LEO ni siku ambayo wanafunzi wa darasa la saba nchini kote, wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE).
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk. Charles Msonde idadi ya watahiniwa mwaka huu imeongezeka kwa kulinganishwa na mwaka jana.
Mwaka huu watahiniwa 917,072 watafanya mtihani huo wa siku mbili ikilinganishwa na mwaka jana ambako walikuwa watahiniwa 795,761.
Kama ilivyo kawaida, Baraza limetahadharisha na kuonya kuhusu vitendo vyovyote vya udanganyifu kwamba yeyote atakayegundulika atachukuliwa hatua kali.
Baraza limewaasa wasimamizi, watahiniwa, walimu, wamiliki wa shule na wananchi wote kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu na kwamba watahiniwa watakaobainika watafutiwa matokeo yao.
Limesema pia kuwa halitasita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha kuwa kuwapo kwake kunahatarisha usalama wa mitihani ya taifa
Siyo hayo tu, bali pia limesema: “Tunaamini kuwa walimu wamewaandaa wanafunzi vizuri hivyo, tunatarajia wataufanya mtihani huo kwa kuzingatia kanuni za mtihani ili matokeo yaonyeshe uwezo wao halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata”.
Hiyo ni tahadhari ya kutosha na ni matarajio kwamba wanaohusika, wakiwamo wanafunzi, walimu, wasimamizi na vituo, watazingatia.
Ni muhimu kuyazingatia hayo kwa sababu katika miaka iliyopita yamewahi kutokea matukio ya udanganyifu ambayo hufanywa na baadhi ya wanafunzi kwa kusaidiwa na walimu wao au wasimamizi wa mitihani.
Vitendo na udanganyifu wa aina hiyo ni wazi unarudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini na juhudi za kuliweka taifa hili katika uwiano unaotakiwa katika elimu, na mataifa mengine, wakiwamo majirani zetu.
Wanafunzi wanaofanya mitihani wanapaswa hatimaye waonekane wamepata elimu bora na siyo bora elimu ili waweze kumudu ushindani uliopo hivi sasa duniani na kwenda sambamba na maendeleo ya haraka ya sayansi na teknolojia.
Ieleweke kwamba elimu si jambo la kubabaisha, ni kitu kinachojidhihirisha wazi wakati wa utendaji.
Kwa maana kwamba, mtu ambaye atakuwa amepata elimu yake kwa ujanjaujanja na udanganyifu lazima utendaji kazi wake utakuwa na walakini na upungufu mkubwa ikilinganishwa na mtu ambaye atakuwa ameipata elimu yake kwa halali.
Kwa sababu hiyo tunawatakia mtihani mwema na usio na udanganyifu wanafunzi wanaomaliza darasa la saba mwaka huu waweze kuwa mabalozi na wawakilishi wazuri wa nchi hii katika masuala ya elimu na maendeleo.