UCHAGUZI wa Rais uliofanyika hivi karibuni nchini Gabon na matokeo yake yaliyotangazwa kuzua hamkani na vurumai mitaani, unawahusu wanasiasa waliolelewa na Hayati Rais Omar Bongo ingawa kila mmoja ana nafasi yake ya nasaba na rais huyo aliyetawala kwa miaka 41.
Ali Bongo ni mtoto wa Hayati Rais Omar Bongo, aliyerithi madaraka mnamo mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake, lakini kama ilivyotokea katika uchaguzi wa hivi karibuni, matokeo yalifuatiwa na vurugu kubwa wakati Jean Ping ni mwanadiplomasia mbobevu aliyewahi kutumikia nafasi ya juu ya uongozi katika umoja wa Afrika (AU), aliyekuwa na ukaribu na Hayati Rais Bongo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na amezaa watoto wawili na binti wa rais huyo wa zamani anayeitwa Pascaline.
Baada ya Ali Bongo kutangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake, Jean Ping, asiyekubaliana na matokeo hayo aliyekimbilia mafichoni kutokana na kusakwa na vyombo vya dola, wafuasi wake waliingia mitaani na kutoshana nguvu na askari katika vurumai zilizohusisha uchomwaji moto wa jengo la Bunge la nchi hiyo, pia helikopta za kijeshi kuyamiminia rasharasha za risasi makao makuu ya chama cha upinzani cha National Union Party kinachoongozwa na Ping na kusababisha vifo vya watu wawili.
Mkanganyiko uliosababisha vurumai zilizotokea unahusiana na matokeo ya ushindi mwembamba wa Rais Bongo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi (Cenap), yaliyompa ushindi wa asilimia 49.8 dhidi ya 48.2 za mpinzani wake na kumhalalisha kutawala kwa muhula mwingine wa miaka saba, kipindi ambacho awamu moja ya Serikali hukaa madarakani katika nchi hiyo.
Hoja za kimsingi za mpinzani wa Bongo ni kuchezewa kwa uchaguzi ikiwemo matokeo ya jimbo analotoka Rais Bongo la Haut-Ogooue ambapo wapiga kura waliojitokeza ni asilimia 99, huku waliompa kura Bongo ni 95. Lakini wakati huo Serikali ikidai kuwa wafuasi wa Ping ni genge la wahalifu walioamua kuanzisha vurugu na kuchoma Bunge, baada ya kiongozi wao Ping kushindwa kwenye uchaguzi ndiyo maana majeshi yalivurumisha risasi kwenye makao makuu ya chama cha upinzani ili kuwadhibiti wahalifu hao.
Mkanganyiko mwingine unaihusu tume ya uchaguzi (Cenap) ambayo imechelewesha kutangaza matokeo yaliyopaswa kutangazwa siku tano kabla ya Jumatano, hatimaye ikahakiki upya matokeo na kumtangaza Bongo (57) kuwa mshindi dhidi ya Ping (73).
Katika hali ya marudio ya kitakachojiri baada ya vurugu za kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, tayari Ufaransa imepaza sauti dhidi ya yanayotokea katika koloni lake hilo la zamani wakitaka matokeo yawekwe hadharani ili kumaliza utata na ubishi, huku Marekani ikisihi kuwepo kwa uvumilivu baina ya pande mbili.
Hapo ndipo mkanganyiko mwingine unapoibuka kwa kuwa inazua maswali mengi kwamba kwanini chaguzi barani Afrika haziwezi kumalizika bila misigano, inayofuatiwa na uingiliaji kati wa mataifa makubwa ili kutuliza hamkani? Swali lingine la kimsingi linalomhusu Rais Ali Bongo ni kuhusu ushindi wake mwembamba, si tu katika uchaguzi huu, lakini pia uliopita mnamo miaka saba nyuma uliozusha vurugu kubwa kuliko hata zinazoonekana sasa.
Hata mfumo wenyewe wa kupata mshindi katika uchaguzi kwenye nchi hiyo unachanganya, kwani bado wanatumia mtindo wa mshindi ni mwenye kura nyingi bila kujali kama zimezidi nusu asilimia 50 ya idadi ya wapiga kura au la!
Ali Bongo alipoingia madarakani alijitahidi kubadilisha mfumo na kuharamisha muundo ambao uliwezesha ufisadi kushamiri kwa kugawanya nguzo za nguvu ya kiuchumi, lakini matatizo ya uchumi aliyoyarithi kutokana na kuanguka kwa bei ya mafuta ghafi inayoyategemea kwa pato la kigeni, yamesababisha ajenda za upinzani kushika nguvu miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo.
Gabon itaendelea kukumbwa na machafuko ya uchaguzi kila baada ya matokeo kama haitabadilisha namna inavyosimamia uchaguzi kwa kuficha takwimu za kura zilizopigwa, pia sheria isiyotekelezeka inayobainisha kuwa kupiga kura ni lazima si hiyari na ukadiriaji wa ushindi bila kujali kiwango cha asilimia kinachotakiwa.
Historia inaihukumu nchi hiyo kwani licha ya Hayati Rais Omar Bongo kufanya mengi katika kipindi alichojisimika madarakani na kuongoza kwa miongo minne na ushei, lakini nchi hiyo inaendesha siasa za kinasaba na kifamilia hususan kwa yanayotokea sasa nchini humo ambapo vurumai na hamkani zote kutokana na uchaguzi zinatokana na mtoto na mkwe wa Rais wa zamani.
Hiyo maana yake ni kuwa masilahi binafsi ya wanasiasa hao na wapambe wao yanatangulizwa mbele kuliko utaifa wa nchi ya Gabon, hilo likiwa ni tatizo sugu kwenye nchi nyingi za Afrika hususan zilizobarikiwa mali ghafi muhimu ya mafuta yanayotegemewa zaidi kuimarisha uchumi wa mataifa hayo.