29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

UDEREVA WA DALADALA ULIVYOKATISHA NDOTO ZA GERVAS

Gervas Willium akiwa na mguu na baada ya kukatwa mguu

 

 

Na CHRISTINA GAULUHANGA DAR ES SALAAM

HUJAFA hujaumbika. Hivi ndivyo ninavyoweza kusema baada ya kijana Gervas William (27), kujikuta akipata ulemavu wa miguu bila kutarajia.

William alipata ulemavu baada ya kupata ajali ya gari iliyosababisha kukatwa mguu.

William ambaye anaishi Mbezi ya Kimara, alipoteza wazazi wake tangu akiwa mtoto.

Licha ya ulemavu alionao, anaamini kuwa si mwisho wa maisha yake.

Anasema mbali ya kuwa mlemavu, bado ana ndoto nyingi ambazo akipatiwa msaada wa mguu na elimu kutoka kwa wasamaria wema anaweza kuzitimiza.

Wiliam anasema baada ya wazazi wake kufariki, ndugu zake walijitolea kumsomesha ambapo alifanikiwa kupata elimu ya sekondari.

Anasema aliamua kujiunga na Chuo cha Ufundi Stadi cha Veta Chang’ombe kusomea ufundi magari.

William anasema alifaulu masomo hayo na kuamua kujiunga na masomo ya udereva na alipomaliza alipata kazi katika gereji za mitaani.

“Kwa kuwa tayari nilikuwa na mwanga wa maisha, niliamua kuanza kujitegemea na kujishughulisha na udereva hali ambayo ilinisaidia kujikwamua kimaisha na kuacha kuwa tegemezi,” anasema William.

Anasema ndoto zake ni kuhakikisha anapata kazi itakayomwezesha kumuingizia kipato kila siku ili aweze kumudu maisha.

William anasema kabla ya kuwa mlemavu alikuwa akiendesha daladala iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Makumbusho.

Anasema mbali ya jitihada hizo, alikuwa akiona maisha yanazidi kuwa magumu kwa kuwa kipato chake kilikuwa kidogo.

Wiliam anasema ilipofika mwaka 2014 aliona ni bora apate familia ambayo inaweza ikamsaidia mawazo, hivyo aliamua kuoa na walifanikiwa kupata mtoto mmoja.

Anasema kamwe hawezi kusahau siku ya Novemba 8, mwaka 2016 alipokuwa abiria katika gari namba T 914 BRG aina ya Coaster wakitokea Mbezi kwenda Buguruni, ambapo walipopata ajali eneo la Ubungo Maji iliyosababishwa akatwe mguu.

“Siwezi kuusahau kamwe mwaka huu kwani ndiyo uliochangia nipoteze malengo yangu yote…mbali ya kukosa uwezo wa kujiendeleza kielimu pia nimekosa maendeleo hali inayosababisha hata kushindwa uwezo wa kumsomesha mwanangu,” anasema William.

Gervas Willium akiwa na mtoto wake
Anaongeza: “Hakuna furaha ndani ya moyo wangu, kwani kila kukicha nikiangalia maisha yangu yalivyo siwezi kufanya lolote bila msaada wa watu. Mwanangu bado anahitaji nguvu zangu ili aweze kwenda mbele jambo ambalo nikilifikiria najikuta natokwa na machozi,” anasema Gervas.

Anasema baada ya kupata ajali hiyo alipelekwa hospitali za wilaya ambako alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini kwa sababu mguu uliharibika vibaya waliamua kuukata ili kuepusha maisha yake.

“Nakumbuka madaktari walijitahidi kunihudumia kadri ya uwezo wao lakini ilishindikana, sitasahahu pale ilipotoka ripoti kuwa ni lazima mguu ukatwe ili kuniepusha na kifo kwa sababu damu ilikuwa ikitoka nyingi mno,” anasema Gervas.

Anasema mara baada ya kupata matibabu aliruhusiwa na kurudi nyumbani na ndipo alipoanza kufuatilia haki zake.

“Cha ajabu tangu nilipoanza kuzunguka polisi ili niweze kupata haki yangu ya msingi ya kulipwa bima, hadi leo hakuna nilicholipwa zaidi ya kuzungushwa tu,” anasema Gervas.

Gervas anasema endapo atafanikiwa kupata msaada wa mguu bandia anaweza kujitahidi kujishughulisha na shughuli mbalimbali.

“Nina imani kuwa kukosa mguu si mwisho wa maisha, hivyo endapo nitapata msaada wa mguu na kupata watu wa kuniendeleza kielimu au kunipa mtaji nitajihidi kujikwamua katika hali ngumu niliyonayo hivi sasa,” anasema Gervas.

Gervas anaiomba Serikali kujitahidi kuiboresha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 kwani imekuwa chanzo cha ajali nyingi. 

Anasema ajali nyingi zinazotokea barabarani chanzo huwa ni uzembe.

Anasema kupwaya kwa sheria hiyo kumesababisha watu wengi kupata ulemavu wa kudumu huku wamiliki wa magari na madereva wakilipa faini ndogo na kutokomea zao kusikojulikana.

“Upungufu wa baadhi ya vipengere katika sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 unachangia kuleta kiburi kwa walimiki wa magari na madereva wao kwani wana amini kuwa wana uwezo wa kulipa faini ndogo iliyopo bila kufahamu athari wanazopata majeruhi au watu waliokufa katika ajali,” anasema Gervas.

Anasema zipo tafiti zinazoonyesha jinsi waathirika wa ajali wanavyoteseka kwa sababu ya umaskini na kushindwa kumudu maisha pindi wanapopata ulemavu wa kudumu.

Gervas anasema kuna umuhimu wa Serikali kuona haja ya kuanza kufanya maboresho ya sheria ya usalama barabarani ili kukomesha ajali za kizembe zinazotokea kila kukicha.

 Unaweza kuwasiliana na Gervas William kwa simu namba, +255 716 890 210 / +255 757 575 811 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles