KAMPALA, UGANDA
SERIKALI ya Uganda imetoa hadi Septemba 30, 2017 kwa watengenezaji wa vileo kusitisha uuzaji wa pombe katika pakiti maarufu kama viroba.
Wizara ya Biashara imesema Serikali itawafungulia mashtaka wauzaji watakaokiuka amri hiyo, ikiwataka wahifadhi pombe katika chupa.
Waziri wa Biashara, Amelia Kyambadde, alisema hiyo ni moja ya mipango iliyokubaliwa baina ya Serikali, wadau na muungano wa biashara ya pombe.
Uuzaji wa viroba umetajwa kuwa chanzo cha ulevi holela na ukosefu wa uwajibikaji kutokana na watu kutumia vibaya pombe hizo.
Wanafunzi na vijana wametajwa kuwa waathirika wakubwa zaidi kutokana na kuzinywa kiholela kwa sababu ya urahisi wake wa bei, upatikanaji na ubebaji huku zikichangia pia uharibifu wa mazingira.
Kwa mujibu wa maofisa, paketi zenye ujazo mdogo zaidi wa milimita 100 huuzwa kwa Sh 500 za Uganda (sawa na Sh 250 za Tanzania).
Kwa sasa asilimia 75 ya pombe huuzwa katika paketi, huku asilimia 25 iliyobaki zikiuzwa katika chupa.
Mkutano huo wa wadau wa sekta ya vileo uliofanyika jana, uliitishwa na Kyambadde katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya ongezeko la ulevi na uharibifu wa tabia miongoni mwa vijana.
Kwa mujibu wa maofisa, pombe za viroba zimesababisha athari mbaya kwa mtu mmoja mmoja na jamii, kutokana na kushindikana kudhibiti matumizi yake.
Kyambadde alisema ijapokuwa Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya pombe katika kutengeneza ajira na kuchangia pato la taifa kupitia kodi, uhifadhi wake unahitaji kubadilika kutoka pakiti ndogo hadi chupa.
Watengeneza pombe walikiri hatari inayosababishwa na pombe za viroba, lakini waliomba muda zaidi hadi mwaka 2018 ili kujiandaa kuhama kutoka upakiaji katika pakiti hadi chupa.
Lakini Serikali ilisema inataka kushughulikia tatizo hilo haraka iwezekanavyo na hivyo miezi tisa kuanzia sasa inatosha kwa wafanyabiashara kujipanga.