatizo la upungufu wa damu litakuwa ni historia katika hospitali zetu,” alisema Joel Joakim