23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ufahamu ugonjwa wa Haemophilia

Na AVELINE KITOMARY, Dar es Salaam

HAEMOPHILIA ni ugonjwa usioambukiza unaotokana na damu kushindwa kuganda kutokana na kutokuwepo kabisa au upungufu wa chembechembe za protin ambazo inasababisha damu igande.

Mtu asipokuwa na hizo chembechembe akipata jeraha damu inatoka mda mrefu bila kukata hali hiyo huweza kusababisha kupoteza maisha.

Kwa kawaida mtu anapopata jeraha mishipa ya damu inatakiwa kusinyaa ili kupunguza utokaji wa damu kuelekea eneo lenye jeraha na kinachofuata baada ya mshipa wa damu kusinyaa zile chembe sahani za damu zinakusanyika kwa wingi katika eneo la jeraha ili kupungza damu kutoka.

Dakatri bingwa wa damu Stella Rwezaura akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa magonjwa ya damu

Baada ya hapo mwili unakuwa na uwezo wa kuzalisha chembecheme zingine kuanzia namba 12 hadi moja na kuweza kufanya kama simenti
Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Mgonjwa ya Damu Kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk Stella Rwezaura anasema uwepo wa chembe sahani (platelate) ndani ya mwili husaidia kuziba jeraha lisitoe damu.

“Iko hivi kwamba kama bomba limepasuka unaweka pale mchanga lakini mchanga hauwezi kuzuia damu kutoka inahitaji simenti ili izibe kwahiyo zile plate late ni kama simenti ambayo ndo inasaidia damu kugande kabisa ili aweze kupata nafuu.

“Lakini kwa mgonjwa wa haemophilia akipata jeraha mshipa wa damu utasinyaa,chembe sahani zitakusanyika kuziba kama kawaida lakini huyu mtu hana protini kwahiyo hana simenti ya kuziba hivyo damu itapungua kidogo na baadae itaendelea kuvuja mpaka apate njia ya kugandisha,”anaeleza Dk. Rwezaura.

JINSI HAEMOPHILIA INAVYOTOKEA
Heamophilia ni mshipa katika vina saba vyenye X- Chromosome ambayo inarithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia mama
Dk. Rwezaura anasema asilimia 30 ya wagonjwa wanapata kwa mabadiliko yasiyo ya kawaida ya vinasaba hata kama haijarithiwa kutoka kwa wazazi.

“Mama ambaye anavinasaba hivyo ananafasi ya kupata asilimia 25 ya watoto wake wa kike kuwa na chembechembe na asilimia 25 ya watoto wa kiume wenye chembechembe.

“Lakini baba mwenye Heamohpilia watoto wake wa kiume wote watakuwa hawana kwasababu atawapa Y –chromosome lakini wa kike watakuwa na chembechembe kwa sababu amewapa X- chromosome,”anabainisha.

Anasema mgonjwa ataishi na ugonjwa siku zote za maisha yake huku akikabiliwa na changamoto za kupoteza damu nyingi anapopata jeraha.“Mwingine anapata shida sehemu za ‘joint’ analala asubuhi akiamka anagunduka kuwa amevimba,hata wakati wa hedhi wagonjwa hawa wanapata tatizo,”anasema.

HALI ILIVYO NA HATUA ZINAZOCHUKULIW
Kutokana na uelewa na hamasa ndogo kuhusu gonjwa huu, Serikali imesema itaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuboresha huduma za matibabu kwa ugonjwa huo ikihusisha kubaini zaidi wagonjwa wenye ugonjwa huo nchini.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa watu wenye magonjwa ya damu uliofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Kwa niamba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii,Jinsi ,Wazee na Watoto idara ya magonjwa yasiyoambukiza Dk James Kihologwe anasema mradi huo pia utaboresha huduma za magonjwa wa haemophilia.

“Serikali kupitia wizara ya afya imekuwa ikiratibu miradi mbalimbali lengo lake ikiwa ni kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza miradi hiyo ni pamoja na ile ya kuwahudumia wagonjwa wa kisukari,saratani selimundu na kadhalika.

“Yapo baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanahitaji mikakati ikiwemo ugonjwa wa hemophilia kwa kutambua na kuona matokea chanya katika kupunguza vifo na madhara kwa wagonjwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanzisha mradi ambao unasaidia upatikana wa haraka huduma vipimo na matibabu kwa wagonjwa wa hemophili na selimundu.

“Serikali imekuwa ikiwezesha matibabu kwa magonjwa ya damu ambazo ni gharama kubwa ambapo serika li peke yake haiwezi kumudu na kuvifanyia ushirikiano na wadau wa sekta ya afya na binafsi,”anabainisha.
Anasema lengo la mradi huo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuwezesha upatianaji wa vipimo, wataalamu wa afya wabobezi na miundombinu sahihi ya matibabu kwa wagonjwa hao.

“Hii ni pamoja na kuanzisha kliniki za hemophilia na sick cell kwenye hospitali zote za rufaa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wabobezi wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Pamoja ya hayo mradi huo utaziwezesha hospitali za rufaa kuanzisha na kutoa huduma za mazoezi tiba kwa wagonjwa pamoja na mfumo maalum wa kugundua magonjwa hawa,”anaeleza.

Anasema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu walioko nchini ni wagonjwa 6,000 mpaka 12,000 na watoto 11,000 wa selimundu huzaliwa huku asilimia 97 ya watu wenye hemophilia Duniani hawajagundulika bado.
“Kwa upande wa Tanzania hadi sasa wagonjwa walitambulika na kuendelea na matibabu ni 127 tu hivyo uanzishwaji wa mradi huu utasaidia upatikanaji wa vipimo kwenye hospitali ya rufaa za mkoa na tunaamini wagonjwa wengi watagunduliwa na kuanzishwa matibabu.

Anaeleza kuwa mradi huo utaongeza kasi ya upatikanaji wa takwimu kwa wagonjwa wa haemophilia pamoja na kufanyika tafiti ,itaharakisha uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa pamoja na kuweka kwa ugonjwa huo katika mpango mkakati wa magonjwa yasiyoambukiza.

“Utahusisha ununuzi wa mashine wa kupimia wagonjwa hospitali za rufaa na kutoa mafunzo maalum ya vipimo hivyo na Mafunzo yatatolewa kwa madakatri wa meno,mifupa,upasuaji,wauguzi,wanasaikolojia,wazazi na watoto.
“Sisi kama serikali tumeanza kulewa sasa kuhusu ugonjwa huu na tumeelewa tumefikia watu wachache 167 katika ya 6000 tutaendelea kutoa elimu ili dalili ziweze kufahamika,”anasisitiza Dk Kihologwe.
CHANGAMOTO ZA WAGONJWA HAO
Akisimulia changamoto wanazopata wagonjwa hao Dk Rwezaura anasema yupo kijana ambaye aliwahi kufanyiwa tohara akiwa na miaka mitano hali iliyofanya kutokawa na damu kwa wiki mbili.
“Kijana wa miaka tisa alikuja tukamwona hapa kliniki alikuwa anatokwa damu tangu akiwa miezi sita na alifanyiwa tohara akiwa na miaka mitano alitokwa na damu kwa wiki mbili na alitolewa Mkoani akaletwa Muhimbili kwaajili ya kupata huduma.
“Baada ya vipimo tukagundua kuwa anahaemophilia lakini bahati mbaya mwaka huo huo mwezi mmoja kabla hatujakutana naye kliniki alipigwa na mwalimu shuleni maeneo ya bega kwahiyo mkono ulitoa damu kwasababu hiyo mkono wake ulianza kuwa mweusi alipewa rufaa ya kuja Muhimbili.
“Bahati nzuri alifika akahudumiwa vizuri uvimbe ukapungua lakini alipata ulemavu wa kukatwa mkono wa kushoto na bahati mbaya alikuwa anatumia mkono wa kushoto kuandika, licha ya kukatwa mkono alivimba goti la kushoto kwahiyo anaulemavu wa mguu pia,”anasimulia Dk Rwezaura.
Anasema kisa kingine ni cha mtoto wa miaka minne alianza kutokwa damu akiwa na mwaka mmoja na kupelekwa Muhimbili na kupata vipimo ambavyo vilionesha kuwa na haemophilia.
“Kwa wakati huo alikuwa anaishi na bibi yake lakini baadae alienda kuishi na mama yake ambaye baada ya kuona anaanza kuvimba akamkimbiza hospitali kwahiyo dakatri alivyoona goti limevimba akaona anahitaji upasuaji akamwingiza chumba cha upasuaji akapasue goti badaa ya hapo katokwa na damu wiki nzima akalazwa ICU wiki mbili hadi damu ilipopungua.
Anaeleza kuwa baada ya wiki tatu mtoto huyo alipelekwa ofisini kwake ambapo alibaini kuwa alifanyiwa upasujai kwenye goti lake kitu ambacho ni hatari kwa maisha yake.
“Kesi nyingine ni binti wa miaka 15 ambaye tumekuwa tukimuona tangu mwaka jana kila mwezi anatakiwa kuongezewa damu kwasababu akiingia hedhi anapoteza damu nyingi sana,”anaelza Dk Rwezaura.
WAHUDUMU WA AFYA WAELEWE HILI
Dk Rwezaura anasema uelewa mdogo kwa wahudumu wa afya unakuwa tatizo kwa wagonjwa wa heamophilia kutokana na kufanya upasuaji bila kujua hali ya mgonjwa.
“Uelewa mdogo ni tatizo utakuta dakatri anamdunga sindano kwenye misuli na kusababisha kuvimba na hii inaweza kuharibu mishipa ya fahamu ambapo hupelekea kupooza au stroke na kusababisha ulemavu wa kudumu.
“Hivyo ni muhimu wahuduma wa afya kama manesi na madaktari kujua kuuliza historia za wagonjwa au kama hajagundulika ni vizuri tatizo kama hilo linavyotokea mgonjwa awahishwe sehemu ambapo anaweza kupata huduma haraka huduma za haemophilia zinatolewa hospitali za kanda,Rufaa na Taifa,”anasisitiza.

WAGANGA WA JADI WAPEWA ELIMU
Dk Rwezaura anasema uelewa wa jamii bado ni mdogo kuhusu ugonjwa huo hivyo elimu zaidi inahitajika ili kuongeza kiwango cha uelewa.
Licha ya uelewa anasema mila na desturi pia ni hatari kwa watu wenye ugonjwa huo.

“Kuna mila na desturi za tohara bila kujua mnaweza kumpoteza mtoto, lakini mtoto akipewa rufaa kwasababu huku ni mbali wanachelewa kufika labda niwaambie sio kila daktari anaelewa kusuhu ugonjwa huo lakini wapo wachache waliobobea.
Anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa watu mbalimbali wakiwemo waganga wa kienyeji hii ni baada ya watu kupelekwa kwa waganga kuchanjwa hali ambayo inahatarisha maisha ya wagonjwa.

“Tulitoa mafunzo kwa waganga wa kienyeji na tuliwaomba kwamba kabla ya kumchanja mgonjwa apelekwwe hospitali au akiwa na uvimbe wasimchanje kwasababu anaweza kuwa na ugonjwa huo na akachanjwa baada ya hapo atapoteza damu nyingi.

“Wengine wanapoona kuwa wagonjwa hawa wanatokwa na damu wakafikiri amelogwa lakini kumbe ni ugonjwa tunawashauri wawalete hospitali kufanya vipimo.
“Na pia katika jamii, kwa wazazi,waalimu na walezi wengine wanawapeleka watoto hospitali na wanajua wanatatizo na bado wanaruhusu kufanyiwa upasuaji hii sio nzuri,”anasisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles