22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ugaidi’ Tanga bado wingu zito

paul-chagonja1Amina Omari, TANGA na Fredy Azzah, Dar

ZIKIWA zimepita siku sita tangu tukio la polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kurushiana risasi kwa takribani saa 48 na watu wanaodaiwa kuwa ni kikundi cha uporaji silaha, wingu zito limeendelea kutanda juu ya suala hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, kutoa kauli katika moja ya mikutano na waandishi wa habari na kudai tukio hilo limehusisha vijana aliowaita wahuni, huku akikiri kwamba hawajafanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa hata mmoja.
Chagonja, alisema hadi wakati huo mtu aliyekuwa akishikiliwa ni mmoja ambaye alikamatwa na vijana wanaojishughulisha na upasuaji kokoto karibu na mapango hayo yaliyopo Kijiji cha Mleni jijini Tanga.
Mbali na hilo, alisema wamekamata silaha moja kati ya mbili zilizokuwa zimeporwa kwa jeshi hilo na kuwa ndani ya mapango hayo walimokuwamo watu hao, jeshi hilo limekuta ngedere watatu ambao walikuwa wamekufa huku wakiwa na majeraha ya risasi.
Kauli hiyo ya Changonja iliongeza utata na wingu juu ya suala hilo ambalo kutokana na taarifa zilizokuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wananchi waliaminishwa ni magaidi ama kikundi ambacho kilikuwa kimejitosheleza kwa silaha.
Moja ya maswali ambayo yalikuwa yakihojiwa na wananchi ni kuwa kama kilikuwa ni kikundi cha wahuni, kwanini Jeshi la Polisi na JWTZ wameshindwa kukidhibiti kwa muda wote waliorushiana risasi na kuzunguka eneo hilo?
Kama walikuta ngedere waliojeruhiwa, muda wote askari hao walikuwa wanarushiana na nani risasi? Ama taarifa kwamba askari hao walikuwa wakirushiana risasi wenyewe kwa wenyewe baada ya kuingia kwenye mapango hayo kwa njia tofauti na baada kukutana na kila mmoja akaona mwenzake ni adui ni za kweli?
Kwa kiasi kikubwa utoaji wa taarifa wakati wa kuendesha operesheni hii ulikuwa wa juu juu, hali iliyofanya hata waandishi kushindwa kuona askari waliojeruhiwa kwenye mapambano haya na kupata taarifa zao za undani.
Hata hivyo, taarifa za askari wa JWTZ aliyeuawa zilifichwa na hakuna aliyekuwa wazi kuzitolea ufafanuzi. Hali hii ilisababishwa na nini?
Kutokana na hali hiyo inawezekana kuna sababu za msingi za kuficha taarifa hizo, lakini pia majibu yanayotolewa na polisi ni mepesi kulingana na uzito wa tukio hilo.

MAJIBU YA POLISI
Jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Freisser Kashai, aliliambia MTANZANIA kuwa majeruhi watano wa tukio hilo wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya madaktari kuridhishwa na hali zao.
Alisema pia hali ya usalama katika eneo la tukio inaridhisha na vikosi vya polisi vinaendelea na doria za kawaida za kuimarisha amani.
“Kwa sasa hali ni ya amani tunaendelea na upelelezi wetu wa kuwahoji watuhumiwa tuliowakamata, huku vikosi vya jeshi vikiendelea kufanya doria ili kuweza kuwabaini watuhumiwa wengine,” alisema Kamanda Kashai.
Alisema kinachoendelea kwa sasa ni upelelezi na misako ili kuweza kuwakamata watuhumiwa wengine na kuendelea kuitafuta silaha moja ambayo bado haijapatikana.
Kamanda aliongeza kuwa kwa sasa vikundi vya jeshi ambavyo vilikuwa vinashirikiana kwenye operesheni vimepungua kwenye eneo la mapango ya Mleni.
Lakini pamoja na kauli hiyo ya Kamanda Kashai, taarifa kutoka katika eneo la tukio zinaeleza hadi kufikia juzi, Jeshi la Polisi pamoja na JWTZ waliongeza idadi ya askari wao.
Hatua hiyo imezidi kuongeza hofu kwa wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo, huku wale waliokimbia makazi yao tangu siku ya tukio wakiwa bado hawajarejea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles