27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa, Magufuli kimya kimya

Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu, Dar es Salaam

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza  kampeni za wagombea urais, wabunge na madiwani nchini, leo wagombea hao wanatarajiwa kurudisha fomu zao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wagombea wawili wa urais ambao wamekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro hicho, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa anayewakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)  kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), watarudisha fomu za kuwania nafasi hiyo huku Jeshi la Polisi likiwa limepiga marufuku mbwembwe na maandamano kwa wafuasi wa vyama vya siasa.

Kutokana na zuio hilo, wagombea hao ambao wamekuwa gumzo katika duru za siasa nchini watarudisha fomu kimya kimya  huku wakisubiri uzinduzi rasmi wa kampeni, kwa mujibu wa ratiba za vyama vyao.

Urejeshaji huo wa fomu unakamilisha siku kadhaa ambazo  wagombea hao walitafuta wadhamini mikoani  kama ilivyo katika mahitaji ya Sheria ya Uchaguzi.

Wakati kampeni zikitarajiwa kufunguliwa kesho baada ya kukamilika kwa uteuzi wa NEC, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwavuli wa Ukawa kikiwa bado hakijataja tarehe ya uzinduzi kwa mgombe urais wake, hali ni tofauti kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Jumapili Agosti 23 mwaka huu kitazindua kampeni zake katika Uwanja wa Jangwani.

Kuanza kwa kampeni hizo  ni mwanzo wa siku 70 za kampeni kwa wagombea wa vyama 13 waliochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.

Baada ya kumaliza hatua ya kutafuta wadhamini, wagombea hao walitakiwa kusaini hati ya kiapo   mahakamani kwa jaji   waweze kukidhi vigezo vya kuwania nafasi hiyo.

Ratiba ya NEC leo

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),   mgombea urais wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa   atarudusha fomu saa 3.00 asubuhi, akifuatiwa na mgombea wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Edward Lowassa saa 4:00 asubuhi huku Dk. John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akitarajiwa kuwasilisha fomu zake saa 5:00 asubuhi.

Ratiba hiyo pia inaeleza kuwa  Chama cha Wakulima (AFP) saa 5:00,  Maximilian Lyimo (TLP) saa 6:30,  Chifu Lutalosa Yemba (ADC) saa 7:00,  ACT- Wazalendo 7:30, NRA saa 8:00, CHAUMMA saa 8:30, Godgrey Malisa (CCK) saa 9:00,  DP saa 9:00 na  TADEA saa 9:30.

Ukawa wanena

Wakati huohuo, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia,   jana alisema kuwa  kasoro ndogondogo zilizopo katika majimbo zitarekebishwa kabla ya kuanza  kampeni.

Alisisitiza kuwa viongozi wa umoja huo watamnadi mgombea wa chama kilichopo katika makubaliano ndani ya eneo husika.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa   NCCR-Mageuzi alisema umoja huo si wa viongozi bali upo kwa ajili ya masilahi ya wananchi hivyo hakuna kiongozi wala mtu ambaye ana mamlaka  ya kupanga mambo kinyume na taratibu zilizowekwa katika makubaliano ya awali ambayo waliyasaini.

“Tunakutana leo (jana) kujadiliana jinsi ya kutatua changamoto hizi zinazojitokeza hata kama nani ametoa maelekezo sisi tunaamini  hakuna aliye juu ya mwenzie. Viongozi wa wilaya  wote tunaomba watekeleze tuliyokubaliana,”alisema Mbatia.

Mbatia aliwataka wanasiasa kufanya kampeni za ustaarabu kwa kujikita  katika hoja za msingi na si kujadili mtu.

“Katika kipindi cha  kampeni nawaomba  wanasiasa wachunge ndimi zao wajadili hoja za elimu, maji na mambo mengine ya msingi …katika majukwaa tunapaswa kubishana kwa hoja na siyo kujadili watu, matusi wala kupigana,”alisema Mbatia.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa kama mwangalizi mkuu wa masuala ya uchaguzi inapaswa kutenda haki  kwa kila chama.

Mbatia pia alizitaka kamati za ulinzi na  usalama  zinazoongozwa na wakuu wa wilaya na mikoa kutojihusisha na masuala ya uchaguzi kwa kuwa teyari ni makada wa vyama.

Kuhusu kuzuiwa Ukawa kutumia Uwanja wa Taifa katika uzinduzi wa kampeini zao, Mbatia alisema uamuzi huo umeonyesha udhaifu wa Serikali katika uamuzi  na kuwapo kwa tatizo kubwa la kutokuwa na maeneo yenye nafasi ya kukusanyika wananchi.

Majimbo  ya Ukawa

Chama hicho pia kimetangaza  majimbo 19 ambayo kitasimamisha wagombea kupitia Ukawa huku kikikanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya jamii kuwa kimejitoa katika umoja huo.

Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Ndelakindo Kessy alisema majimbo hayo yameongezeka kutoka 14 ya awali hadi 19.

Alisema  majimbo ambayo kitasimamisha wagombea ni    Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Buyungu, Manyoni, Vunjo.

Mengine ni Mwanga, Mufindi Kusini, Mtwara Mjini, Ileje, Gairo, Kibakwe, Mtera, Mpwapwa, Serengeti, Ngara na Nkenge.

Kova na CCM kuzomewa

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  Suleiman Kova amepiga marufuku watu wanaozomea wanachama wa CCM waliovalia sare zao.

Alitoa onyo hilo kwa waandishi wa habari jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik.

Kauli hiyo imekuja baada ya mitandao ya jamii kuonyesha picha mbalimbali za video zilizosambazwa katika mitandao ya jamii zikiwaonyesha watu wakiwazomea wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokuwa wamevaa sare za chama hicho.

Alisema kitendo hicho cha kuzomea ni kibaya  kwa sababu  ni cha uchochezi na   kinaweza kuvuruga amani siku za usoni.

“Tuna ushahidi wa video hiyo inayosambazwa kwenye mitandao ya jamii ikiwaonyesha baadhi ya watu wakizomewa hadharani kama vile barabarani na sokoni jambo ambalo ni kinyume cha sheria na maadili ya siasa nchini.

“Kitendo kile ni cha uchochezi na ipo siku kitasababisha watu kupigana na kulipiza kisasi, hakikubaliki kisheria na hata katika jamii.

“Mtu kavaa sare za chama chake, kama wewe si mfuasi wake unakerwa na nini?  Katika kipindi hiki uvumilivu wa siasa unahitajika sana,” alisema.

Alisema  picha hiyo ya video inachunguzwa na    watu wanaoonekana wakitekeleza kitendo hicho watachukuliwa hatua. Wakati huo huo, Kamanda Kova alisema  polisi imejipanga kuimarisha ulinzi katika mikutano yote ya vyama vya siasa na hawahitaji msaada wa vikundi vya ulinzi wa vyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles