27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ufisadi wagubika zabuni uagizaji mafuta

Charles_MwijageNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HOFU imetanda kwa watumiaji magari na mitambo nchini kutokana na taarifa kwamba bei ya dizeli na petroli inaweza kupanda kutokana na kuzuka utata katika zabuni  Namba PIC/2015/G-P/37 iliyopewa Kampuni ya Nishati ya Augusta bila kufuata utaratibu wa zabuni rasmi.

Zabuni hiyo ambayo ni ya kuagiza mafuta nje ya nchi ndiyo inatajwa kuwa ghali zaidi tangu Kampuni ya Uratibu wa Uagizaji wa Mafuta (PICL) ianzishwe miaka kadha iliyopita.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana hatua hiyo ya kutolewa   zabuni hiyo kinyume cha utaratibu  ni mpango unaoratibiwa na vigogo wa Serikali kwa ajili ya kutafuta fedha za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Taarifa kutoka ndani ya Wizara ya Nishati na Madini zinaeleza kuwa licha ya wafanyabiashara wa mafuta kupinga   zabuni hiyo kutofuata utaratibu,   bado kuna baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wamekuwa wakikinga kifua katika kutoa uamuzi.

Mtoa habari wetu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema utata mkubwa umezuka katika utoaji wa tenda hiyo kwa vile mfumo wa PICL kuhusu utaratibu wa uagizaji  mafuta kwa pamoja (BPS) ambao umekuwa ukifanya kazi kwa ufanisi zaidi ya miaka miwili sasa, umekiukwa.

Katika nyaraka zinazohusiana na tenda hiyo, gharama ya zabuni hiyo ni Dola za Marekani 20 kwa kila tani mita moja ambayo inatajwa kuwa ni gharama ya juu zaidi kuliko zabuni Na. PIC/2015/G-P/36 , Julai mwaka huu.

Kwa mujibu wa zabuni hiyo ambayo inamalizika Septemba mwaka huu, mita tani 438, 961 ziliagizwa na kampuni za biashara ya mafuta  ambazo hazikujua kuwapo  zabuni hiyo ghali namba 37 kabla ya kuwasilisha oda husika.

Mtoa habari huyo aliiambia MTANZANIA kuwa kwa gharama ya Dola 20 kwa kila mita tani moja ambayo ni  zaidi ya zabuni za awali, umma utalazimika kulipa zaidi  ya Dola 8,779,220 (zaidi ya Sh bilioni 20) kwa mafuta hayo yaliyoagizwa na Kampuni ya Augusta Energy, gharama ambazo hazingekuwapo iwapo mchakato halali ungefuatwa.

Hali hiyo inaonyesha ongezeko kubwa la gharama katika  zabuni 37 iliyotolewa  kwa Kampuni ya Augusta.

“Ukiangalia zabuni namba 34 gharama za uagizaji zilikuwa Dola za Marekani milioni 34.156; zabuni 35 (Dola milioni 48,877); zabuni 36 (dola milioni 44.315), lakini zabuni hii namba 37 yenye utata gharama za uagizaji ni Dola milioni 64,911,”kilisema chanzo chetu.

MTANZANIA ilipomtafuta mmoja wa watendaji wanaohusika na suala la usimamizi wa sekta ya mafuta na mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema  suala hilo bado ni kizungumkuti  ingawa alikiri kwamba PIC imekiuka utaratibu.

“Utata wa suala hili ulianza na suala la Premium ambayo ni gharama ya uagizaji, usafirishaji na faida ya aliyeagiza, na ongezeko hili la karibuni Sh bilioni 20 linatokana na kukosekana usimamizi mzuri na kukiukwa   sheria.

“Tunajua mamlaka zinazohusika ziliiandikia  PICL (kampuni inayosimamia uagizaji wa mafuta kwa pamoja), lakini imekuwa kimya. Hatari ya suala hili mzigo huu utabebwa na mwananchi wa kawaida.

“… kuna hatari kubwa   katika kipindi cha Septemba na Novemba mwaka huu bei ya mafuta kwa wakazi wa Dar es Salaam itapanda hadi Sh 2,500 hadi Sh 2,700 kwa lita,” alisema.

Mtendaji huyo alisema kama zabuni hiyo ingeshindanishwa gharama  ya uagizaji ingekuwa katika bei ya kawaida na yenye manufaa kwa mlaji wa mwisho.

“Kama kungekuwa na ushindani gharama za uagizaji wa mafuta zisingezidi Dola milioni 15 lakini kwa zabuni hii imepanda hadi kufikia Dola milioni 18 jambo ambalo si sahihi,” alisema.

Alipotafutwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kutoa ufafanuzi wa suala hilo, muda wote simu yake iliita bila majibu.

MTANZANIA pia ilimtafuta Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, ambaye alisema   yuko jimboni mkoani Kagera.

“Unasema kuna malalamiko, sawa kesho (leo) nitarejea Dar es Salaam na kwenda ofisini   niangalie hilo suala na malalamiko halafu nitarejea kwako kukupa undani wa suala hilo,” alisema Mwijage.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uratibu wa Uagizaji Mafuta ya Petroli (PIC), Michael Mjinja, alipopigiwa simu yake iliita bila majibu.

Julai mwaka huu,   Mjinja aliziandikia barua kampuni za uagizaji mafuta nchini  akisema mpango huo utaingia kwenye kipindi cha mpito   kuanzia Agosti hadi Novemba mwaka huu.

“Kutokana na hilo, nahitaji kupata mahitaji yenu ya  shehena ya mzigo mnayohitaji  kwa kipindi cha Oktoba na Novemba,” Ilisema sehemu ya barua hiyo huku ikitaka mahitaji hayo yawasilishwe ofisini kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles