23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Clinton, Trump ‘watimua mbio’ ya mwisho kuelekea Ikulu

Clinton, TrumpKWA Wamarekani wengi, Siku ya Wafanyakazi inamaanisha mwanzo wa ufunguzi wa muhula wa shule, ikisherehekewa Jumatatu ya kwanza ya mwezi Septemba.

Kadhalika inamaanisha kumalizika kwa kipindi cha utamaduni wa uvaaji wa mavazi meupe nchini humo.

Tofauti na mataifa mengine duniani ikiwamo Tanzania yanayoitumia Mei Mosi, Marekani na Canada huadhimisha Siku ya Wafanyakazi katika Jumatatu ya kwanza ya Septemba.

Ni kuenzi vuguvugu za wafanyakazi na michango yao iliyopelekea kuifanya  Marekani kuwa taifa kubwa na lenye nguvu kiuchumi na kijeshi duniani.

Inajulikana pia kama Jumatatu ya wikiendi ndefu, hali kadhalika kama wikiendi ya Siku ya Wafanyakazi.

Kama hiyo haitoshi inahesabiwa ijapokuwa si rasmi kama mwisho wa majira ya kiangazi na mwanzo wa majira ya majani kupukutika bila kusahau kupulizwa kwa kipenga cha kuanza ligi mbalimbali za michezo nchini humo na kwingineko.

Lakini unapokuja mwaka wa uchaguzi wa urais, inamaanisha mchuano wa mwisho kuelekea Siku ya Uchaguzi umeanza na dirisha kwa wagombea urais; Hillary Clinton na Donald Trump kuvuta wapiga kura linafungwa kwa kasi.

Kambi zote mbili zinakabiliwa na kalenda yenye matukio muhimu kwa kampeni zao kipindi hiki cha mapukutiko, ambazo zina nafasi kubwa kutengeneza matokeo ya mwisho ya kampeni.

Katika kipindi hiki cha mapukutiko tukio la kwanza ni lile litakalowakutanisha wagombea hao leo lijulikanalo kama Jukwaa la Amri Jeshi Mkuu.

Na Septemba 23, ni siku ambayo barua pepe zaidi za Clinton zinatarajia kuanikwa wakati huo huo, majimbo ya kwanza yatashuhudiwa yakipiga kura za mapema.

Septemba 26 nayo ni maalumu kwa mdahalo wa kwanza kati ya mitatu ya urais, utakaofuatiwa na ule wa wagombea wenza hapo Oktoba Nne.

Mdahalo wa pili wa urais utafanyika Oktoba tisa na wa mwisho Oktoba 19.

Trump amekuwa akiburuza nyuma ya Clinton kitaifa na katika majimbo muhimu tangu kumalizika kwa mikutano mikuu ya vyama, ambayo iliwapitisha rasmi kufuatia ushindi wao wakati wa kura za mchujo.

Lakini pia kwa kadiri muda ulivyoenda uongozi wa Clinton dhidi ya Trump umekuwa ukipungua na kuelekea kukabana koo.

Kwa sababu hiyo muda uliobaki ni muhimu mno kwa kila mmoja kujipanga vyema kuanzia wiki hii.

Naam, kuanzia leo, wakati wapiga kura watakapopata fursa ya kuwalinganisha na kuwapima Clinton na  Trump katika tukio tuliloona likijulikama kama Jukwaa la Amiri Jeshi Mkuu.

Jukwaa hilo lililoandaliwa na askari maveterani wa Marekani waliopigana vita Irak na Afghanistan, litarushwa moja kwa moja na vituo vya NBC na MSNBC.

Likiwa tukio la kwanza maalumu kwa Uchaguzi Mkuu na wagombea hao watakabiliwa na maswali kutoka kwa watazamaji wanaojumuisha maveterani na askari wa sasa masuala kuhusu usalama wa taifa, jeshi na masuala ya maveterani hao.

Na kwa mdahalo wa kwanza kati ya mitatu ya urais utakaofanyika Septemba 26 katika Chuo Kikuu cha Hofstra mjini New York ni muhimu pia.

Miaka minne iliyopita, Mitt Romney alionesha umahiri katika mdahalo wa kwanza dhidi ya Rais Barack Obama ambao ulimsaidia kwa muda ukipunguza pengo la uongozi alilokuwa nalo Obama.

Lakini ni wazi kufanya vyema katika mdahalo mmoja kwa gavana huyo wa zamani wa Massachusetts hakukutosha.

Jukwaa la Amiri Jeshi Mkuu ni pekee ambalo wagombea hao wataonekana pamoja kabla ya kuanza kwa upigaji kura wa mapema katika majimbo 37 na wilaya ya Columbia.

Maeneo hayo yana utamaduni wa upigaji kura mapema, chini au zaidi ya wiki tatu  kabla ya uchaguzi mkuu.

Miongoni mwa sababu za kuwapo utaratibu wa kupiga kura mapema ni kutoa fursa kwa watu wanaojaribu kuepuka misururu mirefu siku ya uchaguzi au wale ambao siku ya uchaguzi hawatakuwepo au watakuwa na majukumu.

Upigaji kura wa mapema una mchango wake katika kuamua chaguzi za urais— karibu asilimia 32 ya wapiga kura walipiga kura mapema mwaka 2012, kwa mujibu wa ofisi ya Sensa Marekani.

Kwa mujibu wa kitengo hicho asilimia 32 ya wapiga kura walipiga kura mapema mwaka huo, likiwa ongezeko dogo ya ilivyokuwa mwaka 2008, ambapo chini ya asilimia 30 walipiga kura ya mapema.

Rais Obama alikuwa miongoni mwa waliopiga kura mapema, ikiwa ni wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu na alitoa wito kwa wengine wanaoweza kufanya hivyo kabla ya siku ya uchaguzi kuiga mfano wake.

Hatua hiyo ilimfanya Obama kuweka historia nyingine ya kuwa rais wa kwanza nchini Marekani kupiga kura ya mapema.

Obama alipiga kura yake wakati wa ziara fupi katika mji wake wa Chicago wakati akiwa katika kampeni ya majimbo manane.

Akiwa amejipanga kwa mchakato huo, takwimu zilionesha ni yeye aliyenufaika na kura za mapema. Kwa mujibu wa msemaji wa kampeni yake Jen Psaki kura hii ya mapema ilionesha Obama alifanya vizuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2008 na kwamba alikuwa akimshinda Romney.

Ikifahamu hilo, kampeni ya Clinton nayo imetilia mkazo kushawishi wapiga kura wanaopiga kura mapema wafanye hivyo kabla ya siku ya uchaguzi.

Faida ya kufanya hivyo ni kwamba timu za kampeni zitakuwa zinajua ni nani ameshiriki kura za mapema na nani bado.

Kwa sababu hiyo, inairahisishia kambi kuwaondoa katika orodha ya waliokwishapiga na kubakiza wale ambao hawajapiga bado kwa kuwekeza nguvu kwao ili wamkumbuke siku ya uchaguzi.

Namna Trump alivyojipanga kuchukua fursa ya upigaji wa kura za mapema haijajulikana huku washauri wake wakisema watakuwa tayari muda ukifika.

Aidha maswali yamezingira kampeni ya Trump namna anavyojipanga katika suala la matangazo ya televisheni, ijapokuwa amejitutumua kununua, lakini bado ameachwa mbali na Clinton kwa uwiano wa 10 kwa moja.

Ndiyo maana Jarida la Wall Street Journal, limeihesabu Jumatatu ya kwanza ya Septemba kama ya mwisho kwa bilionea huyo wa mali zisizohamishika.

“Iwapo hawataweza kumfanya Trump abadilike ifikapo Siku ya Wafanyakazi, Republican haitakuwa na njia nyingine zaidi ya kuachana na mtu asiye na matumaini kwa kujikita katika chaguzi za seneti na ubunge,” liliandika katika tahariri yake Agosti 14 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles